Wapinzani acheni chokochoko-Scolastika Kevela

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe (UWT) , Scolastika Kevela amevitaka vyama vya upinzani kuacha kuleta chokochoko nchini kwa kigezo cha kutaka katiba mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Kevela ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart amesema, Rais Samia Suluhu Hassan alishatolea ufafanuzi suala hilo kwa kusema kuwa apewe muda hivyo wanapaswa kutulia.

Amesema, kauli hiyo ya Samia ilipaswa kuheshimiwa na kupokelewa kwa mtazamo chanya na wananchi wote hususani wale wanaoleta chokochoko hasa wapinzani hao ambao muda mwingi wamekuwa wakianzisha jambo ili kutafuta sababu za kuanzisha chokochoko.

“Rais Samia aachwe afanye kazi yake tuliyomtuma wananchi wananchi kwa mujibu wa katiba, ndiyo kwanza uongozi wake una miezi minne madarakani, hizi kelele za wanaotaka katiba zinatolewa kwa lengo la kutaka kumtoa katika reli ya kuwatumikia watanzania,”amesema Scolastika. 

Pia amesema, anashangazwa na wapiga kelele hao kuanza kujitokeza kwa wingi na kuleta chokochoko hizo ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Samia tofauti na awali, kwani kabla yake kulikuwa na kiongozi mwingine katika nafasi hiyo, lakini hawakuthubutu kufanya hivyo.

“Mimi kama Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Njombe nalaani chokochoko hizo na zaidi nawaomba watanzania wote wenye mapenzi mema na nchi hii kuendelea kuunga mkono juhudi anazozifanya Rais wetu kutuletea maendeleo watanzania wote,” amesema Scolastika.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa juhudi mbalimbali anazoendelea kuzichukua katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na mataifa mengine duniani.

Amesema, kitendo cha Rais huyo kukutana na viongozi kutoka mataifa mbalimbali na wakati mwingine kufanya ziara katika mataifa hayo, kinaonyesha dhamira yake ya kushirikiana na mataifa hayo katika masuala mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa uchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news