Waitara awataka Wakandarasi kuepuka rushwa

Na DENIZA CYPRIAN, WUU

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amewataka wakandarasi wazawa kuepuka vitendo vya rushwa wakati wa kuomba na kutekeleza zabuni za miradi ya Serikali inayotangazwa kwani kwa kufanya hivyo kunapelekea kutekeleza miradi hiyo chini ya kiwango au wakati mwingine kushindwa kabisa kuimaliza.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akisisitiza jambo wakati akifunga mkutano wa nne wa mashauriano wa wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa mwaka 2021 ulioandaliwa na Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB), jijini Mwanza.

Aidha, Waitara ameeleza nia ya Serikali kuendelea kuwapa miradi mingi wakandarasi wazawa lakini lazima waoneshe uwezo wao kwa Serikali kwa kutekeleza miradi waliyopewa tayari kwa mifano ili Serikali iendelee kuwadhamini.

Ameyasema hayo jijini Mwanza wakati akifunga mkutano wa nne na wa mwisho wa mashauriano na wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa mwaka 2021, ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza miradi inayotolewa kwa wakandarasi wazawa itekelezwa kwa ubora na viwango kama ilivyo katika mikataba na thamani ya fedha ionekane.

“Nawasihi msitoe rushwa katika kuomba miradi, mshirikiane, muache ubinafsi ili muweze kupata miradi mikubwa na kuitekeleza kwa pamoja, kama kuna changamoto mikutano mikubwa kama hii ndio mahali sahihi ya kuzungumzia utatuzi wa changamoto hizo,”amesisitiza Waitara.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akizungumza na uongozi wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), katika mkutano wa nne wa mashauriano wa wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa mwaka 2021 ulioandaliwa na Bodi hiyo, jijini Mwanza.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wakandarasi wazawa kushiriki miradi mikubwa inayofanywa na wakandarasi kutoka nje ili waweze kuwa wabobezi kwenye kazi hizo na wakati mwingine miradi kama hiyo inapohitaji kufanyiwa ukarabati inaweza kufanywa na wakandarasi wa ndani badala ya kuwaachia wakandarasi wa kigeni kuja kuendelea kutekeleza miradi hiyo.

Kwa upande wake Msajili wa CRB, Rhoben Nkori, amemuambia Naibu Waziri Waitara kuwa Bodi yake itafanya majumuisho ya maazimio yote ya mikutano minne iliyofanyika na kuyawasilisha Wizarani kwa ajili ya kupatiwa utatuzi wa changamoto na kuona namna bora ya kuwawezesha wakandarasi hao hasa katika miradi inayotarajiwa kutangazwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akizungumza na wadau kutoka Benki ya CRDB ambao wanatoa mikopo kwa wakandarasi wazawa ili kuweza kupata mitaji ya kutekeleza miradi mikubwa nchini, baada ya kufunga mkutano wanne wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi jijini Mwanza.

“Mheshimiwa Naibu Waziri jumuiya ya wakandarasi inapenda kukushukuru kwa kushirikiana nasi katika mikutano yetu miwili ya Arusha na hapa Mwanza, na kwa niaba ya wenzangu napenda kukuahidi kuwa maelekezo yako yote uliyotupatia kwenye vikao hivi viwili tunakwenda kuyafanyia kazi”, amesema Nkori.

Jumla ya wadau 1,366 wa Sekta ya Ujenzi wameshiriki katika mikutano minne ya mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi katika mikoa ya Arusha, Mbeya, Dar es Salaam na Mwanza ambapo kati ya hao wakandarasi ni 1,035 na wasio wakandarasi 336.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news