NA GODFREY NNKO
MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umewekeza Shilingi bilioni 1.84 hadi Juni 2025 katika kuboresha upatikanaji wa teknolojia kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kukuza elimu jumuishi na kupunguza pengo la kidijitali nchini.
Kupitia uwekezaji huo, jumla ya shule 22 katika mikoa 18 zimefikiwa na mpango wa elimu jumuishi kwa kupewa vifaa maalumu vya kiteknolojia vinavyowawezesha wanafunzi wenye ulemavu wa kuona kupata fursa ya kujifunza kwa kutumia teknolojia.
Aidha, walimu 5,094 wa shule za umma wamepatiwa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), huku wasichana 1,581 wa shule za sekondari nao wakinufaika na programu za kuwajengea uwezo katika matumizi ya teknolojia.
Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji, Utafiti na Maendeleo wa UCSAF, Mhandisi Albert Richard ameyasema hayo Novemba 3, 2026 jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao kazi kati ya mfuko huo, wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR).
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Richard amesema, hadi Oktoba 2026, jumla ya shule 1,167 za umma zilikuwa zimenufaika na mipango mbalimbali ya mfuko huo, ikiwemo miradi inayolenga kupanua matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu.
Afisa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Alex Malanga akiongoza kikao kazi kati ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), wahariri na waandishi wa habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR).Shule zilizofikiwa na mradi wa elimu jumuishi zipo katika mikoa mbalimbali nchini zikiwemo Mpwapwa mkoani Dodoma, Mkolani na Bwiru Boys mkoani Mwanza, Kashaulili mkoani Katavi, Morogoro na Kilosa mkoani Morogoro, Shinyanga mkoani Shinyanga na Songea Boys mkoani Ruvuma.
Shule nyingine ni Kazima mkoani Tabora, Haile Selassie na Alli Mohamed Shein Mjini Magharibi, Patandi Maalum mkoani Arusha, Rugambwa Girls mkoani Kagera, Jambiani na Jendele Kusini Unguja, Kyela mkoani Mbeya.
Nyingine ni Njombe Viziwi mkoani Njombe, Balangdalalu mkoani Manyara, Mtwara Ufundi mkoani Mtwara, Kantalamba mkoani Rukwa, Moshi Secondary mkoani Kilimanjaro na Pujini Secondary Kusini Pemba.
Miongoni mwa vifaa vilivyotolewa katika shule hizo ni mashine za Braille, Orbit Readers, vifaa vya kuchapisha maandishi ya nukta nundu (Embosser) pamoja na vifaa vingine saidizi vinavyolenga kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu wa kuona kupata na kutumia taarifa za kielimu kwa urahisi zaidi.
Shule 10 zaidi kuingizwa kwenye mpango
Kwa mwaka wa fedha 2026/27, shule nyingine 10 zimepangwa kuingizwa katika mpango huo.
Shule hizo ni Musoma Tech mkoani Mara, Mustafa Sabodo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Malangali mkoani Iringa, Old Bendera mkoani Kilimanjaro, Buhongwa Secondary mkoani Mwanza, Mlingano mkoani Tanga, Kantalamba mkoani Rukwa, Mubaba mkoani Kagera, Tanga Tech katika Halmashauri ya Manispaa ya Tanga na Kigoma Girls mkoani Kigoma.
Walimu 5,094 wanufaika wa mafunzo ya TEHAMA
Mhandisi Richard amesema, katika eneo la kujenga uwezo wa walimu, UCSAF imegharamia mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 5,094 wa shule za umma tangu mwaka wa fedha 2016/17.
Kati yao, walimu 4,533 wanatoka Tanzania Bara na 561 kutoka Zanzibar, hatua inayolenga kuongeza ujuzi wa kutumia teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji.
Aidha, kwa mwaka wa fedha 2026/27, mfuko huo umepanga kutoa mafunzo kwa walimu wengine 692, wakiwemo 592 kutoka Tanzania Bara na 100 kutoka Zanzibar.
Katika kundi hilo, walimu 100 wa elimu maalumu pia watajumuishwa ili kuongeza uwezo wao wa kutumia teknolojia katika kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Sambamba na mafunzo kwa walimu, UCSAF kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kutekeleza programu ya kuwawezesha wasichana kushiriki kikamilifu katika matumizi ya TEHAMA kupitia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Girls in ICT Day), yanayofanyika kila mwaka mwezi Aprili.
Amesema, kupitia programu hiyo, wasichana 1,581 kutoka shule za sekondari za umma wamepatiwa elimu na ujuzi kuhusu matumizi ya teknolojia.
Kwa mwaka wa fedha 2026/27, UCSAF inalenga kuwafikia wasichana 440 kutoka shule za msingi na sekondari, vyuo pamoja na makundi ya wenye ulemavu (PDW).
Mafunzo hayo yanatarajiwa kutolewa kupitia vituo vitano vilivyopo Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na Zanzibar.
Vituo 17 vya intaneti ya bure vimefunguliwa
Katika jitihada za kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano, UCSAF pia imefungua vituo 17 vinavyotoa huduma ya intaneti ya bure katika maeneo mbalimbali nchini.
Mhandisi Richard amesema, maeneo yaliyofikiwa ni pamoja na viwanja vya maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam, Nyerere Square na Chuo Kikuu cha Dodoma (CIVE) mkoani Dodoma, Soko la Nyamagana jijini Mwanza, Kiembesamaki Zanzibar, Soko la Tabora na Chuo cha Mafunzo cha Lungemba kilichopo Mafinga.
Aidha, kupitia mradi wa mwaka wa fedha 2024/25, vituo 25 vya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT-DART) vinatarajiwa kuunganishwa na huduma ya intaneti kwa gharama ya Shilingi milioni 500.
Kwa upande mwingine, katika mwaka wa fedha 2025/26, maeneo mengine 60 yaliyopo Tanzania Bara na Zanzibar yamepangwa kuunganishwa na huduma hiyo ili kuongeza fursa za wananchi kupata taarifa na kutumia huduma za kidijitali.
Ofisi 10 za halmashauri kuunganishwa na mkongo wa taifa wa mawasiliano
Pia, amesema katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano katika ngazi za Serikali za Mitaa, UCSAF pia inatekeleza mradi wa kuunganisha ofisi 10 za halmashauri na mkongo wa taifa wa mawasiliano ya intaneti ya kasi kupitia teknolojia ya nyuzi za mawasiliano (faiba).
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha ofisi hizo zinapata huduma ya intaneti yenye uhakika na hivyo kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema, zoezi la kutambua maeneo yatakayohusika na mradi huo limekamilika, huku mchakato wa kumpata mkandarasi kwa ajili ya utekelezaji ukiendelea.
UCSAF imesisitiza kuwa, itaendelea kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na wadau wengine kuhakikisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na teknolojia unapanuka katika maeneo mbalimbali nchini.
Juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi wa kidijitali na kuhakikisha makundi yote ya wananchi, wakiwamo watu wenye ulemavu, wanawake, wasichana na jamii zilizo katika maeneo yenye changamoto za mawasiliano, yanapata fursa sawa za kunufaika na maendeleo ya teknolojia.
Uhakika wa Intaneti na Simu
Wakati huo huo, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imetangaza mkakati thabiti wa kuboresha miundombinu ya mawasiliano ya simu na mtandao wa intaneti katika maeneo mbalimbali nchini, ikijumuisha reli ya mwendokasi (SGR), Reli ya Kati (MGR) na reli ya TAZARA.
Mhandisi Richard amesema, mfuko huo unalenga kukamilisha uboreshaji wa mawasiliano ya intaneti na simu kwa watoa huduma wote katika kipande cha SGR kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma.
Hatua hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja ili kutatua kero ya kukatika kwa mawasiliano inayowakabili abiria wanapokuwa safarini.
"Tumedhamiria kuhakikisha wasafiri wanapata huduma bora na ya uhakika ya mawasiliano bila usumbufu wowote kuanzia safari inapoanza hadi mwisho,"amesema Mhandisi Richard.
Kuhusu maeneo mengine ya kimkakati, Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa, kupitia mradi wa Awamu ya 11A, UCSAF itaimarisha huduma katika maeneo 198 nchini.
Maeneo hayo yanajumuisha mipakani, hifadhi za taifa, pamoja na njia za reli ya zamani (MGR) na TAZARA.
Ofisi ya Msajili wa Hazina
Wakati huo huo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), Bw. Sabato Kosuri amewataka wahariri na waandishi wa habari nchini kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu, uwekezaji na mchango wa taasisi na mashirika ya umma katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Amesema, Ofisi ya Msajili wa Hazina ina jukumu muhimu la kusimamia mali na uwekezaji wa Serikali unaomilikiwa kwa niaba ya wananchi, hivyo ni muhimu kuwepo kwa ushirikiano kati ya taasisi hizo na vyombo vya habari ili kuhakikisha umma unafahamu shughuli zinazotekelezwa, wajibu wa kila taasisi pamoja na namna zinavyowajibika.
Bw. Sabato ameeleza kuwa, OTR inasimamia taasisi na mashirika ya umma 308, ambazo zina wajibu wa kutumia rasilimali na mitaji iliyowekezwa na Serikali kwa ufanisi ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Amesema, kikao hicho ni sehemu ya jitihada za kujenga utamaduni wa mawasiliano ya wazi kati ya taasisi za umma na vyombo vya habari, badala ya kusubiri hadi changamoto au kasoro zijitokeze ndipo taasisi husika zitoe ufafanuzi kwa umma.
Pia, amesema kwa muda mrefu taarifa nyingi zilizohusu baadhi ya mashirika na kampuni za umma zilizokuwa zikipewa nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari zilihusu hoja za ukaguzi, ubadhirifu, upotevu wa mali za Serikali na matumizi mabaya ya madaraka.
Hata hivyo, amesema OTR imeona umuhimu wa kubadili utaratibu huo kwa kuanzisha mazungumzo ya mara kwa mara na wahariri na waandishi wa habari ili kutoa nafasi ya kueleza mafanikio, changamoto na mipango ya taasisi hizo, huku ikipokea ushauri na kukosolewa pale inapobidi.
Amesisitiza kuwa, ushirikiano huo unapaswa kujengwa katika misingi ya mazungumzo, uwazi, ushauri na uwajibikaji, akibainisha kuwa lengo si kuzuia vyombo vya habari kutekeleza wajibu wake wa kukosoa, bali kuimarisha uelewa wa umma kuhusu shughuli za taasisi za Serikali na mchango wake katika maendeleo ya nchi.
Akizungumzia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Bw. Kosuri amesema, mfuko huo haupaswi kutazamwa kama taasisi inayojihusisha na ujenzi wa minara ya mawasiliano pekee, bali kama chombo cha kimkakati kinachochangia ukuaji wa uchumi.
Vilevile, kuchangia ustawi wa jamii na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi, hususan wanaoishi katika maeneo ya vijijini na yasiyovutia wawekezaji wa sekta binafsi.
Ameeleza kuwa, kupitia uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano, UCSAF imekuwa na nafasi muhimu katika kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma hizo kati ya maeneo ya mijini na vijijini, hivyo kuwawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia.
Bw. Kosuri amesisitiza kuwa, upatikanaji wa mawasiliano una mchango mkubwa katika kurahisisha huduma za kifedha, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali na huduma za kutuma na kupokea fedha, ambazo zimekuwa zikiboresha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Aidha, amesema miundombinu hiyo inafungua fursa za ajira na kujiajiri kwa vijana kupitia matumizi ya teknolojia, huku ikiwezesha wananchi kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali za biashara kwa kutumia huduma za kidijitali.
Mkuu huyo wa Mawasiliano ameongeza kuwa, Tanzania inapojipanga kujenga uchumi imara, shindani na jumuishi, haiwezi kupuuza nafasi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kwa kuwa ni moja ya nguzo muhimu zinazowezesha uchumi wa kisasa na kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji na utoaji huduma.
Amesema, maendeleo ya uchumi yanahitaji miundombinu madhubuti itakayowawezesha wananchi, wajasiriamali na wawekezaji kupata taarifa, kuwasiliana na kutumia teknolojia katika kuboresha shughuli zao za kila siku.
Hivyo, kutokana na umuhimu huo, amewahimiza wahariri na waandishi wa habari kutumia fursa ya kikao hicho kuelewa kwa kina majukumu na utekelezaji wa UCSAF, ili waweze kufikisha kwa wananchi taarifa sahihi kuhusu huduma na fursa zinazopatikana kupitia mfuko huo.
Bw. Sabato amesema ni muhimu wananchi kuelimishwa kuhusu namna wanavyoweza kutumia miundombinu na huduma za mawasiliano zilizowezeshwa na Serikali ili kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Tags
Braille
Elimu Jumuishi
Habari
Mpwapwa
Njombe Viziwi
Orbit Readers
Patandi Maalum
Shule za Mahitaji Maalumu
UCSAF











