Prof.Mark Mwandosya asimulia Mungu alivyomnusuru kifo kutokana na Corona

Kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja nimekuwa nikiugua na kutibiwa ugonjwa wa COVID19 unaotokana na virusi vya Corona (SARS-CoV-2). Ni jinsi gani niliweza kuambukizwa ugonjwa huu kijijini kwetu Lufilyo, Busokelo, Mbeya, pamoja na kuzingatia tahadhari zote dhidi ya maradhi haya ni kitendawili.
Prof. Mark Mwandosya alipokuwaHospitalini, Nairobi, Kenya

Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai, zawadi ya Pasaka. Nawashukuru pia mke wangu Lucy Akiiki, watoto na wajukuu, familia za Kahigwa na ya Mwandosya, Madaktari na Wauguzi wangu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, na Hospitali ya Nairobi (Nairobi Hospital), AMREF Flying Doctors, Uongozi wa Stanbic Bank Tanzania Limited na Stanbic Kenya Ltd, Balozi Chirau Mwakewere na Mama Rose Mwakwere wa Nairobi, Mheshimiwa Jaji Paul Mugamba wa Mahakama ya Juu Uganda na Mama Grace Mugamba, familia ya Kabange wa Nairobi, na ndugu na marafiki wote wanaoendelea kunitakia heri na afya njema. Asanteni sana.

Huu ni ushuhuda wangu kwamba Corona/Covid 19 ipo Tanzania .

Tumebahatika kuvuka kipindi cha mpito salama na kumpata Rais mpya, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Mwenyezi Mungu amjalie neema na baraka tele. Mheshimiwa Dr Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais, ambaye nampongeza kwa uteuzi, amepitia hayo yaliyonisibu.

Nawaomba, tena kwa unyenyekevu mkubwa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Dr Philip Isdor Mpango na Mheshimiwa Dr Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwamba, tuongozwe na sayansi, na tuungane na tushirikiane na wenzetu duniani kote katika kupambana na ugonjwa huu kama tunavyofanya katika milipuko ya magonjwa mengine. Kwani katika mlipuko wowote, hakuna anayeweza kuwa salama mpaka wote duniani tumekuwa salama.
Prof. Mark Mwandosya akiwa eneo la Kilimani baada ya kuruhusiwa kutoka Hospitalini, Nairobi, Kenya

Maombi yangu kwa Mwenyezi Mungu ni kwamba, ikiwezekana, Mtanzania mwingine awaye yote aepushwe na mateso na taabu za kukabiliana na maradhi haya. Hakika siwezi kumtakia mtu mwingine yeyote, hata aliye adui yangu mkubwa namna gani, kama yupo, apate ugonjwa huu.

Tutakiane Pasaka njema. Mwenyezi Mungu ibariki Tanzania.

Pro Deo et patria.
Mark Mwandosya
Nairobi
5 Aprili 2021

Post a Comment

0 Comments