Waziri Mkuu Majaliwa ana kwa ana na Rais wa Benki ya Afrika mjini Rabat

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Waziri Mkuu Kaasim Majaliwa ameishukuru Benki ya Afrika (BOA) kwa jitihada zake za kuendelea kuisaidia Tanzania katika Sekta mbalimbali za maendeleo.

Ametoa kauli hiyo Julai 14, 2021 wakati alipozungumza na Rais wa benki hiyo Othman Benjelloun kwenye hoteli ya Sofitel, Rabat Nchini Morocco.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Rais wa Benki ya Afrika Othman Benjelloun, kwenye hoteli ya Sofitel Jijini Rabat, Morocco.

Amesema kuwa, uwepo wa benki hiyo nchini Tanzania umewawezesha wananchi kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa na Benki hiyo, "kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tunaishukuru Benki ya Afrika kwa jitihada hizi".

Aidha, Waziri Mkuu alimshauri Rais Benjelloun kuendelea kupanua wigo wa huduma za benki hiyo nchini ili kuwafikia watanzania wengi zaidi hasa katika sekta za Elimu, Kilimo, Mifugo na Madini. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia kitabu cha maelezo kuhusu Benki ya Afrika ambacho alikabidhiwa na Rais wa Benki hiyo, Othman Benjelloun kwenye hoteli ya Sofitel Jijini Rabat, Morocco.

Waziri Mkuu aliahidi kuwa ataandaa utaratibu wa kuukutanisha uongozi wa Benki hiyo na sekta binafsi nchini Tanzania ili kuona namna watakavyoweza kushirikiana katika kuwahudumia Watanzania.

Kwa upande wake, Rais Benjelloun amesema lengo la benki hiyo ni kuendelea kukuza uwekezaji wake nchini Tanzania. "Sisi tupo tayari kuwekeza katika maeneo ambayo viongozi wa taifa la Tanzania watatushauri lengo likiwa ni kutoa mchango wetu katika kujenga uchumi".
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi Rais wa Benki ya Afrika Othman Benjelloun zawadi ya biadhaa mbalimbali zinazozalishwa Tanzania, baada ya mazungumzo yao kwenye hoteli ya Sofitel Jijini Rabat, Morocco.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongozana na Rais wa Benki ya Afrika Othman Benjelloun, baada ya mazungumzo yao kwenye hoteli ya Sofitel Jijini Rabat, Morocco, Julai 14, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Naye, Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda alisema kuwa benki hiyo isaidie kukuza mahusiano ya Tanzania na Morocco katika sekta ya kilimo hasa kwenye mazao kama vile Mchele, Tumbaku, kahawa na mazao mengine.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar Leila Muhamed Mussa amesema yapo maeneo ya fukwe ambayo hayajawekezwa mpaka sasa hivyo ni fursa kwa wawekezaji kuyatumia na kwamba Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefungua milango kwa wawekezaji.

Pia aliiomba benki hiyo kuona namna ya kuwawezesha wakulima wa viungo ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija.

Post a Comment

0 Comments