Walimu wapatiwa hati za viwanja, Waziri Mabula awapa mbinu za kupiga hatua

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dokta Angeline Mabula ametoa hati 315 kwa walimu wa shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya Ilemela ikiwa ni juhudi zake za kuhakikisha walimu wa manispaa hiyo wanamilikishwa ardhi kwa gharama nafuu, anaripoti Munir Shemweta, WANMM...

Walimu waliopatiwa hati za viwanja ni sehemu ya walimu 525 walioomba kupatiwa viwanja katika eneo la Nyamiswi Manispaa ya Ilemela ambapo wengine walishindwa kukamilisha malipo ya viwanja hivyo.

Akizungumza wakati wa kugawa hati hizo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari za Manispaa ya Ilemela, Dokta Mabula mbali na kuwapongeza walimu hao kwa kukamilisha malipo hadi kumilikishwa ardhi na kuwataka kuzitumia hati hizo kwa shughuli za maendeleo.  

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dokta Angeline Mabula akimkabidhi hati, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mihama iliyopo Manispaa ya Ilemela, Tumsime Mihama wakati alipotoa hati 315 kwa walimu wa shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya Ilemela, akiwa katika ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Mwanza. (Picha na Munir Shemweta).

Aidha, Dokta Mabula ambaye ndiye aliyewahamasisha walimu hao kujiunga pamoja kwa ajili ya kupata viwanja aliyataka makundi mengine maalum kujiunga pamoja kwa lengo la kuona namna ya kuyasaidia kupata viwanja katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

"Suala la makazi siyo la walimu pekee, tuone kama kuna kundi lingine maalum nalo likajiunga kama walivyojiunga walimu na kuchangia fedha ili kupatiwa viwanja,"amesema Naibu Waziri Mabula.

Kwa mujibu wa Dokta Mabula kilichofanyika kwa walimu wa Manispaa ya Ilemela ni juhudi za Rais Dokta John Pombe Magufuli kutaka kila mwenye ardhi awe na umiliki ili kujua mipaka yake na kupata hati kwa lengo la kupunguza migogoro ya ardhi na wakati huo kuitumia hati  kwa shughuli za maendeleo.

 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dokta Angeline Mabula akizungumza na walimu wa Manispaa ya Ilemela (hawapo pichani) wakati wa kuwakabidhi hati 315 za umiliki wa ardhi, wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika Mkoa wa Mwanza. (Picha na Munir Shemweta).

Amewaasa walimu kutumia benki ikiwemo Benki ya NMB kuomba mikopo ya ujenzi wa nyumba ili kuwezesha eneo walilopata kwenda kwa kasi hasa ikizingatiwa eneo hilo limepakana na eneo la Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo cha Afya na Hospitali ya Wilaya ya Ilemela na kubainisha kuwa eneo hilo ni zuri na hata kama walimu hao hawatakaa wanaweza kupangisha na kuingiza fedha kidogo kidogo.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya mradi wa viwanja vya walimu katika halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Albert Mahuyu amesema pamoja na kamati yake kukutana na changamoto kadhaa wakati wa zoezi hilo ikiwemo baadhi ya walimu kushindwa kukamilisha malipo kwa wakati, lakini imefanikisha upimaji viwanja 525 na kuingiza kiasi cha shilingi milioni 404.


Sehemu ya walimu wa Manispaa ya Ilemela waliopatiwa hati na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dokta Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Mwanza. (Picha na Munir Shemweta).

Naye Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa Baraka Ladislaus amesema, benki yake iko tayari kutoa mikopo kwa walimu na kubainisha mikopo inayotolewa na benki hiyo kuwa ni ile ya kununua, kuezeka na kumalizia nyumba pamoja na mkopo wa kurudishiwa fedha uliyojengea nyumba na mikopo iko hadi ya milioni 200 na unarejesha kidogokidogo kwa takribani miaka mitano.


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news