Naibu Meya Manispaa ya Musoma, Haji Mtete azindua Bismart Cup

Na Fresha Kinasa, Diramakini Blog

NAIBU Meya wa Manispaa ya Musoma Haji Mtete amewaasa Wazazi na walezi katika Manispaa hiyo kujenga tabia ya kuwapa fursa ya kushiriki michezo mbalimbali Watoto wao kwani kufanya hivyo ni kuwajenga kiafya, kiakili na kuwafanya wathamini fursa zitokanazo na michezo kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Naibu Meya wa Manispaa ya Musoma Haji Mtete akiongoza mazoezi ya kupasha misuli Moto kwa vijana wa Shule 12 ambazo zinashiriki michiano ya Bismart Cup' katika Manispaa ya Musoma.
Mh. mtete ameyasema hayo Septemba 11, 2021 wakati akizindua Mashindano ya Mpira wa miguu kwa wavulana ya 'Bismart Cup' yaliyoandaliwa na Taasisi ya elimu ya Bismart Brands Accademy iliyochini ya Mkurugenzi wake, Boniphace Ndengo. 

Ambapo yanafanyika katika Shule ya Msingi Mukendo iliyopo Manispaa ya Musoma yakishirikisha timu 12 za wanafunzi waliofanya mtihani wa taifa wa kuhitimu darasa la saba katika Manispaa hiyo huku timu ya Mukendo na Nyarigamba zikifungua michuano hiyo kwa kucheza mchezo wa kwanza.

Haji amesema, wazazi na walezi wana jukumu la kuthamini michezo na hivyo kuwaruhusu watoto wao kushiriki kwa ukamilifu kutokana na kuwa na mchango mkubwa katika kutatua tatizo la ajira kwa vijana, kuwajenga kiafya, kiakili pamoja na kudumisha mahusiano mema miongoni mwao na jamii kwa ujumla.
Pia, amewapongeza waandaaji wa mashindano hayo kwani yatawaandaa vijana kiafya, kuwajengea umoja na kuwaimarisha katika kuhakikisha wanakuwa wana michezo bora kwa siku za usoni. Huku akiwahimiza kuendelea kusoma kwa bidii na kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo ya elimu ikiwemo elimu, teknolojia, ubunifu na kukuza vipaji.

"Nimpongeze Mkurugenzi wa Bismart Brands Accademy, Boniphace Ndengo amekuwa mbunifu sana wa kuanzisha fursa mbalimbali ambazo zimekuwa zikitoa mchango mkubwa wa maendeleo ya vijana na kwa wakazi wa Musoma na Tanzania kwa ujumla. Niwaombe wananchi kutumia fursa ambazo amekuwa akizitoa kwa ajili ya manufaa,"amesema Mheshimiwa Mtete.

Mratibu wa mashindano hayo ya 'Bismart Cup', Mwalimu Michael Richard amesema,lengo la mashindano hayo ni kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana wanaopenda mchezo wa mpira wa miguu sambamba na kutangaza programu mbalimbali zinazotolewa na Bismart Brands Accademy kwa faida ya jamii.

Mwalimu Peter Getere ni kocha wa timu ya Nyarigamba inayoshiriki michuano hiyo, ambapo amepongeza Taasisi ya Bismart Brands Accademy kwa kuandaa mashindano hayo ambapo amesema yatakuwa na faida kwa vijana. Huku akitoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huo na kuweza kuandaa mashindano ili kuibua vipaji na kuviendeleza.

Pius Juma ni mkazi wa Kata ya Mukendo Manispaa ya Musoma, ambapo amesema kitendo kilichofanywa na Taasisi ya Bismart Brands Accademy kinatoa changamoto kwa wadau wengine wa elimu na michezo kufanya hivyo katika kuunga mkono juhudi za serikali kuandaa wanamichezo mahiri kwa siku za usoni.

Michuano hiyo ipo katika makundi mawili ambapo kundi 'A' linajukuisha timu za Mukendo, Nyarigamba,Nyasho,Rwamulimi, Nyamatare na Mtakuja. huku kundi 'B' likiwa na timu za Nyakato,Mwisenge,Kiara,Buhare, Kigera na Kamunyonge na fainali inatarajiwa kuchezwa Septemba 19, 2021 na mshindi atakabidhiwa zawadi.

Post a Comment

0 Comments