🔴LIVE:Rais Samia akipokea ndege mpya leo Julai 30,2021

VIDEO: MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AKIPOKEA NDEGE MPYA AINA YA DASH 8 - Q400 KATIKA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA JULIUS NYERERE LEO TAREHE 30 JULAI, 2021
RAIS SAMIA AAHIDI KUISIMAMIA ATCL NA KUWATAKA WATENDAJI WA SHIRIKA HILO KUZITUNZA NDEGE

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameahidi kulisimamia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), huku akiwataka watendaji wa Shirika hilo, kuzitunza Ndege zote zinazonunuliwa na kudhibiti hujuma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa pamoja na Viongozi mbalimbali akikata utepe kuashiria kupokea Ndege Mpya aina ya Bombadier DASH 8-Q400 iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania na kukodishwa kwa Shirika la Ndege la ATCL ilipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo tarehe 30 Julai, 2021. Wa pili kushoto ni Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango na wa tatu kulia ni waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

Kauli hiyo aliitoa leo wakati wa hafla ya mapokezi ya Ndege ya tano aina ya Bombardier Dash 8-Q-400 ambayo inalifanya ATCL kuwa na jumla ya Ndege tisa, iliyofanyika Uwnaja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam.

Alisema tayari amepokea mpango kazi wa shirika hilo na hivyo ataupitia kwa kushirikiana na wasaidizi wake ili kuona namna nzuri ya kufanya.

Rais Samia ameeleza kulifanyia kazi suala la kuzirudishia asilimia 20 ya hisa katika utoaji huduma za chakula ndani ya Ndege kwa ATCL ambazo kwa sasa zipo chini ya Msajili wa Hazina.

Wito kwenu watumishi wa ATCL Ndege hizi tunanunua na jasho na damu ni vyema mkazitunza kwa kudhibiti hujuma, kwani zikitunzwa zitaleta tija iliyitarajiwa," anasema.

Alisema hatua ya serikali kuweka mkazo katika usimamizi wa shirika hilo inatokanana ukweli kwamba usafiri wa anga una fursa ya soko kubwa kwa siku zijazo.

Rais Samia anabainisha kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia mwaka 2018 wasafiri wa Ndege walikuwa bilioni 4.52 na kufikia mwaka 2040 watakuwa bilioni 20.7 hivyo uwekezaji wanaofanywa na serikali unalenga kuvuna fursa hiyo.

"Katika ongezeko hili la wasafiri wa anga naamini Tanzania nasi tutapata fursa ya soko," alisema.

Aliweka wazi kuwa mbali na usafirishaji wa abiria kupitia usafiri wa anga Tanzania itasafirisha bidhaa mbalimbali yakiwemo matunda na mbogamboga.

"Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mbogamboga mwaka 2019 tuliingiza Dola za Marekani milioni 700 na mwaka 2025 tunatarajia kuingiza Dola za Marekani bilioni mbili hivyo usafiri wa anga ni muhimu kwetu," alisisitiza.

Aliongeza pia ili kuvutia Utalii ni muhimu kwa taifa kuwa na Shirika imara la usafiri wa anga kama ilivyo katika mataifa mengine, ndiyo maana uwekezaji mkubwa unafanywa huko.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwasalimia Wananchi waliofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya kumuunga Mkono kwenye mapokezi ya Ndege Mpya aina ya Bombadier DASH 8-Q400 iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania na kukodishwa kwa Shirika la Ndege la ATCL ilipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo tarehe 30 Julai, 2021.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho, alisema ujio wa Ndege hiyo, utaongeza safari za ndani na kikanda ikiwemo Lubumbashi na maeneo mengine.

Alisema jitihada zinazofanywa sasa ni kuanzisha safari za Dubai, Lubumbashi, Ndola, London na Nairobi.

Naye Mtendaji Mkuu wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi, alibainisha kuwa kufikia mwezi Oktoba shirika hilo litapokea Ndege nyingine mbili.

Alisema kwa sasa Shirika lina marubani 100 kutoka 11 waliokuweo wakati shirika linafufuliwa na wahandisi ni 109 kutoka 27 wa awali.

Alisema mbali na mchango wa ukuaji wa kiuchumi Ndege hizo pia ni fursa ya ajira kwa Watanzania.
Alibainisha kuwa serikali itaendelea kuimarisha sekta ya usafiri wa anga, majini na ardhini, hivyo wiatanzania wajipange na fursa zitokanazo na uwekezaji huo.

"Ningependa kuwaambia watu wa sekta binafsi kuanzisha kongani za kiuchumi katika maeneo ambayo serikali inawekeza ili kunufaika na fursa," alisisitiza.

Kuhusu mafanikio ya Shirika, Rais Samia alisema kwa sasa idadi ya wasafiri wa ndani imeongezeka kutoka 4,000 wakati shirika linafufuliwa hadi kufikia 60,000 na hivyo kuifanya kumiliki soko kwa asilimia 73.

Alitaja mengine ni kuwa na karakana yenye uwezo wa kufanya matengenezo yote madogo ya Ndege, pia kubadilisha Injini ya Ndege aina ya Boeing na hivyo kuepuka gharama kwa serikali.

Hata hivyo, alieleza kufurahishwa na hatua ya Shirika hilo kuwa na marubani wanne wanawake huku wengine watatu wakitarajiwa kujiunga baada ya kuhitimu masomo yao hivi karibuni.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kupokea Ndege Mpya aina ya Bombadier DASH 8-Q400 iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania na kukodishwa kwa Shirika la Ndege la ATCL ilipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo tarehe 30 Julai, 2021. (PICHA NA IKULU).

Kuwasili kwa ndege hiyo kunaifanya Tanzania kupitia Shirika lake la Ndege (ATCL), kuwa na jumla ya Ndege tisa kati ya 11 zilizoahidiwa na serikali kufikia mwaka 2025.

Pamoja na Ndege hiyo, zilizotangulia kuingia nchini nne ni Bombardier Dash 8 Q-400 (zinabeba abiria 76 kila moja), mbili Boeing 787-800 (zinabeba abiria 262 kila moja) na mbili aina ya Airbus A220-300 (kila moja inabeba abiria 160).

Post a Comment

0 Comments