OTR yasisitiza uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa uwekezaji wa Serikali

NA GODFREY NNKO

OFISI ya Msajili wa Hazina (OTR) imesisitiza umuhimu wa uwazi, uwajibikaji na utawala bora katika usimamizi wa mali na uwekezaji wa Serikali.
Imebainisha kuwa, misingi hiyo ni muhimu katika kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa tija na kuleta manufaa kwa Watanzania.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa OTR, Bw. Sabato Kosuri ameyasema hayo leo Novemba 2, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi kati ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), wahariri na waandishi wa habari, kilichoandaliwa chini ya uratibu wa OTR.

Amesema, jukumu la OTR ni kusimamia mali na uwekezaji wa Serikali katika taasisi na mashirika ya umma ili kuhakikisha rasilimali hizo zinatumika ipasavyo na kuleta matokeo yanayokusudiwa kwa manufaa ya taifa.

Bw. Kosuri amesema, utekelezaji wa jukumu hilo unahitaji kuwepo kwa mifumo imara ya utawala bora na uwajibikaji, huku uwazi ukiwa nguzo muhimu ya kuimarisha usimamizi wa mali za umma.

Ameeleza kuwa, ushirikishwaji wa wananchi katika kutoa maoni na mapendekezo kuhusu usimamizi wa uwekezaji wa Serikali ni muhimu, kwa kuwa taasisi na mashirika hayo ni mali ya Watanzania.

Pia, amesisitiza kuwa, viongozi na watendaji waliokabidhiwa dhamana ya kusimamia rasilimali hizo wana wajibu wa kuhakikisha uwekezaji wa umma unaleta tija, huku wananchi wakipewa nafasi ya kuchangia mawazo yatakayosaidia kuboresha usimamizi wake.

Akizungumzia malengo ya maendeleo ya taifa, Bw. Kosuri amesema, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kujenga uchumi wenye thamani ya dola trilioni moja, jambo linalohitaji kuimarisha ushindani wa uchumi na kuhakikisha makundi mbalimbali yanashiriki katika mchakato wa maendeleo.

Ameitaja TISEZA kuwa taasisi yenye nafasi ya kimkakati katika kufanikisha azma hiyo kupitia uratibu, uwezeshaji na uhamasishaji wa uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Vilevile, amesema mamlaka hiyo ina mchango muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia mitaji katika sekta mbalimbali, hususan maeneo ya viwanda na maeneo maalum ya kiuchumi, hatua inayoweza kuongeza ushindani na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Bw. Kosuri ameongeza kuwa, kikao kazi hicho ni fursa kwa wahariri na waandishi wa habari kufahamu kwa kina majukumu ya TISEZA, mchango wake katika kukuza uwekezaji na namna inavyoshiriki katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amefafanua kuwa, mkutano huo umeandaliwa kwa mfumo wa semina ili kutoa nafasi kwa washiriki kujifunza, kujadiliana na kuuliza maswali kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu shughuli na fursa za uwekezaji nchini.

Aidha, amewahimiza waandishi wa habari kutumia nafasi yao kuutangaza ulimwengu fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania, huku wakiwafahamisha wananchi kuhusu fursa mbalimbali zinazoweza kuchangia maendeleo ya kiuchumi.

Amesema, vyombo vya habari vina jukumu muhimu la kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu mazingira ya uwekezaji nchini, hivyo kusaidia kuvutia wawekezaji na kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here