DODOMA-Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Dodoma leo Oktoba 6, 2026 imewapatia mafunzo maalum wataalamu kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) juu ya matumizi ya kifaa cha kisasa cha kupima usahihi wa mita za maji majumbani bila kulazimika kuzifungua, kinachojulikana kama Portable Water Meter Test Kit.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wataalamu wa DUWASA kuhakikisha kila dira ya maji inayosoma matumizi ya mteja nyumbani inatoa usomaji sahihi, hivyo kuzuia upotevu wa maji usio wa lazima.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wataalamu wa DUWASA kuhakikisha kila dira ya maji inayosoma matumizi ya mteja nyumbani inatoa usomaji sahihi, hivyo kuzuia upotevu wa maji usio wa lazima.Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Vipimo kutoka WMA Mkoa wa Dodoma, Ndugu Masanja Nilla, amesema moja ya njia madhubuti ya kuzuia upotevu wa maji ni kuhakikisha mita zote za maji zinafanyiwa uhakiki na kupima kwa usahihi.
"Kifaa hiki ni muhimu sana kwa sababu kina uwezo wa kupima usahihi wa mita ya maji ikiwa bado imefungwa nyumbani kwa mteja. Hakuna haja ya kuifungua. Kama mita inapima pungufu au zaidi, itaonekana hapo hapo," alisema Nilla.
Naye Meneja wa WMA, Mkoa wa Dodoma, Bw. Saidi Ibrahim ameongeza kuwa matumizi sahihi ya kifaa hicho yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia upotevu wa maji, kuongeza mapato ya Serikali kupitia malipo sahihi ya ankara za maji, na kupunguza malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wananchi wanaolalamikia bili kubwa za maji wakati matumizi ni kidogo.
Kwa upande wao, wataalamu wa DUWASA wameishukuru WMA kwa mafunzo hayo na kueleza kuwa yatawasaidia kuboresha huduma zao na kujenga imani kwa wateja wao.
Mafunzo haya ni sehemu ya jukumu la msingi la Wakala wa Vipimo la kutoa elimu na kusimamia matumizi ya vipimo sahihi katika sekta zote muhimu ikiwemo sekta ya maji, ili kulinda maslahi ya mlaji na mtoa huduma.


