TARURA inavyorejesha faraja kwa wananchi wa Kilindi kupitia barabara ya lami

NA YUSUPH MUSSA

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Bokwa, Kata ya Bokwa, Tarafa ya Kwekivu, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga wamesema hawakufikiria kama siku moja watakuja kuona barabara ya lami ikifika kijijini kwao ama wilaya hiyo ikiwa na lami.Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Mhandisi Martin Mwashambwa (kulia) akiangalia ujenzi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kipande cha mita 400 katika Kijiji cha Bokwa, Kata ya Bokwa mjini Songe ikiwa ni sehemu ya mradi wa kilomita tano kutoka Bokwa- Lengatei wilayani Kiteto mkoani Manyara. (Picha na Yusuph Mussa).

Wakizungumza na DIRAMAKINI BLOG kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema wameshangaa kuona Serikali ikiweka lami kwenye baadhi ya barabara, huku baadhi ya barabara zikitengenezwa kwa kiwango cha changarawe kwa ajili ya kuwezesha wananchi kuweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi.

Mohamed Chambo (83) mkazi wa Kijiji cha Bokwa amesema, katika umri wake hajawahi kuona lami ikiwekwa kwenye wilaya hiyo, lakini sasa ameshuhudia ikiwekwa kwenye kijiji chake, na kusifu Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwezesha kuwatengenezea barabara za vijijini ili ziweze kuwasaidia kwenye shughuli zao za kila siku.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Mhandisi Martin Mwashambwa akizungumza na DIRAMAKINI BLOG kwenye eneo la ujenzi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kipande cha mita 400 katika Kijiji cha Bokwa, Kata ya Bokwa mjini Songe wilayani Kilindi ikiwa ni sehemu ya mradi wa kilomita tano kutoka Bokwa- Lengatei wilayani Kiteto mkoani Manyara. (Picha na Yusuph Mussa).

"Mimi nina miaka 83, lakini sijawahi kuona lami kwenye wilaya hii ya Kilindi. Lakini sasa naona barabara ya lami inapita kwenye kijiji chetu. Nimshukuru Rais (Samia Suluhu Hassan) na Serikali yake kwa kutuletea lami,"amesema Chambo.

Naye Habiba Yassin ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Bokwa, pamoja na kujengewa barabara ya lami, pia mradi huo wa barabara wa kilomita tano umewapa ajira hasa wanawake, kwani walijitosa kwenye ujenzi huo kwa kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kuchimba mitaro, kuokota mizizi, kuokota mawe makubwa ambayo hayatakiwi kuwepo kwenye ujenzi, ambayo pia wananchi waliyachukua na kuponda na kupata kokoto.

"Mradi huu wa barabara, pamoja na kwamba umeletwa ili tuwe na barabara nzuri, lakini sisi wakazi wa Kijiji cha Bokwa tumepata neema nyingi ikiwemo kufanya kazi mbalimbali. Sisi kama wanawake tuliweza kuchimba mtaro uliopo pembeni ya barabara. Pia tumeweza kuokota mawe, kusaidia mafundi na kuweza kulipwa. Na kuna akina mamalishe wanapika chakula kwa ajili ya wafanyakazi.

"Mimi mwenyewe nina watoto watatu, na wote wanasoma Shule ya Msingi Bokwa. Pesa ninayopata kwenye ujenzi huu wa barabara umeniwezesha kuwahudumia watoto wangu kwa kupata mahitaji muhimu. Hivyo tunaishukuru Serikali kutupatia barabara hii sababu imekuja na neema nyingi,"amesema Yassin.
Ujenzi wa mifereji ukiendelea kwenye barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kipande cha mita 400 katika Kijiji cha Bokwa, Kata ya Bokwa mjini Songe wilayani Kilindi ikiwa ni sehemu ya mradi wa kilomita tano kutoka Bokwa- Lengatei wilayani Kiteto mkoani Manyara. (Picha na Yusuph Mussa).

Meneja wa Wakala wa Barabara wa Mjini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Kilindi, Mhandisi Martin Mwashambwa amesema, mradi wa barabara kwa kiwango cha lami wa Bokwa wilayani Kilindi hadi Kata ya Lengatei, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara ni wa kilomita tano, na unatekelezwa kwa awamu.

Mhandisi Mwashambwa amesema Awamu ya Kwanza mradi huo unajengwa kwa mita 400, ambapo utekelezaji wake unafanywa chini ya mkandarasi JP Traders Ltd kutoka mkoani Dar es Salaam, na utagharimu sh. milioni 315, ambapo mradi umeanza Septemba 3, 2021 hadi Machi 3, 2022.Ujenzi wa mifereji ukiendelea kwenye barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kipande cha mita 400 katika Kijiji cha Bokwa, Kata ya Bokwa mjini Songe wilayani Kilindi ikiwa ni sehemu ya mradi wa kilomita tano kutoka Bokwa- Lengatei wilayani Kiteto mkoani Manyara. . (Picha na Yusuph Mussa).

"Barabara ya Bokwa- Lengatei ya kilomita tano, inajengwa kwa awamu. Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imetengewa sh. milioni 315 kwa ajili ya kutengeneza kipande cha mita 400, na kazi imeanza tangu Septemba 3, mwaka 2021, na inatarajiwa kukamilika Machi 3, 2022. Lakini kutokana na kasi ya mkandarasi JP Traders Ltd ya jijini Dar es Salaam, kazi hii inaweza kukamilika Januari, 2022.

"Ni kweli, sisi TARURA hii ni mara yetu ya kwanza kuweka lami kwenye Wilaya ya Kilindi. Na tutaendelea kuboresha barabara zetu kila tutakapopata fedha kutoka serikalini. Mfano barabara ya Bokwa- Lengatei kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imepata sh. milioni 315, lakini hatujui mwaka wa fedha 2022/2023 itatengewa kiasi gani cha fedha,"amesema Mwashambwa.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Mhandisi Martin Mwashambwa (kushoto) akiangalia ujenzi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kipande cha mita 400 katika Kijiji cha Bokwa, Kata ya Bokwa mjini Songe ikiwa ni sehemu ya mradi wa kilomita tano kutoka Bokwa- Lengatei wilayani Kiteto mkoani Manyara. Katikati ni Msimamizi wa Mradi Mhandisi Vedastus Buliro. (Picha na Yusuph Mussa).

Mwashambwa amesema Wilaya ya Kilindi ina mtandao wa barabara wa kilomita 871.59. Kati ya hizo, kilomita 59.72 ni za kiwango cha changarawe, na kilomita 811.8 ni za udongo. Lakini kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetoa sh. bilioni moja kwa ajili ya kufungua barabara, na kufanyia maboresho zile za udongo kuwa za changarawe. Pia kuna sh. milioni 500 ambazo nazo zitafanya kazi ya kutengeneza maeneo korofi na makaravati ili barabara zipitike mwaka mzima.

Naye Msimamizi wa Kampuni ya JP Traders Paul Michah amesema wanakwenda vizuri japo kokoto nyembamba kwa ajili ya uwekaji wa lami na shughuli nyingine wanazichukulia mbali, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, na watamaliza barabara hiyo ndani ya muda waliopangiwa.

Post a Comment

0 Comments