Bima ya Afya Elimu ya Juu ilivyogeuka mkombozi kwa wanafunzi nchini

NA GODFREY NNKO

"Bima ya Afya kwa wanafunzi wa elimu ya juu ni mkombozi wakati wa dharura. Huondoa wasiwasi wa gharama za afya. Na ukiwa na bima mara zote unakuwa mwenye ujasiri na uhakika wa matibabu saa 24;

Hayo yamebainishwa kwa nyakati tofauti na wanafunzi, wahadhiri, walimu, wazazi na walezi mbalimbali wakati wakizungumza na mwandishi wa makala haya kuhusiana na umuhimu wa bima ya afya kwa wanafunzi nchini.
Miongoni mwa viongozi wa Serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati akichangia mada katika kikao kazi kati ya NHIF na TAHILISO kilichofanyika Novemba 6,2021 katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupeana mrejesho wa usajili wa bima ya afya kwa wanafunzi.

Aidha, mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao unatoa bima ya afya kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, kati na ufundi nchini kwa lengo la kuwawezesha kupata huduma za matibabu kwa gharama nafuu.

Kwa mujibu wa NHIF, mwanafunzi aliyesajiliwa anapata huduma za matibabu kupitia kadi yake ya bima ya afya wakati wote anapokuwa masomoni na wakati wa likizo. Huduma hizo zinapatikana katika vituo vya matibabu zaidi ya 9,000 vilivyosajiliwa na NHIF nchi nzima.

Kwa nyakati tofauti wanafunzi, wahadhiri, walimu na wazazi wameelezea namna ambavyo bima ya afya ina nafasi kubwa katika maisha ya wanafunzi katika kipindi chote cha masomo yao.

Wanafunzi

Wanafunzi kutoka Chuo cha Taifa cha Utalii Bustani Campus jijini Dar es Salaam akiwemo Joseph Daffa,Winfrider Jeremiah na Petro Mhode wanasema kuwa, bima ya afya ni muhimu sana kwa mwana chuo kwani inampa uhakika wa kutibiwa kwenye vituo vikubwa vya afya.

"Na matibabu ambayo unapata huko si bora tu umepata matibabu, bali unapatiwa huduma bora ambazo zinakufanya uwe na faraja muda wote. Kwa hiyo nikiri wazi kuwa, bima ya afya inampa mwanachuo uhakika wa kutibiwa kwenye vituo vikubwa vya afya kwa huduma bora zaidi,"anasema Joseph Daffa ambaye ni miongoni mwa wanafunzi hao.

Kwa upande wake, Winfrider Jeremiah anasema kuwa, bima ya afya inayotolewa kwa wanafunzi na NHIF ni bora na ya uhakika, hivyo ombi lake ni kuona unawekwa mfumo ambao wanafunzi wote watajiunga na bima hiyo ili kuwapa uhakika wa matibabu.

"Serikali ikifanikiwa kulifanyia jambo hili kazi, hakika wanafunzi tutaendelea kufurahia huduma za matibabu kupitia bima ya afya na itatufanya wanafunzi tuwe tunapata huduma kwa haraka na kwa uhakika zaidi,"anasema Jeremiah.

Naye Petro Mhonde anasema kuwa, "awali ya yote niipongeze Serikali kwa kuona umuhimu wa bima ya afya kwa wanafunzi hapa nchini, hii ni huduma ambayo kamwe hauwezi kuichukulia poa, maana ukiwa na kadi yako ya bima ya afya umejipa uhakika wa kupata matibabu muda wowote na kwa haraka.
Miongoni mwa viongozi wa Serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati akichangia mada katika kikao kazi kati ya NHIF na TAHILISO kilichofanyika Novemba 6,2021 katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupeana mrejesho wa usajili wa bima ya afya kwa wanafunzi.

"Kubwa zaidi ninaiomba Serikali iangalie namna ya kuja na mfumo bora zaidi wa kuwafanya wanafunzi wawe wanapata bima kwa muda mfupi na waboreshe mifumo ya utoaji huduma kwa wanafunzi maana baadhi ya hospitali kumekuwepo changamoto ndogondogo ingawa haziwezi kutukwamisha kupata huduma ya matibabu,"anasema.

Oscar Tamba mwanafunzi Chuo cha Biblia Dodoma (CBC) anasema, bima ina faida kubwa pale unapougua ghafla, lakini hauna kipato, hivyo inasaidia zaidi tofauti na mfanyakazi.

"Pia kwa wenye kipato kidogo inasaidia kuokoa maisha yao pale wazazi wanapokuwa hawana fedha, badala ya kuanza kuhangaika kutafuta fedha inakuwa rahisi kupatiwa huduma za matibabu haraka,"amesema.

Pia amesema, kuna haja ya kutoa elimu kwa wanafunzi ili kujua umuhimu wa bima ya afya katika maisha yao hususani wawapo chuoni.

Frolence Mabula na Celvini Mbwambo wanasema, bima ya afya ina faida kubwa kwao,kwani unaweza kuumwa ghafla ikakusaidia sana katika matibabu.

Wamesema kuwa, bima imekuwa ikiwasaidia kwenye matibabu pale wanapokuwa hawana fedha za papo kwa papo, hivyo wanahimiza wanafunzi wengine wakate bima hiyo.

Kwa upande wake, Ester Hiza kutoka mkoani Kilimanjaro anasema kuwa,bima ya afya ina mchango mkubwa sana, "kwa sisi wanfunzi inapotokea tunapata tatizo lolote lile la kiafya ni rahisi sana kupata matibabu na dawa bila kipingamizi chochote na uangalizi wa juu zaidi wa daktari.

"Tunajivunia sana kuwepo kwa bima ya afya hususani kwa wanafunzi, maana inaturahisishia huduma za matibabu na pia inapunguza malakamiko ya wanafunzi kukosa huduma za matibabu kwa kukisa fedha,"anasema Hiza.
Mwanafunzi huyo anasema, jambo la kuboresha ni kuhakikisha kadi za bima zinafika kwa wakati vyuoni,"waboreshe system (mifumo) zao ili kuepuka kuweka taarifa zisizokuwa sahihi na mlengwa husika,watenge muda maalumu wa ufuatiliaji wa bima ya afya wa kuanglia uhitaji wa mteja,"anaongeza Hiza.

Wakati huo huo, mwanafunzi Halima Said kutoka mjini Moshi mkoani Kilimanjaro anasema kuwa, bima ya afya ni muhimu sana kwao wanafunzi na imewasaidia kupata huduma za matibabu pindi wanapougua wakiwa vyuoni bila usumbufu.

"Unajua ndugu mwandishi,gharama za matibabu ni kubwa sana kama mtu huna bima ya afya na kwa hali zetu za maisha ni ngumu kuwa na hela ya kulipa pindi mtu unaumwa, hivyo bima ya afya ina umuhimu sana kwetu sisi wanafunzi.

"Niipongeze sana Serikali kwa kuja na utaratibu huu, lakini kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa bima hiyo kwa wakati, lakini pia kumekuwa na tatizo la bima hizo kuandikwa tarehe za mwisho wa matumizi ambazo si sahihi.

"Mfano unakuta bima yako inaisha muda wake Januari 2022, lakini kwenye kadi imeandikwa Januari 2025, hii imekuwa ikichanganya wanafunzi wengi na kujikuta kadi inaisha muda kabla ya kuanza maandalizi ya kuipata nyingine na hivyo kukosa huduma.

"Tuombe wahusika wa bima waendelee kuboresha huduma zao na kuhakikisha tarehe za kuisha kadi zinaandikwa kwa usahihi na pindi wanafunzi wanapoomba zifike kwa wakati,"anasema Mwanafunzi huyo.

Walimu

Nao walimu kutoka chuo hicho cha utalii, Raban Lutengwa na Madam Zera wanasema kuwa, bima ya afya kwa wanafunzi ni muhimu sana kwani inamsaidia kila mmoja aliyejiunga kuepuka gharama za matibabu za papo kwa hapo katika hospitali, kituo cha afya na zahanati popote pale nchini.

"Bima ya afya kwa wanafunzi na hata Watanzania ni jambo la heri sana, hivyo nichukue nafasi hii kutoa wito kwa wanafunzi wote kuona umuhimu wa kujiunga na huduma hii ambayo imekuwa mkombozi kwao na imekuwa ikiwapunguzia gharama za mara kwa mara kwa ajili ya matibabu,"amesema Raban.

Mipango

Hivi karibuni Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu nchini (TAHLISO) walijadili na kukubaliana kuendelea kushirikiana kuhakikisha kila mwanafunzi wa chuo kikuu na cha kati anakuwa na kadi ya NHIF kwa uhakika wa matibabu. 

Aidha, TAHLISO imeipongeza NHIF kwa kutoa ushirikiano mkubwa katika kuwahudumia wananfunzi pale panapokuwepo na uhitaji.

Nkinda

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa TAHILISO, Frank Nkinda wakati akizungumza katika mkutano kati ya NHIF na viongozi wa shirikisho hilo uliofanyika Septemba, mwaka huu jijini Dodoma.

“Kwa kweli kabla sijawa kiongozi wa TAHLISO sikuwa naijua NHIF vema, lakini sasa nimeweza kuifahamu na naweza kujibu simu nyingi za wanafunzi ninazopokea wanapopata changamoto, lakini naushukuru uongozi wa NHIF unakuwepo kutatua matatizo pale zinapotokea,” amesema Nkinda.

Amesema, wao kama viongozi wa wanafunzi wako imara katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu ya kutosha kuhusu bima ya afya kwa wanafunzi ili kuwa uhakika wa matibabu awapo vyuoni.

“Nahimiza tuwe na mpango mathubuti wa kuhakikisha kuwa maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu ulazima wa wanafunzi wa vyuo vyote vikuu na vya kati nchini yanatekelezwa kwa vitendo,”amesema Nkinda.

Pia amesisitiza kuendelea kwa ushirikiano wa NHIF na viongozi wa wanafunzi katika vyuo, hivyo kuendeleza uhusiano mzuri ambao umejengwa ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali zinapojitokeza na kuondoa malalamiko ya yasiyokuwa ya msingi.

NHIF

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF,Bernard Konga wakati akifungua mkutano kati ya NHIF na viongozi wa shirikisho hilo uliofanyika Septemba, mwaka huu jijini Dodoma amesema, "niwakumbushe lengo hasa la mfuko kuanzisha mpango wa huduma za bima ya afya kwa wanafunzi lilikuwa ni kumuondolea mwanafunzi mzigo wa gharama za matibabu ili aweze kuwa na ujasiri wa kuendelea na masomo yake bila kikwazo cha afya yake akiwa chuoni na wakati wa likizo.
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF,Bernard Konga wakati akifungua mkutano kati ya NHIF na viongozi wa TAHILISO uliofanyika Septemba, mwaka huu jijini Dodoma.

“Naomba niwajulishe kuwa mfuko uko katika maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake na hatuwezi kusahau mchango wa kundi la wanafunzi ambao ni wadau wa mfuko na kuona njia bora ya kuweza kuendeleza ushirikiano mzuri uliyopo,"amesema.

Konga anasema kuwa, ufanisi wa utekelezaji wa mpango huu unategemea sana ushirikiano wa pande zote ikiwa ni wanafunzi wenyewe, chuo husika na mfuko huo. 

"Bila ushirikiano na kila upande kutekeleza wajibu wake ipasavyo hatuwezi kuepuka changamoto katika utekelezaji na mwathirika mkuu anakuwa mwanafunzi.Hata hivyo hapo nyuma kulikuwa na changamoto kubwa ya wanafunzi kukosa vitambulisho vya bima ya afya kwa wakati, changamoto ambayo kwa kiasi kikubwa imeshughulikiwa cha msingi ni kuendelea kuwa na ushirikiano kwenye kutekeleza hilo,"amesema Mkurugenzi Mkuu huyo.

Wazazi

Kwa upande wao wazazi na walezi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam wamesema kuwa, bima ya afya kwa wanafunzi wakiwa vyuoni ni jambo muhimu, kwani si tu kwamba inawapunguzia gharama za matibabu kwa watoto wao bali inawapa nafasi ya kujipanga kwa ajili ya mambo mengine.

"Si muda wote mzazi au mlezi anakuwa na fedha mkononi, wakati mwingine unaweza kukuta mwanafunzi anaumwa ghafla, mfukoni hauna kitu, unajikuta unaumiza kichwa na hauna la kufanya ikizingatiwa gharama za matibabu zipo juu sana,ukiwa umemkatia bima ya afya badala ya kuwaza, unaendelea kuwajibika kwa mambo mengine ya maendeleo ya familia,"anasema Julius Tarimo mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam.

Tarimo anaongeza kuwa, bima ya afya ni usalama si kwa wanafunzi peke yao bali pia kwa familia, hivyo amesisitiza kila jamii kutambua umuhimu wa kuwa na bima ya afya hususani inayotolewa na NHIF ambayo inawapa uwanda mpana wa kupata matibabu popote pale nchini.

Naye Sauda Khamis mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam anasema, bima ya afya kwa wanafunzi wa elimu ya juu ni kipaumbele muhimu kama ilivyo ada na mahitaji mengine kwa mwanafunzi.

"Ukiwa na bima ya afya chuoni, wewe ni shujaa, kwani unafanya masomo yako kwa ujasiri na uhakika. Unakuwa hauna hofu wala wasiwasi pindi inapotokea dharura ya ugonjwa, wewe likitokea jambo lolote linalotatiza afya yako unachukua kadi yako na mara moja unakwenda kupata matibabu katika kituo unachoona kinakufaa, hilo ni jambo la kheri sana, hivyo wazazi na walezi wenzangu yafaa tuhakikishe watoto wetu wanapata bima ya afya wakiwa vyuoni kwa uhakika wa matibabu ya haraka,"amesema Khamis.

Kwa upande wake Ernest Thomas mkazi wa Ilala anasema kuwa, inafaa NHIF kuja na bima jumuishi na shirikishi kwa wanafunzi wote kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu.

"Bima hiyo inaweza kuwa na gharama tofauti kulingana na ngazi ya elimu ya mwanafunzi, hii itasaidia hata wale ambao wapo shule za awali hadi huko vyuo kupata kadi ya bima ya afya ambayo inawapa uhakika wa matibabu, na ikiwezekana Serikali ije na sheria ya kumtaka kila mwanafunzi nchini awe na bima ya afya, hii itasaidia sana maana watoto wanaumwa sana na wakati mwingine wamekuwa wakikosa matibabu kwa wakati kutokana na hali ya uchumi ya wazazi wao," anasema Thomas.

Wahadhiri

Profesa Fadhili Ngumia ambaye ni Mhadhiri wa Chuo cha Mipango Dodoma amesema kuwa, huduma hiyo inasaidia pale unapokuwa hauna fedha mfukoni na inasaidia kutibiwa kwa gharama ndogo kuliko ambavyo hauna pesa, lakini pia bima inasaidia kuleta maendeleo ya nchi bila afya huwezi kufanya kazi.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Faustine Bee amesema kuwa, bima inafaida kubwa kwa jamii na vyuoni kwa wanafunzi na watumishi.

"Bima inasaidia kupata matibabu.Kila mtu anapata hata kama hana fedha keshi ila changamoto kubwa ni uelewa mdogo kwa vijana juu ya bima. Hivyo, NHIF inapaswa kufanya kazi kubwa ya kutoa elimu,"amesema.

Anaongeza kuwa, "wakati mwingine utakuta mwanafunzi hawezi kutunza kadi ya bima kiusahihi.Wengi hawawezi kutunza, lakini pale wanapopata changamoto huwa wanaanza kuhangaika.

"Serikali ijitahidi kuongeza wigo zaidi na kupunguza ada na makato ili watu waweze kujiunga na kulipia bima huku elimu ikiendelea jutolewa ili kupunguza magonjwa mengi,"amesema.

Kwa upande wake Dkt. Lameck Mashalla ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Utawala Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo amesema, bima ya afya inasaidia kwenye kulipia matibabu kwa wepesi hata wakienda likizo wanafaidika nazo kwenye vituo mbalimbali vya afya.

Amesema, Serikali inapaswa kuona haja ya kuboresha kwenye ulipaji wa fedha kwa wanafunzi kwa kuangalia namna ya kulipa kwa semister ili kulipia nusu na akimaliza mwaka amalize nyingine ili kuwasaidia wanafunzi kujitokeza kwa wingi,kwani huwa wanakuwa na changamoto ya kiuchumi.

UDSM

Mshauri wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),Paulina Mabuga anasema, wanafunzi wengi wa vyuoni hususani wa 'undergraduate' wameweza kupata mafanikio makubwa katika usajili wa bima ya afya.

Anasema, miongoni mwa mafanikio haya ni pale mwanafunzi anapoumwa ghafla kutohangaika, kwani inamfanya kwenda moja kwa moja hospitalini.

"Huu mpango uliowekwa na Serikali wa lazima mwanafunzi kukata bima ya afya moja kwa moja ni mzuri sana, kwani wanafunzi walikuwa wanapata shida miaka ya nyuma,"anasema na kuongeza,

"Kabla ya mpango huu kuwepo iliwafanya wanafunzi watoe hela na gharama za matibabu unakuta ni kubwa na kushindwa kuzimudu,"anasema Mabuga.

Anasema, changamoto zipo ila sio kubwa kwa wanafunzi ikiwemo wanafunzi kuchelewa kujisajili, hivyo inamlazimu anapougua kutumia hospitali ya chuo.

Anasema, pia baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakichelewa kukata bima mapema hadi pale wanapougua ndio ukumbuka kukata bima ambapo inawafanya kulipia kwa gharama.

"Utakuta mwanafunzi anaumwa jino leo na daktari kamwambia afanye operesheni hapo ndipo mwanafunzi anakurupuka kukataa bima, wakati inakuwa kachelewa na anapaswa kusubiri kwa muda ndiyo apate bima hiyo,"anasema.

Anasema, wanafunzi pia wamekuwa wana changamoto ya kutochukua kadi zao mapema katika maeneo husika hadi pale wanapoumwa.

Post a Comment

0 Comments