Serikali yakubali kuunganisha vijiji 20 umeme kupitia REA Jimbo la Njombe Mjini

Serikali imekubali kuunganisha vijiji 20 vilivyokuwa vimeachwa kuunganishiwa umeme kwenye Mpango wa Wakala wa Umeme Vijiji (REA) katika Jimbo la Njombe Mjini, ANARIPOTI MWANDISHI DIRAMAKINI.
Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati, Stephen Byabato ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma leo wakati akijibu maswali yaliyoulizwa na Mbunge wa Njombe Mjini, Deodatus Mwanyika.

Akiuliza maswali ya nyongeza, Mwanyika amesema baada ya kufuatilia kwa karibu sana imedhihirika wazi kuwa katika Jimbo la Njombe ni vijiji vinne tu, ndivyo vilivyoingizwa kwenye mpango wa kupata umeme wa REA ili kukamilisha idadi ya vijiji 1,974 ambavyo havina umeme huo nchini.

Amesema, kuna vijiji takribani 20, ambavyo vimesahaulika, hivyo iliiomba Serikali itoe kauli kuhusiana na suala hilo na iwadhihirishie wananchi wa Vijiji vya Njombe kwamba baada ya mazungumzo yake na Waziri, vijiji hivyo vimeingizwa kwenye mpango huo wa REA.

Katika swali lake la pili, aliuliza kuwa pamoja na vijiji vingi kuunganishwa hasa katika Jimbo la Njombe Mjini, bado wana tatizo la kukatikakatika kwa umeme kwa kiwango kikubwa sana.

Amesema hiyo inaashiria kwamba pamoja na kuunganishiwa umeme, tatizo hilo litaendelea kuwa kubwa, hivyo alitaka kupata maelezo ya Wizara ya Nishati, kuhusiana na tatizo hilo katika Mji wa Njombe.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri Byabato, alikiri kuwa ni kweli mara ya kwanza vilichukuliwa vijiji vinne, lakini baada ya Mbunge Mwanyika kuwasiliana na ofisi, Wizara imeamua kuongeza vijiji hivyo 20 kwenye mpango wa REA.

"Na tunamshukuru na kumpongeza mheshimiwa mbunge kwa ufuatiliaji wake mkubwa," amesema Byabato.

Hata hivyo, amesema kimsingi vijiji hivyo havikuwa vimeachwa, bali vilikuwa vimebaki kwa sababu vipo katika eneo linalokaribiana na mji, havikuwa vimeingia kwenye mradi wa REA, lakini wamevichukua na kuviingiza kwenye mradi huo.

"Kwa hiyo vijiji hivyo 20 nimhakikishie mheshimiwa Mwanyika kwamba vimeingia na vitapata umeme katika awamu hii ya kupeleka umeme vijijini,"amesema Byabato.

Kwa upande wa swali lake la pili, Naibu Waziri Byabato, alikiri maeneo ya Njombe yanalo tatizo kubwa la ukatikaji mkubwa wa umeme.

Amesema, Njombe inapata umeme katika kituo cha kupoza umeme cha Makambako na kwamba kuna kilometa 60 kutoka Makambako hadi Njombe Mjini.

Amesema, Njombe wanayo matatizo makubwa matatu, la kwanza ni baraka ambazo Njombe imezipata ya kuwa na miti mingi sana.

Amesema, pamoja na kufyeka miti kwenye njia inayopitisha umeme, lakini miti inayokua nje ya njia hiyo baadaye inaangukie kwenye njia yao ya umeme, lakini wameendelea kufyeka miti hiyo.

Aidha, wamekuwa wakiwahamasisha wananchi wawaongezee njia nje zaidi, ili wanapofyeka miti inayotoka kwao isije ikaleta shida kwenye njia yao.

Tatizo la pili, amesema ni radi. Pia amesema Mbeya, Kagera na Mjombe wana shida sana kwenye miundombinu yao ya umeme na kila transfoma wanayofunga, wanafunga vifaa vya kuzuia radi.

Hata hivyo, amesema kwa sasa kila transfoma wanayofunga wanaweka vifaa ili kuhakikisha transfoma haziharibiki mara kwa mara.

Post a Comment

0 Comments