WAZIRI LUKUVI AAMURU KUFUTWA HATI YA ARDHI NA KUSHUSHA NEEMA KWA WAKAZI WA MHANDU NYAMAGANA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameshusha neema kwa wakazi wa kata ya Mhandu katika halmashauri ya manispaa ya Nyamagana mkoa wa Mwanza kwa kuamuru kuondolewa katika daftari Hati ya kitalu Na 153 eneo hilo na kupatiwa wananchi 74 waliokuwa katika mgogoro,anaripoti Munir Shemweta (WANMM) Nyamagana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akipata maelezo kuhusiana na eneo lenye mgogoro wa muda mrefu la Mhandu katika wilaya ya Nyamagana alipokwenda kutatua mgogoro huo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza tarehe 3 Machi 2021.
Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Mwanza Kiamoni Kibamba akizungumza kabla ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutatua mgogoro wa muda mrefu wa wakazi wa kata ya Mhandu wilaya ya Nyamagana wakati akiwa katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Mwanza tarehe 3 Machi 2021.

Akitoa uamuzi huo leo tarehe 3 Machi 2021 katika wilaya ya Nyamagana alipokwenda kutatua mgogoro wa eneo hilo uliodumu kwa takribani miaka 14, Waziri Lukuvi alisema, hati ya mtu anayedaiwa mmiliki wa eneo hilo anayetambulika kwa jina la abdallah maliki ilitakiwa kufutwa muda mrefu kwa kuwa hajalipia kodi ya pango la ardhi kwa miaka 15.

"Hati miliki ikaondolewe katika daftari la hati na jaji amethibitisha katika maamuzi yake kuwa wamiliki wa asili katika eneo hili hawakulipwa fidia,"amesema Lukuvi.

Waziri wa Ardhi ameongeza kuwa, kutokana na maamuzi hayo sasa wananchi wa eneo hilo watatakiwa kupimiwa kulingana na ukubwa wa eneo analomiki na kila mmiliki atatakiwa kulipa tozo la mbele (Premium) asilimia 2.5 kufidia gharama ambayo mmiliki wa awali alishindwa kulipa kodi ya pango la ardhi.

"Huyu mtu ameshindwa kuendeleza kwa wakati na hajalipa kodi kwa miaka 15 sasa wananchi wapimiwe na kupatiwa eneo bila fidia. Huwezi kupewa eneo una hati watu sabini wanajenga miaka 15 wewe una hati umekaa nayo tu,"amesema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Lukuvi Serikali itahakikisha inalinda hati ya mmiliki wa ardhi huku mmiliki akitakiwa kulinda eneo lake na kusisitiza kuwa hati ya ardhi ni dhamana na ndiyo inayotoa usalama wa mmiliki.

"Mtu hajaonekana halafu atoe kibali cha kuvunja nyumba. Sheria hairihusu umilikishaji juu ya hati nyingine ndiyo maana nimeamua kuifuta kwanza hati hii ndiyo hati nyingine iweze kusajiliwa,"amesema Lukuvi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wakazi wa Kata ya Mhandu wilaya ya Nyamagana alipokwenda kutatua mgogoro wa muda mrefu wa ardhi katika eneo hilo akiwa katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Mwanza tarehe 3 Machi 2021.

Aidha, aliagiza eneo lingine kitalu 154 linalokaliwa na wananchi 40 na kumilikiwa na Abdulkarim Mbaga mmiliki wake apelekewe ilani ya siku 90 kabla ya hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi ya eneo lake.

Akiwasilisha mgogoro huo mbele ya Waziri wa Ardhi mwakilishi wa wananchi wa Kata ya Mhandu Sokoni Bw. Kazimiri Shimbi alisema kuwa, muda mrefu wananchi wa eneo hilo wamekuwa katika mgogoro wa ardhi wakishitakiwa na mtu wasiyemjua jambo lililosababisha kushindwa kurasimishiwa makazi katika eneo hilo kwa madai ya kuvamia eneo. 

Hata hivyo, kwa mujibu wa Shimbi wananchi hao wa Mhandu mara kadhaa wamekuwa wakishinda kesi mahakamani dhidi ya mdai.

Post a Comment

0 Comments