Wenye ulemavu wa kusikia wakumbana na vikwazo huduma za afya

Na Mashaka Mhando, Tanga

WATU wenye ulemavu wa kusikia (Viziwi), wanakutana na changamoto mbalimbali za kupata huduma ikiwemo kuandikiwa dawa zisizohusiana na maradhi wanayougua.
Mwenyekiti wa CHAVITA Taifa, Nidrosy Mlawa akitoa mada kuhusu mtu aliyepoteza uwezo wa kusikia (Kiziwi).
Akizungumza katika warsha ya siku mbili iliyoandaliwa na Chama Cha Viziwi nchini (Chavita), Mratibu wa mafunzo ya kukuza hadhi ya lugha ya alama nchini, Lupi Maswanya amwsema, Viziwi wengi wanapokutana na daktari wanashindwa kuelewana.
Mratibu wa mafunzo ya kukuza hadhi ya lugha ya alama nchini, Lupi Maswanya.

Amesema, licha ya mgonjwa kushindwa kuelewana na watoa huduma za afya, lakini pia ndugu na walezi wa watu hao wenye ulemavu na wao pia hawawezi kuwasiliana nao ili kumbainishia tatizo la mgonjwa daktari.

Alisema kutokana na kukosekana kwa mawasiliano, viziwi wamekuwa wakipatiwa dawa zisizokuwa sahihi kutokana na kutokuelewa tatizo hasa analougua.

"Kuna changamoto kwa viziwi kushindwa kuwasiliana na madaktari na ndugu pia hawawezi kuwasiliana nao, unakuta kiziwi anapewa dawa isiyokuwa ya ugonjwa wake, hii ni hatari sana," amesema Maswanya ambaye pia ni ofisa Ustawi wa Chavita

Amesema kuwa, njia pekee ya kuondoa tatizo hilo ni kuwa na wakalimani katika sehemu za huduma ikiwemo hospitali, mahakamani na maeneo mengine muhimu ambayo viziwi wamekuwa wakienda kufuata huduma.

Mratibu huyo amesema, ili jamii iweze kuwasiliana na watu wenye ulemavu wa kusikia ni vema sasa masomo yakafudishwa kwa lugha ya alama ili kuwajengea uwezo viziwi pamoja na jamii nyingine.

Mratibu huyo amesema, kwa upande wa elimu lipo tatizo katika ufundishaji wa masomo ya sayansi katika shule za sekondari ambako kuna baadhi ya alama hazipo.

"Masomo ya sayansi kwa shule za sekondari kuna baadhi ya alama zimekosekana hivyo wanafunzi viziwi wanashindwa kwenda sambamba na wenzao hali iliyopelekea mwaka 2016 viziwi walifeli mitihani ya kidato cha nne hasa mkoa wa Njombe.

Hata hivyo, amesema mafunzo wanayotoa kwa viongozi wa serikali wakiwemo walimu, Ustawi wa jamii na polisi kupitia dawati la jinsia litawaongezea ufahamu wa lugha ya alama kwa kazi zao za kila siku.

"Mradi umekuja baada ya changamoto wanayokutana nayo viziwi…Huu mradi ni wa miezi 18 na tumechagua mikoa ya Mtwara, Tanga na Dodoma," amesema.
Mwenyekiti wa Chavita mkoani Tanga, David Nyange.

Awali Mwenyekiti wa Chavita mkoani Tanga, David Nyange amesema, lengo la warsha hiyo ni kuwajengea uwezo na mwamko wa ufahamu wa lugha ya alama wazazi pamoja na viongozi wa serikali

Amesema, ipo haja kwa kuongeza wakalimani katika maeneo ya huduma ili watu wasiosikia waweze kuwasiliana na watu wengine.
Pia mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wazazi wenye watoto viziwi kuhakikisha wanajifunza lugha za alama ili waweze kuwasiliana katika mambo mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news