MWANZA- Katika hatua muhimu ya kukuza elimu ya fedha nchini, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesaini hati tatu za makubaliano ya ushirikiano na taasisi mbalimbali, kwa lengo la kuongeza uelewa wa masuala ya kifedha na kujenga uwezo wa wananchi na wataalamu katika usimamizi wa fedha.
Makubaliano hayo yamesainiwa tarehe 29 Oktoba 2026 kupitia Chuo cha Benki Kuu jijini Mwanza, yakihusisha Benki Kuu ya Madagascar, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chama cha Wafanyakazi Wakusanya Mapato Tanzania (TAREWU).
Utoaji saini wa hati hizo umefanyika kwa kushirikisha viongozi wa taasisi husika, akiwemo Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, na Gavana wa Benki Kuu ya Madagascar, Bw. Aivo Handriatiana Andrianarivelo. Viongozi wengine walioshiriki ni Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. William Anangisye, Katibu Mkuu wa TAREWU, Bw. Michael Marere, pamoja na Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu, Tawi la Mwanza, Dkt. Nicas Yabu.
Akizungumzia umuhimu wa ushirikiano huo, Gavana Tutuba amesema elimu ya fedha ni nyenzo muhimu katika kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi, akiba na uwekezaji. Ameeleza kuwa, kupitia makubaliano hayo, wananchi wanatarajiwa kunufaika na maarifa yatakayowawezesha kuelekeza rasilimali zao katika shughuli za kiuchumi zenye tija, zinazochangia ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa ajira.
Naye Prof. Anangisye ameeleza utayari wa UDSM kuendelea kushirikiana na BoT katika kuendeleza elimu ya usimamizi wa fedha. Amesema chuo hicho kina wataalamu wenye ujuzi na uzoefu katika masuala ya uchumi ambao wanaweza kutoa mchango muhimu katika kufanikisha malengo ya ushirikiano huo.
Kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali pamoja na programu za uhamasishaji wa elimu ya fedha kwa umma, BoT inalenga kuongeza uelewa wa masuala ya fedha na kuwajengea wananchi uwezo wa kutumia fursa za kifedha kwa manufaa yao binafsi na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Tags
Benki Kuu ya Madagascar
Benki Kuu ya Tanzania
BoT
Chuo cha Benki Kuu Mwanza
Elimu ya Fedha
Emmanuel Tutuba
Habari
TAREWU
UDSM






