Waziri Biteko ataja vinara wa utoroshaji madini ya dhahabu

Waziri wa Madini, Doto Biteko ametaja majina matatu ya wafanyabiashara wa kununua na kuuza madini ya dhahabu (dealers) ambao wanashiriki katika vitendo vya utoroshaji dhahabu Mkoa wa Geita, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.

Amesema, ana majina ya wafanyabiashara sita katika mkoa wa Geita, lakini ameamua kutaja majina matatu kwanza na mengine matatu ameyahifadhi .
Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akihoji baadhi ya mambo kwa mfanyakazi wa Idara ya Madini Kitengo cha kukusanya mapato ya madini katika Soko Kuu la Dhahabu mjini Geita alipofika leo kukagua utendaji wa soko hilo,kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini). 

Amesema, wafanyabiashara hao wananunua dhahabu nje ya masoko na kuuza kusikojulikana kinyume na sheria zinazosimamia sekta ya madini nchini.

Waziri Biteko ametaja majina hayo kuwa ni mfanyabiashara wa Dhahabu Maduka Mbaraka,Makandaga Sita na Makaranga Kiserya.

Ametaja majina hayo katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Kituo cha Uwekezaji cha mjini Geita (EPZA) alipokuwa na kikao cha pamoja na wafanyabiashara wadogo wadogo wa dhahabu (brokers) na wafanyabiashara wakubwa wa dhahabu (dealers) ili kujadili namna ya kudhibiti utoroshaji wa madini.

Amesema, wafanyabiashara hao anawapa onyo la mwisho ili waweze kujirekebisha na wasipobadilika na kuacha tabia hiyo ya kutorosha madini hatua kali zinatachukuliwa dhidi yao ikiwemo kuwafilisi mali zao pamoja na kuwafikisha mahakamani.

Waziri Biteko amewataka wafanyabiashara kuzingatia sheria na kanuni wakati wanafanya biashara hiyo ili kuepuka kufilisika au kufungwa kwa makosa ya kukiuka sheria za madini.
Wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa dhahabu Mkoa wa Geita wakiwa katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Kituo cha Uwekezaji cha Mjini Geita (EPZA) wakiwa kwenye kikao na Waziri wa Madini, Doto Biteko. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Amesema kuwa, Rais John Magufuli aliwafutia kodi na tozo nyingi za madini ambazo zilikuwa zinafikia takribani asilimia 21 ili waweze kufanya biashara hiyo bila kutorosha madini.

Ametaja kiwango cha kodi wanacholipa kwa mujibu wa sheria kuwa ni asilimia saba tu ambacho ni rafiki kwa kila mfanyabiashara hiyo .

Waziri Biteko amesema kuwa awali alipata majina ya wanunuzi 16 ya wafanyabiashara wa Dhahabu wanaojihusisha na utoroshaji, lakini baada ya uchunguzi wa kina wamethibitisha bila shaka wahusika ni watu sita katika mkoa wa Geita.

Amewataka wafanyabiashara hao wasioneane wivu wa kibiashara kwa kuwasingizia wengine kuwa wanahusika na utoroshaji baada ya kuona wenzao wanafanyabiashara vizuri badala yake watoe taarifa sahihi na zenye ukweli.

Katika hatua nyingine Waziri wa Madini Biteko,ameagiza wafanyabiashara wadogo wa Dhahabu (brokers) kununua dhahabu bila kuzuiliwa kwa kuwekewa matabaka ya Dhahabu inayotoka kwenye viwanda vya kuchenjua Dhahabu ( Elution plant) na inayotoka kwenye mialo .

Agizo hilo limekuja baada ya mfanyabiashara Charles Kazungu kulalamikia utaratibu wa kuzuia wafanya biashara hao kununua dhahabu inayotoka kwenye vinu vya kuchunjulia badala yake wameelekezwa wanunue inayotoka kwa mchimbaji mdogo anayepata Dhahabu kwa kukamatisha kwa Zebaki .

Biteko amesema, sheria inamruhusu mfanyabiashara huyo mdogo kununua dhahabu yoyote na kiwango chochote ilimradi hawezi kuuza nje ya nchi.

Aidha ,Waziri Biteko ametoa siku 30 kwa mgodi wa uchimbaji wa madini ya Dhahabu wa Geita (GGML) kulipa fidia wananchi 1,200 ambao nyumba zao zimepasuka kutokana na shughuli za uchimbaji zinazofanywa na mgodi huo.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akitembelea Soko Kuu la Dhahabu mjini Geita,kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel na kulia ni Mbunge wa Jimbo la Busanda, Tumaini Magesa.(Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Constantine Kanyasu amepongeza uamuzi wa Waziri Biteko kuchukua hatua kali dhidi ya wafanyabiashara wanaotorosha madini kwani wanahujumu mapato ya serikali.

Pia amesema kitendo cha kutoa siku 30 kwa GGML kulipa fidia wananchi 1200 wa mitaa inayozunguka mgodi huo ambayo nyumba zao zilipasuka ni jambo muhimu na kutaka mgodi huo kuheshimu maagizo hayo.

Amesema siku za nyuma mgodi huo ulisingizia mlipuko wa ugonjwa wa Covid -19 lakini sasa hivi ni muda muafaka kuwalipa wananchi hao.

Waziri wa Madini Doto Biteko yuko mkoani Geita katika ziara za kukutana na wadau wa madini ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara na wachimbaji wa madini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news