China yatoa onyo, Korea Kaskazini yaipongeza

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa China, Xi Jinping ameyaonya mataifa ya kigeni dhidi ya kujaribu kuionea China akisema enzi za kufanya hivyo zimepitwa na kwamba taifa hilo la kikomunisti limechukua mwelekeo wa kujiimarisha na kutorudi nyuma.
Rais Xi ameyasema hayo leo wakati wa hotuba yake kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 100 tangu kuundwa kwa Chama cha Kikomunisti cha China ambacho kimeliongoza taifa hilo la Mashariki ya Mbali kwa zaidi ya miaka 70.

Kwenye sherehe hizo zilizoandaliwa kwa mtindo wa kuonesha nguvu za China, Rais Xi aliahidi kuimarisha nguvu za kijeshi za taifa hilo, kukirejesha kisiwa cha Taiwan chini ya himaya ya China pamoja na kuimarisha nafasi ya Beijing katika uendeshaji wa mji wa Hong Kong.

Wakati huo huo, Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un amesema kuwa, analenga kuimarisha zaidi mahusiano yake na China wakati anajaribu kuikwamua nchi yake kutoka mzozo mkubwa unaohusishwa na janga la virusi vya corona.

Shirika la Habari la Korea Kaskazini liliripoti kuwa, Kim alitoa matamshi hayo kupitia ujumbe wa pongezi alioutuma kwa Rais Xi Jinping wa China kwa maandhimisho ya miaka 100 tangu kuundwa kwa Chama cha Kikomunisti cha China.

Kim amenukuliwa akisema chama tawala cha kikomunisti cha Korea Kaskazini kwa kushirikiana na chama tawala cha China kitaimarisha urafiki kati ya Pyongyang na Beijing katika kiwango cha juu kwa kuzingatia zama za sasa na mahitaji ya raia wa pande mbili.

China ni mshirika mkuu wa Korea Kaskazini na ni miongoni mwa mataifa machache ambayo hayatekelezi kikamilifu vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya Pyongyang kutokana na mradi tata wa silaha za nyuklia nchini humo.

Post a Comment

0 Comments