BRELA yazidi kuchanja mbuga yanoa maafisa biashara,TEHAMA yasisitiza ukiwa jikoni, umelala unaweza kujimilikisha kampuni

Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni nchini (BRELA) imeendelea kuwajengea uwezo maafisa biashara na maafisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa mikoa na halmashauri zote nchini,anaripoti Christina Njovu (BRELA) Moshi.

Bw. Hilary M. Msele akifurahia baada ya kukabidhiwa cheti cha usajili wa jina la biashara (Makutano Bucha) na Afisa wa Brela, Bi.Yvonne Massele katika mafunzo ya utoaji wa huduma za Sajili na Leseni kwa njia ya mtandao kwa maafisa TEHAMA na biashara wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga yanayofanyika mkoani Kilimanjaro. (BRELA).
Lengo likiwa ni kuwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi na kutatua changamoto zinazotokana na mifumo wakati wa usajili wa majina ya biashara na utoaji leseni za biashara nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Mheshimiwa Alhaji Mwangi Rajab Kundya akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa biashara wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga yanayofanyika mkoani Kilimanjaro. (BRELA).

Mkuu wa wilaya ya Moshi, Mheshimiwa Mwangi Rajab Kundya akipokea zawadi kutoka kwa Afisa Tawala na Rasilimali Watu BRELA Tulizo Mpina kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA mara baada ya kufungua mafunzo ya utoaji wa huduma za Sajili na Leseni kwa njia ya mtandao kwa maafisa tehama na maafisa biashara wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga yanayofanyika mkoani Kilimanjaro. (BRELA).

Mkuu wa Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Alhaji Mwangi Rajab Kundya ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya utoaji wa huduma za Sajili na Leseni kwa njia ya mtandao kwa maafisa TEHAMA na maafisa biashara wa mikoa ya Kaskazini ikiwemo mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Arusha yanayoendendeshwa na Wakala ya Usajili Biashara na Leseni (BRELA) na kufanyika kwa muda wa siku tano mkoani Kilimanjao.

“Natambua kwamba BRELA inatoa huduma zake zote kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa ORS na National Business Portal kwa takriban miaka miwili sasa, baadhi ya changamoto zinazotokana na mfumo ya kielektroniki wameendelea kuzitatua kwa kutumia maafisa TEHAMA wa ndani na ndio maana wamejumuishwa katika mafunzo haya, ni jambo la kujivunia sana,"amesema Mkuu huyo.
Aidha, amewaomba washiriki wa mafunzo hayo pindi watakaporudi katika vituo vyao vya kazi wakaondoe dhana iliyojengeka miongoni mwa wananchi ya kuwatazama sawasawa na maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kusema, “Napenda nisisitize ukweli huu kwamba, leo hii afisa biashara akionekana mahali fulani katika biashara watu wanamtazama sawa sawa na afisa wa TRA.

"Wanamuona kama mtu ambaye amekwenda kwa dhumuni la kukusanya mapato, kukusanya kodi, lakini wanasahau jukumu muhimu sana la afisa biashara kuwa msaidizi na mshauri wa biashara mwenye lengo la kufanya biashara ikue ili iwe na tija kwake na kumuwezesha kulipa kodi stahiki ili yeye na serikali yake waweze kufaidi matunda hayo,"amesema.

Akitoa rai kwa maafisa biashara hao na kwa washiriki wengine watakaopatiwa mafunzo hayo, Mkuu huyo wa wilaya amewataka kutoa huduma hizo saidizi kwa wananchi kwa weledi na uaminifu mkubwa na kujiepusha kabisa na vishawishi au kupokea rushwa katika utoaji wa huduma zao ili mafunzo hayo yaoneshe matokeo chanya na lengo kuu lililokusudiwa na Serikali liweze kutimia.

Hata hivyo, DC Kundya amesema,mafunzo hayo kwa nia njema yana lengo la kuhakikisha kwamba huduma zinazotolewa na BRELA zinawafikia wananchi kwa karibu zaidi na hivyo kuwapunguzia kero na usumbufu na gharama zisizokuwa za lazima katika uratibishaji wa biashara hapa nchini.


Bw.Avit A. Mushi akifurahia baada ya kukabidhiwa cheti cha usajili wa jina la biashara (Amka Bucha) na afisa tawala na rasilimali watu BRELA, Tulizo Mpina katika mafunzo ya utoaji wa huduma za sajili na leseni kwa njia ya mtandao kwa maafisa tehama na biashara wa mikoa ya kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga yanayofanyika mkoani Kilimanjaro. (BRELA).


Naye Afisa Tawala na Rasilimali Watu BRELA, Tulizo Mpina amesema kuwa, lengo la kutoa mafunzo hayo kwa maafisa biashara kunatokana na lengo la kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuwa wafanyabiashara ndio wanaowajibika moja kwa moja kwa wananchi kutoa elimu elekezi na kuweza kuwahudumia badala ya kufunga safari na kuwafuata BRELA makao makuu.

Amesema, kwa sasa mtu anaweza kusajili jina la biashara yake akiwa nyumbani kwake hata akiwa jikoni anapika ama chumbani amelala.

Mkuu wa wilaya ya Moshi, Mheshimiwa Mwangi Rajab Kundya akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa BRELA mara baada ya kufungua mafunzo ya utoaji wa huduma za Sajili na Leseni kwa njia ya mtandao kwa maafisa Tehama na maafisa biashara wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga yanayofanyika mkoani Kilimanjaro. (BRELA).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news