HESLB yatoa mikopo ya Awamu ya Pili kwa wanafunzi 90,235

DAR ES SALAAM- Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Jumatano Oktoba 21, 2026 imetangaza awamu ya pili ya orodha ya wanafunzi 90,235 wenye sifa ambao wamepangiwa mikopo na ruzuku yenye thamani ya TZS 284.73 bilioni kwa ajili ya mwaka wa masomo 2026/2027.
Orodha ya wanufaika iliyotangazwa inajumuisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanaendelea na masomo walioahiliwa katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu na vyuo vya kati.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Dkt. Bill Kiwia.

Wanafunzi 25,630 wa Shahada ya awali wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 82.31 bilioni, wanafunzi 3,445 wa Stashahada (Diploma) wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 9.25 bilioni.

Pia, wanafunzi 417 wa Stashahada ya Juu ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (Postgraduate Diploma in Legal Practice) wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 1.04 bilioni.

Aidha, wanafunzi 6,225 wanaendelea na masomo wamepangiwa mikopo kwa mara ya kwanza yenye thamani ya TZS 20.38 bilioni na wanufaika wa Ngorongoro Scholarship wamepangiwa ruzuku yenye thamani ya TZS 66 milioni.

Orodha hiyo pia inajumuisha wanufaika wa mikopo wanaoendelea na masomo wakiwemo wanafunzi 47,670 wa shahada ya awali ambao wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 153.16 bilioni na wanafunzi 6,834 wa stashahada ambao wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 18.50 bilioni.

Wanufaika waliopangiwa mikopo

Orodha ya awamu ya pili, inafanya idadi ya jumla ya wanafunzi 256,010 ambao wamepangiwa mikopo na ruzuku katika awamu ya kwanza na awamu ya pili yenye thamani ya TZS 820.4 bilioni.

Hatua zinazofuata

Bodi imekamilisha upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza. Hata hivyo, wanafunzi ambao bado hawajapangiwa mikopo na wana taarifa za ziada kuwezesha kukata rufaa, wanashauriwa kufanya hivyo kuanzia tarehe 25 Oktoba, 2026 dirisha la rufaa litakapofunguliwa.

Jedwali la mgawanyo wa mikopo Awamu ya Pili
Kundi la WanafunziIdadi ya WanufaikaThamani ya Mikopo (TZS)
Shahada ya Awali (Mwaka wa 1)25,630Bilioni 82.31
Stashahada / Diploma (Mwaka wa 1)3,445Bilioni 9.25
Wanasheria kwa Vitendo (Law School)417Bilioni 1.04
Wanaendelea na Masomo (Wapya)6,225Bilioni 20.38
Shahada ya Awali (Wanaendelea)47,670Bilioni 153.16
Stashahada / Diploma (Wanaendelea)6,834Bilioni 18.50
Ngorongoro Scholarship (Ruzuku)-Milioni 66.00
JUMLA KUU (AWAMU YA PILI)90,235Bilioni 284.73

"Tunaendelea kupanga ruzuku kwa wanafunzi wapya wa Samia Scholarship na wanafunzi wanaoendelea na masomo watapangiwa mikopo katika awamu zijazo kwa kadri tunavyopokea matokeo kutoka vyuoni."

HESLB imewakumbusha waombaji wa mikopo na ruzuku wenye sifa kwa mwaka wa masomo 2026/2027 ambao bado hawajapangiwa mikopo au ruzuku, kuendelea kufuatilia taarifa za maombi yao kupitia 'SIPA' wakati taratibu za uchambuzi na upangaji wa mikopo na ruzuku zikiendelea.
Taarifa ya Bodi ya Mikopo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. jamani mbona wengine acount zetu zinasoma verification passed hii ina maana gani au ndio tumekosa mkopo kwa mwaka huu hamna awamu nyingine

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here