NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kufuta leseni ya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni iliyokuwa imetolewa kwa kampuni ya Farizal Forex Bureau Limited, baada ya kubainika kuwa kampuni hiyo imekiuka masharti ya leseni pamoja na matakwa ya sheria inayosimamia biashara hiyo.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel M. Tutuba.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi wa kufuta leseni hiyo umetokana na mamlaka aliyopewa Gavana kupitia Sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992, na Kanuni namba 40 ya Kanuni za Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni za Mwaka 2023.
Leseni hiyo yenye namba BCL Na. 0602-00 imefutwa kuanzia tarehe 5 Oktoba 2026.
Benki Kuu imeeleza kuwa, imechukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa kampuni hiyo imekiuka vigezo na masharti ya leseni ya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni, pamoja na matakwa ya Sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 na kanuni zake.
Kutokana na uamuzi huo, kuanzia tarehe tajwa, Farizal Forex Bureau Limited hairuhusiwi tena kufanya biashara yoyote ya kubadilisha fedha za kigeni kwa kutumia leseni iliyofutwa.
Benki Kuu imewataka wananchi kuzingatia taarifa hiyo na kuepuka kufanya miamala na kampuni hiyo, huku ikisisitiza kuwa inaendelea kuhakikisha inalinda maslahi ya watumiaji wa huduma za kubadilisha fedha za kigeni.
Aidha, Benki Kuu imesema inaendelea kusimamia kwa karibu maduka yote ya kubadilisha fedha za kigeni nchini ili kuhakikisha yanazingatia sheria na kanuni zinazosimamia biashara hiyo.
Tags
Benki Kuu
Benki Kuu ya Tanzania
BoT
Farizal Forex Bureau
Fedha za Kigeni
Habari
Leseni
Tanzania

