Rhobi Samwelly asisitiza umoja, mshikamano kwa wajumbe UWT

Na Fresha Kinasa, Diramakini Blog

Mjumbe wa Baraza la Wanawake Tanzania (UWT) Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly amewaasa Wajumbe wa Baraza la UWT Wilaya ya Musoma Mjini kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwao pamoja na kusimamia uhai wa jumuiya hiyo kwa kuongeza wanachama wapya katika maeneo yao na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla.
Mjumbe wa Baraza la UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly akizungumza na Wajumbe wa UWT Wilaya ya Musoma Mjini kushoto kwake ni Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Wilaya ya Musoma Mjini, Stella Majani na viongozi wengine wa jumuiya hiyo.

Rhobi ameyasema hayo Septemba 3, 2021 wakati akizungumza katika kikoa cha kawaida cha Baraza la UWT Wilaya ya Musoma Mjini kilichofanyika Kata ya Nyakato Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Ambapo pamoja na mambo mengine, ameahidi kushirikiana na jumuiya hiyo mkoani humo kwa kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo itakayowaingizia kipato ndani ya jumuiya na kukuza uchumi wa wanawake.

"Kama jumuiya tunapaswa kuongeza wanachama wengi zaidi, tuwahamasishe kinamama wajiunge, na pia ni muhimu kuwa miradi ambayo itawasaidia Wanawake ndani ya jumuiya na mabinti ambao wanakuwa na changamoto za kiuchimi. Uchumi unapokuwa mzuri katika familia hata vitendo vya ukatili wa kijinsia vitapungua, kama ambavyo Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imeeleza kuimarisha maisha bora ya wananchi lazima tuitekeleze kwa pamoja kwa kushirikiana kubuni na kuibua miradi yenye tija kwetu sote,"amesema Rhobi.
Wajumbe wa Baraza la UWT Wilaya ya Musoma Mjini wakifuatilia hotuba ya Mjumbe wa Baraza la UWT taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly katika kikao cha kawaida kilichofanyika Kata ya Nyakato Manispaa ya Musoma.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Musoma Mjini, Stella Majani akifungua kikao cha kawaida cha jumuiya hiyo kilichofanyika Kata ya Nyakato Manispaa ya Musoma kushoto kwake ni Katibu wa UWT Mkoa wa Mara, Sarah Kailanya. Kulia ni Mjumbe wa Baraza la UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly.

Aidha, amesema atashirikiana na jumuiya hiyo katika kusimamia Maendeleo ya Wanawake na Watoto wa kike ikiwemo kupinga mila kandamizi dhidi yao katika kuhakikisha wanafikia malengo bora sambamba na kuunga mkono juhudi za maendeleo za Rais Samia Suluhu Hassan kwa vitendo Kupitia fursa za kiuchumi na kusomesha Watoto wa kike waje kuwa Viongozi katika jamii na taifa kwa siku za usoni.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa (UWT)Wilaya ya Musoma Mjini, Stella Majani amewaomba wajumbe wa baraza hilo katika kata zote kuendelea kuhamasisha wananchi na wanachama wa CCM katika maeneo yao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona sambamba na kuhamasisha wananchi kuzingatia miongozo yote ya Serikali kwa ufanisi.

"Kuanzia Septemba 6, mwaka huu tutaanza kutembea tawi kwa tawi, kata kwa kata kuhamasisha kinamama kuchanja kwa hiari na kuwahimiza uzingatiaji wa taratibu zote za afya kama ambavyo Serikali imekuwa ikitoa maelekezo kusudi kwa pamoja tushiriki kupambana na janga hili. Huku tukisisitiza uhai wa chama na wananchi kuwajibika kufanya kazi halali za maendeleo,"amesema Majani.
Mjumbe wa Baraza la UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly akimkabidhi hati ya kiwanja Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Wilaya ya Musoma Mjini, Stella Majani wengine ni viongozi wa jumuiya hiyo akiwemo Katibu wa UWT Wilaya ya Musoma Mjini na pembeni kulia ni Katibu wa jumuiya hiyo Mkoa wa Mara Sarah Kailanya.
Mjumbe wa Baraza la UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly kushoto katikati ni Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Wilaya ya Musoma, Stella Majani na kulia ni Sarah Kailanya ambaye ni Katibu wa UWT Mkoa wa Mara. (Picha zote na DIRAMAKINI BLOG).

Sarah Kailanya ni Katibu wa UWT Mkoa wa Mara ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la UWT Wilaya ya Musoma amewataka watendaji wa jumuiya hiyo kuendelea kufanya kazi za jumuiya kwa ufanisi unaotakiwa na kuhamasisha ulipaji ada.

"Kupitia kikao hiki watendaji wa UWT Katika maeneo yenu nendeni mkafanye kazi ya kuimarisha jumuiya, kakaeni na mabaraza katika ngazi za kata na matawi kusudi kujiimarisha zaidi," amesema Kailanya.

Katika kikao hicho, Mjumbe wa Baraza la UWT taifa Mkoa wa Mara Rhobi Samwelly amekabidhi hati namba 646989 ya kiwanja namba 185 Block G, kilichopo Kata ya Kamunyonge kwa Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Musoma Mjini, Stella Majani kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya jumuiya hiyo.

Post a Comment

0 Comments