Rais Magufuli amtumbua Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Igunga

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Desemba, 2020 ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora Bw. Revocatus Kuuli, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini (Igunga).
Hayo yamebainishwa leo Desemba 28, 2020 kupitia taarifa ya Gerson Msigwa ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU wakiwa mjini Igunga.

Mhe. Rais Magufuli ametengua uteuzi huo kufuatia tuhuma za kujitwalia ardhi ya wananchi bila kufuata utaratibu, utendaji kazi usioridhisha na ubadhilifu wa fedha za maduhuli ya Serikali zinazomkabili Mkurugenzi Mtendaji huyo.

Mhe. Rais Magufuli ametangaza uamuzi huo aliposimama kuwasalimu wananchi wa Igunga wakati akiwa safarini, ambapo wananchi na viongozi wa Tabora wamepata fursa ya kueleza kero zao.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Phillemon Sengati kuteua mtumishi mwadilifu atakayekaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mpaka hapo uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji mwingine atakayeendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano utakapofanyika.

Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, anazo taarifa nyingi za dosari za Bw. Kuuli, alishamuonya juu ya vitendo vyake vya kuwadhulumu wananchi wakiwemo wanawake na hivyo Serikali anayoiongoza haiwezi kumvumilia kiongozi wa namna hiyo.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru wananchi wa Igunga na Watanzania kwa ujumla kwa kumchagua kwa kura nyingi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili na ameahidi kuwatumikia kwa uwezo wake wote.

Amewapongeza wananchi wa Tabora, Igunga na Nzega kwa kupata maji kutoka Ziwa Victoria na amewasihi kutumia maji hayo vizuri kwa manufaa yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news