Watupa taka ovyo kulipa 50,000/- papo kwa papo jijini Tanga

NA HADIJA BAGASHA

JIJI la Tanga linaandaa sheria ya mtu akikutwa anatupa takataka awapo katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo, akikamatwa atalazimika kulipa faini ya papo kwa papo ya sh. 50,000 ili kulinda ubora na usafi wa mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Meya wa Jiji hilo Abdulhaman Shilow, alisema katika kukabiliana na watupa taka hovyo katika mitaa, wataajiri vijana 50 ambao watakuwa mitaani kuwafizia watu wanaotupa taka.

Shilow alikuwa akizungumza ushindi wa kwanza walioupata kwa usafi wa mazingira ambapo walipewa kombe, cheti na shilingi milioni 2 hatua ambayo wanaona ili kulinda ushindi huo ni kuhakikisha wanatekeleza sheria hiyo.
"Kuanzia Januri mwakani tutaanza sheria ya kuwakamata watu wanaotupa takataka hovyo na kuwapiga faini ya sh. 50,000 papo hapo.Na tutatoa ajira kwa vijana 50 ambao watahusika katika ukamataji huo," alisema.

Hata hivyo, Meya alisema ushindi wa kwanza kwa Jiji hilo haukuja bahati bali wameshirikiana viongozi, wananchi na wadau mbalimbali ambao wamefanikisha suala la usafi wa mazingira katika mitaa mbalimbali.
Amewataka wananchi washirikiane na viongozi katika kuhakikisha wanatunza maeneo yao na kiasi cha sh 2,000 wanacholipia kwa mwezi kwa kila kaya, waendelee kulipa ili kazi ya kusafisha mitaa iwe rahisi.

Jiji la Tanga limekuwa la kwanza kwa usafi wa mazingira likifuatiwa na Arusha huku Jiji la Mwanza likishika nafasi ya tatu.

Post a Comment

0 Comments