Manchester United yalipiza kisasi kwa Tottenham Hotspur

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Klabu ya Manchester United imeanza kurejesha faraja kwa mashabiki wake baada ya kutembeza kichapo kikali kwa Tottenham Hotspur.
Ni kupitia mtanange ambao umepigwa Oktoba 30, 2021 katika dimba la Tottenham Hotspur ambapo Cristiano Ronaldo alianza kuziumiza nyavu za Tottenham ndani ya dakika 39 katika kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo ndani ya dakika 64, Edinson Cavani aliachia mkuki wa moto hadi kwenye nyavu za Tottenham, dakika ya 86, Marcus Rashford alifunga mahesabu kwa goli safi, hadi dakika tisini zinakatika, Man United walichukua alama tatu zilizosindikizwa na mabao matatu kwa sufuri.

Ushindi huo umetibu majeraha ya wiki iliyoitwa wiki nyeusi na kocha Ole Gunnar Solskjaer baada ya kipigo kizito cha Liverpool.

Vijana hao walishindwa kupumua kwa Liverpool baada ya kucharazwa bakora tano za nguvu ambapo wao waliambulia sufuri.

Mabao ya Liverpool yalifungwa na Naby Keita ndani ya dakika ya tano, Diogo Jota ndani ya dakika 13, Mohamed Salah ndani ya dakika 38, 45, na dakika ya 50 ambapo Paul Pogba ndani ya dakika 60 alipigwa kadi nyekundu. Mtanange huo ulipigwa katika dimba la Old Trafford.

Ushindi huo unaifanya Manchester United kukwea mpaka nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na alama 17, ushindi ambao pia unafanya kazi ya Ole Gunnar Solskjaer Man United kuendelea kuwa na matumaini.

Post a Comment

0 Comments