ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, Zanzibar iko tayari kuimarisha ushirikiano na Shirikisho la Urusi katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo nishati, bandari na usafirishaji, utalii, elimu na utafiti, afya na Uchumi wa Buluu.
Ameyasema hayo leo Septemba 28,2026 alipokutana na ujumbe kutoka Shirikisho la Urusi ulioongozwa na Bw. Denis Agafonov, Mkuu wa Kurugenzi ya Wataalamu katika Ofisi ya Rais wa Shirikisho la Urusi na ujumbe wake waliofika Ikulu Zanzibar.
Rais Dkt.Mwinyi amesema, Zanzibar inalenga kutumia fursa za ushirikiano na Urusi katika uwekezaji, teknolojia, utalii, nishati, uvuvi, tafiti za pamoja na maendeleo ya Uchumi wa Buluu, huku akisisitiza umuhimu wa kugeuza maeneo yaliyojadiliwa kuwa miradi yenye matokeo yanayoonekana.
Naye Bw. Denis Agafonov amesema, Urusi iko tayari kuendelea kujadiliana na Zanzibar kuhusu maeneo yenye fursa za ushirikiano na uwekezaji.





