Vijana waipa Amsha Amsha 2020 ya Uhuru Fm siri ya tabasamu lao

MUUNGANO wa Vijana wa Kilimo cha Kitalu Nyumba (MVIKIKINYU) katika Halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjato umeipongeza Serikali kwa kuwapa elimu ya mkulima na kuwawezesha kumiliki kitalu nyumba kinachowasaidia kujiongezea kipato, anaripoti PIUS NTIGA kutoka MOSHI.

Tunatekeleza ya Serikali ya Awamu ya Tano, haitekelezi programu ya namna hii tu mkoani Kilimanjaro bali nchini kote,pichani ni Mradi wa Kitalu Nyumba Jimbo la Madaba ambapo vijana wengi wamepata mafunzo ya kujenga na kuzalisha ikiwa ni programu maalumu ya kuwezesha vijana chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kutokana na hayo wameahidi kuhakikisha wanakichagua tena Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kiendelee kuongoza na wao kama vijana waendelee kunufaika.

Wakizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru Fm wilayani humo,wamesema awali maisha yalikuwa ya shida kutokana na kukosa kufanya shughuli yoyote ya kuwaongezea kipato, lakini kupitia asilimia 10 ya mapato inayotolewa na halmashauri kwa vijana,wanawake na wenye ulemavu imewasaidia sana.

“Sisi kama vijana hapa kazi yetu kubwa ilikuwa kukaa vijiweni,hatukuwa na shughuli yoyote ya kufanya,wakati mwingine tunagombana na wazazi, lakini ukiangalia ni vile wamechoka kutuhudumia maana tulikuwa mzigo kwao,lakini kwa sasa tunamshukuru Mungu tunajihudumia wenyewe na kusaidia familia zetu,”amesema Katibu wa MVIKIKINYU, Frank Kimaro wa Uru Kusini.

Amesema, kwa sasa jukumu lao kubwa ni kuhamasisha vijana wenzao ili katika uchaguzi wa Oktoba 28,mwaka huu kura zote ziende kwa CCM kwa kuwa ndicho chama kilichoonyesha dhamira ya dhati a kuwakumbatia vijana.

Kwa upande wake, Anthony Maro mkazi wa Uru Kusini amesema kupitia kitalu nyumba hicho jamii sasa inawaamini na fursa nyingi zimejitokeza katika sekta ya kilimo.“Hapa mnapoona hii ni awamu ya pili,awamu ya kwanza tulilima tumepata faida,na kupitia kilimo hichi tumepata mwamko na tunalima na kwingine,”amesema.

Amewahimiza vijana wengine kujiunga kwenye vikundi ili serikali iweze kuwasaidia kwa kuwawezesha mikopo na ujuzi na hivyo kuzalisha ajira na kujiongezea kipato.

Pamoja na mafanikio hayo ameiomba Serikali kuwasaidia kupata mashine ya kuchakata mazao ya mboga mboga ili mazao wanayozalisha iendane na ukubwa wa masoko na mashine ya kuchakata chakula cha mifugo.

Akitoa taarifa ya mradi huo,Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya, Restina Mwasha amesema halmashauri hiyo ni miongoni mwa halmashauri zilizopata fursa ya kujengewa kitalu nyumba kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupata ujuzi na stadi za kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba (Greenhouse technology) unaotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira,Vijana na Wenye Ulemavu.

Amesema, awamu ya kwanza ililenga vijana 20 na mafunzo yalitolewa 2019 na awamu ya pili ilifanyika 2020 lengo likiwa ni kuongeza tija na kuvutia vijana wengi kujiajiri katika kilimo.

“Halmashauri iliwezesha upatikanaji wa eneo hili la mradi na kusogeza miundombinu ya maji karibu ambapo katika mradi huu walijengewa uwezo kwenye mpango wa biashara,mbinu shirikishi za kilimo,uvunaji na uhifadhi, kalenda za mazao,ujasiriamali,kuboresha rutuba ya udongo na kalenda za mazao,"amesema.

Ametaja baadhi ya mafanikio ya mradi huo kuwa ni vijana kupata mafunzo ya kilimo ambapo walitambua fursa mbalimbali zilizopo na namna ya kuzitumia,vijana wameweza kujiongeza na kuumia fursa katika eneo hilo kwa kulima mboga za majani.

Ameweka bayana matarajio ya vijana wanaosimamia kitalu hicho kuwa ni ujenga vitalu kwenye maeneo yao kupitia uwezeshaji wa mikopo isiyo na riba kutoka halmashauri,kuanzisha kiwanda kidogo cha ukaushaji wa mazao ya mbogamboga na matunda na kuanzisha uchakataji wa vyakula vyote vya mifugo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news