Wizara ya Fedha yawakaribisha wawekezaji kuwekeza katika Sekta ya Afya nchini

NAIROBI-Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) amewakaribisha wawekezaji kuwekeza katika sekta ya afya Tanzania, akisema nchi ina sera thabiti zinazotabirika pamoja na mazingira salama na rafiki kwa uwekezaji.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), Mhe. Luswetula ametoa mwaliko huo wakati akichangia hoja katika Jukwaa la Mazungumzo ya Ngazi za Juu la Mawaziri wa Fedha kuhusu kuimarisha uwekezaji wa pamoja katika sekta ya afya, lililofanyika katika Hoteli ya JW Marriott, Nairobi, Kenya.

“Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya afya, pamoja na sera imara na zinazotabirika zinazoambatana na mazingira bora ya uwekezaji na usalama. Kinachohitajika ni kufuata sheria za nchi ili uwekezaji uwe na manufaa kwa mwekezaji na Watanzania kwa ujumla,”amesema Mhe. Luswetula.

Akizungumzia mkutano huo, Mhe. Luswetula amesema,majadiliano katika jukwaa hilo yalilenga kujadili mikakati ya kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia huduma za afya, utekelezaji wa ahadi za pamoja za ufadhili pamoja na kuweka sera na mazingira wezeshi yatakayochochea uwekezaji katika sekta hiyo.
Amesema kuwa, Tanzania imepiga hatua katika kuweka mazingira yanayowezesha upatikanaji na utoaji wa huduma bora za afya, hatua ambayo inatoa fursa zaidi kwa sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya sekta hiyo.

Aidha, amesema Tanzania imeendelea na utekelezaji wa programu ya Bima ya Afya kwa Wote, huku Serikali ikiwekeza kwa kiasi kikubwa katika eneo hilo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya nchini.

Amesema,uwepo wa mfumo mpana wa bima ya afya unatarajiwa kuwa na mchango katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya na kuwawezesha wananchi kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli zao za maendeleo.

Vilevile amesema kuwa, majadiliano hayo yalihusu matumizi ya mbinu bunifu za ufadhili na mifumo ya kuchanganya vyanzo mbalimbali vya fedha ili kuongeza rasilimali zinazohitajika katika kuboresha huduma za afya.
Mkutano huo uliowakutanisha Mawaziri wa Fedha kutoka nchi mbalimbali za Afrika zilizosaini Hati za Makubaliano (MoU) na Serikali ya Marekani kuhusu ufadhili wa sekta ya afya ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu wa Hazina ya Marekani anayeshughulikia Masuala ya Kimataifa, Bi. Erin Browne pamoja na viongozi na maafisa mbalimbali kutoka nchi shiriki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here