Miaka 60 ya Uhuru:Tanzania yakamata tani 356 za dawa za kulevya

NA AHMED SAGAFF- MAELEZO

SERIKALI ya Tanzania imekamata tani 356 za dawa za kulevya kuanzia mwaka 2017 hadi 2021.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Bw. Gerald Kusaya alipozungumza na wanahabari kuhusu mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

"Mamlaka toka kuanzishwa kwake mwaka 2017 hadi kufikia mwishoni mwa Septemba 2021 kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ilifanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 45,784 wa dawa za kulevya, kilogramu 356,563.1 za dawa za kulevya pamoja na kuteketeza ekari 628.75 za mashamba ya bangi," alieleza.

Akitoa ufafanuzi, Bw. Kusaya ameitaja bangi kuongoza katika orodha ya dawa za kulevya zilizokamatwa.

"Dawa za kulevya zilizokamatwa ni kilogramu 1,125.41 za heroin, kilogramu 26.67 za cocaine, kilogramu 199,740 za bangi, kilogramu 97,640 za mirungi, kilogramu 57,600 za kemikali bashirifu na kilo 431.02 za methamphetamine," amesema.

Kamishna Jenerali Kusaya amesema nini?

>Amesema, tatizo la dawa za kulevya limekuwepo nchini kwa muda mrefu tangu baada ya kumalizika kwa vita kuu ya pili ya Dunia. 

Aidha, amesema liliongezeka zaidi katika kipindi cha miaka ya 90 na kuilazimu Serikali kuanzisha Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini ambayo ilianzishwa na Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya Mwaka 1995.

>Tume hiyo ilianza kazi mwaka 1997 kwa lengo la kuratibu wadau wanaohusika na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya nchini.

>Serikali katika kuimarisha udhibiti na mapambano dhidi ya dawa za kulevya, amesema ilipendekeza kutungwa kwa sheria mpya ambayo mwezi Aprili mwaka 2015, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015.

>Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 chini ya Kifungu cha 3 ilianzisha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambayo ilianza kazi rasmi mwezi Februari, 2017.

>Majukumu ya mamlaka ni kufafanua, kuhamasisha, kuratibu na kutekeleza hatua zote zinazolenga katika udhibiti wa dawa za kulevya, matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya nchini.

Mafanikio je?

>Kamishna Jenerali Kusaya amesema, tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambayo ilichukua nafasi ya iliyokuwa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya ambapo jukumu lake la msingi lilikuwa ni kuratibu pekee jitihada za kupambana na dawa za kulevya nchini zimeleta matokeo chanya.

>Mamlaka toka kuanzishwa kwake mwaka 2017 hadi kufikia mwishoni mwa Septemba 2021 kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ilifanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 45,784 wa dawa za kulevya, kilo 356,563.1 za dawa za kulevya pamoja na ekari 628.75 za mashamba ya bangi ziliteketezwa.

>Mchanganuo wa watuhumiwa na uzito wa dawa za kulevya zilizokamatwa ni kama ifuatavyo; Watuhumiwa 2,231 walikutwa na Heroin, 502 walikutwa na Cocaine, 37,743 walikutwa na Bangi, na 5,308 walikutwa na Mirungi.

>Dawa za kulevya zilizokamatwa kwa uzito ni Kilogramu 1,125.41 za heroin, Kilogramu 26.67 za cocaine, Kilogramu 199,740 za bangi, Kilogramu 97,640 za mirungi, Kilogramu 57,600 za Kemikali Bashirifu, na Kilo 431.02 za Methamphetamine

>Aidha, ukamataji uliofanyika tarehe 24 Aprili, 2021 wa kilo 859.36 za dawa za kulevya ukihusisha watuhumiwa 7 raia wa Iran katika Bahari ya Hindi eneo la Kilwa Masoko mkoani Lindi umevunja rekodi na kuwa ukamataji wa kwanza wa kilo nyingi toka nchi yetu ipate uhuru.

>Vilevile, jumla ya kilo 2,192.9 za Heroin, kilo 390.8 za Cocaine na kilo 431.02 ya Methamphetamine zilikamatwa katika kipindi cha mwaka 2011 hadi 2021. Kamishna Jenerali Kusaya amesema, ukamataji wa Heroin umekuwa mkubwa zaidi ikilinganishwa na dawa za kulevya aina ya Cocaine na Methamphetamine

>Mamlaka katika kutekeleza Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, ilifanikisha kufunguliwa jumla ya kesi 6,894 katika Mahakama mbalimbali Nchini. Jumla ya kesi 336 zilitolewa maamuzi mahakamani na kati ya hizo Jamhuri ilishinda kesi 243.

>Mamlaka kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Kimataifa kama vile United Nations Office On Drugs and Crime (UNODC), Interpol, Drug Enforcement Administration (DEA) na National Crime Agency (NCA) imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuvunja na kudhoofisha mitandao mikubwa ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya ndani na nje ya nchi.

>Jitihada za Serikali za kupambana na dawa za kulevya zimefanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya nchini ambapo kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2019 ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), nchi ya Tanzania ilifanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kutoka Nchi zalishaji kwa zaidi ya asilimia 90.

>Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na taasisi zingine zisizo za kiserikali imefanikiwa kupanua huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya nchini.

>Huduma hii, ilianza rasmi Nchini mwaka 2011 ambapo hadi 2016 kulikuwa na vituo vitatu tu nchini ambavyo vilihudumia waathirika 3,500. Tangu kuanzishwa kwa Mamlaka mwaka 2017, kumekuwa na ongezeko la vituo nane zaidi na hivyo kufanya jumla yake kuwa vituo kumi na moja (11) mpaka sasa vikihudumia zaidi ya waathirika 10,565 kila siku.

>Vilevile, Mamlaka imekuwa ikisimamia upatikanaji wa uhakika wa dawa ya methadone kwa ajili ya tiba ya waraibu wa Heroin kwa kusimamia uagizaji, usambazaji na udhibiti wake. Aidha, wenye matatizo yaliyosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya wapatao 169,269 walipatiwa huduma za tiba katika Vitengo vya afya ya akili Nchini.

>Mamlaka kwa kushirikiana na Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi iliyopo Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa programu ya Kukuza Ujuzi kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya waliopata nafuu. Shabaha ya kwanza ni vijana wapatao 200 walio kwenye matibabu kwenye Kliniki za Methadone ambao watapatiwa nafasi katika vyuo vya VETA, SIDO na vinginevyo kulingana mahitaji yao ya fani mbalimbali.
Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Bw. Gerald Kusaya. (Picha na Maktaba).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news