Rais Samia asisitiza haki, usawa katika utatuzi wa migogoro ya kazi

DODOMA- Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameitaka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi kutatua migogoro ya kazi kwa usawa, ikizingatia sheria na kulinda haki za wafanyakazi na waajiri.
Rais Dkt. Samia amesema hayo leo Novemba 2, 2026, katika hafla ya uapisho wa viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Amesisitiza kuwa maamuzi ya migogoro ya kazi yazingatie makosa yaliyothibitishwa bila kujali nafasi au utambulisho wa mtu, "ili kulinda haki za wafanyakazi na waajiri," hususan katika zama hizi ambapo shughuli za sekta binafsi nchini zinaendelea kupanuka.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu na kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na utendaji wa taasisi za umma.

Aidha, ameitaka Tume hiyo kulinda maslahi ya nchi kwa kufuatilia nafasi ya Tanzania kimataifa katika masuala ya utawala bora na kutoa ufafanuzi kwa wakati.
Rais Dkt. Samia pia amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora kusimamia matumizi ya fedha, utekelezaji wa miradi ya Serikali na utatuzi wa kero za wananchi wa Mkoa huo.

Walioapishwa ni Mhe. Angeline Lubala Mabula kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora; Ndugu Dunford George Mpelumbe kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; na Ndugu Omar Ali Omar Bhai kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Wengine ni Jaji Mstaafu Wilfred Peter Dyansobera kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, pamoja na Makamishna sita wa Tume hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here