Makamu wa Rais Ndejembi afungua mkutano wa wabunge wanawake maziwa makuu Dar

DAR ES SALAAM- Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, Novemba 2, 2026, amefungua rasmi Mkutano wa Wabunge Wanawake wa Jukwaa la Mabunge la Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR), kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akihimiza wanawake kushiriki kikamilifu katika kuzuia migogoro, upatanishi na maamuzi ya amani na usalama.
Mkutano huo unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, kuanzia Novemba 2 hadi 5, 2026, umewakutanisha wabunge wanawake, maspika wa bunge na viongozi wa taasisi, kikanda, mashirika na wadau wa maendeleo kutoka nchi 12 za Ukanda wa Maziwa Makuu, ukiwa na kaulimbiu isemayo “Kwa amani na maendeleo ya Ukanda wa Maziwa Makuu.”

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mhe. Ndejembi amesema ushiriki wa wanawake katika masuala ya amani na usalama ni msingi wa kujenga amani endelevu, demokrasia na maendeleo jumuishi. Ameeleza kuwa wanawake huathirika zaidi na migogoro, licha ya mara nyingi kutoshirikishwa katika maamuzi ya kutafuta suluhu.
Amesema, Tanzania imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha ushiriki wa wanawake kupitia Mpango Kazi wa Taifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama (NAP-WPS) wa mwaka 2025–2029, uliozinduliwa Agosti 2025, unaolenga kutekeleza Azimio Na. 1325 la Umoja wa Mataifa. Mpango huo unalenga kuongeza ushiriki na uongozi wa wanawake katika michakato ya amani, usalama na ujenzi upya wa jamii.
Aidha, amezihimiza nchi wanachama kuimarisha ushirikiano, kuheshimu mamlaka na mipaka ya kila nchi na kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo badala ya matumizi ya silaha. Pia amesisitiza umuhimu wa kuwapa wanawake nafasi na ushawishi wa kweli katika kujenga amani ya kikanda.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azan Zungu, amesema Tanzania imepiga hatua katika ushirikishwaji wa wanawake Bungeni, ambapo hadi mwaka 2025, wanawake walikuwa asilimia 39 ya wabunge wote, huku kamati saba za kudumu za Bunge zikiongozwa na wanawake

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here