Maganja wa NCCR Mageuzi aahidi elimu bure hadi vyuo vikuu na neema nyingine

Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha NCCR Mageuzi, Yeremia Kulwa Maganja, amewaomba wananchi wa Musoma na Mkoa wa Mara kwa ujumla, wamchague katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu, kusudi aweze kufufua viwanda vyote vilivyokufa na kujenga vingine vipya kusudi vichangie kukuza uchumi wa Mkoa wa Mara,anaripoti Amos Lufungulo, Mara.
Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha NCCR Mageuzi, Yeremia Kulwa Maganja akimnadi Mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Mjini, Joyce Sokombi (katikati ) wakati wa mkutano uliofanyika Nyasho Stendi  Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara. (DIRAMAKINI ).

Maganja amesema, ufufuaji wa viwanda hivyo, utaendana na uwekezaji katika fursa za kilimo, mifugo, uvuvi kwa kuweka mfumo bora na thabiti utakaokuwepo sambamba na kutangaza kwa upana unaotakiwa fursa zilizopo mkoani Mara ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ziwa Victoria pamoja na kuimarisha uhusiano mipakani ili biashara ya utalii iweze kuwanufaisha wakazi wa Mkoa wa Mara.

"Uongozi wa kilichokuwa kiwanda cha nguo cha Musoma cha MUTEX kilikufa kutokana na uongozi mbovu miaka ya 1992, tuchagueni sisi tukafufue viwanda, tutajenga pia viwanda na mahoteli makubwa katika Mkoa wa Mara lengo ni kufufua uchumi wa wakazi wa Mkoa wa Mara, tumejipanga kukuza ustawi wa maendeleo ya kijamii kwa watu, uchumi wao pamoja na kuimarisha utulivu wa kisiasa nchini kwa ufanisi mkubwa,"amesema.

Pia ameongeza kuwa, chama hicho kitaondoa utaratibu wa Bodi ya Mikopo uliopo kwa sasa na badala yake, wanafunzi wote watasoma bure mpaka elimu ya chuo kikuu kuwezesha elimu bure na bora sambamba na kuajiri watumishi wa kada mbalimbali kwa wingi katika kulisukuma Taifa kimaendeleo, na hivyo amewaomba wakazi wa Musoma na Watanzania wote wampe ridhaa akayatekeleze hayo.

"Ndani ya siku 100 mkinichagua nitasimamia mwafaka wa Kitaifa kuleta maridhiano ya pamoja ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, watu wameumia kisiasa, kiuchumi, kijamii,pia ndani ya miezi 12 nitasimamia suala la katiba mpya kwa kuanzia rasmu ya Jaji Warioba ilipokomea kwenda mbele, nitawaletea Katiba mpya ambayo itafaa sana kwa watu wote,"amesema Yeremia.

"NCCR Mageuzi tumejipanga kukuza uchumi wa watu siyo takwimu kwenye karatasi bali uhalisia wa maisha ya Wananchi. Tutabooresha pia huduma ya maji ili wananchi wasipate tabu kupata maji safi na salama umbali wa mita 100, tunataka maji yawe karibu na wananchi,"amesema Yeremia.

Naye Mgombea Ubunge Kupitia chama hicho cha NCCR Mageuzi Jimbo la Musoma Mjini, Joyce Sokombi amesema akipewa ridhaa atahakikisha kwamba anawezesha shule zote za sekondari zinajengewa mabweni na uzio kwa lengo la kulinda watoto wa kike wasipewe mimba hatua ambayo pia itaongeza ufaulu katika masomo yao.

"Haiwezekani mtoto anaishi Kata ya Nyasho, lakini anasoma sekondari iliyopo kata nyingine kabisa ya mbali, mkinichagua kuwa Mbunge wenu watu wa Musoma Mjini, nitawezesha ujenzi wa sekondari ndani ya kata husika watoto wasitembee kwenda mbali kwa maana tatizo hili limekuwa likipelekea mimba kwa watoto wa kike kwa kupewa lifti na watu na baadaye kuwashawishi kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi na hivyo hushindwa kufaulu vizuri katika masomo yao,"amesema Sokombi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news