Rais Dkt.Mwinyi awaachia jukumu wanasheria nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza matumaini yake kuwa, iwapo dhana ya Uchumi wa Buluu itaeleweka vyema kutakuwa na nafasi nzuri ya kurekebisha na kuboresha sheria na taratibu za Mahakama katika safari ya kuujenga uchumi wa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akipandisha bendera ya Mahakama Kuu Tanzania katika hafla ya Ufunguzi wa Wiki ya Sheria iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma leo Januari 23, 2022,kushoto kwa Rais ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe.Dkt. Tulia Ackson. 

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Januari 23, 2022 katika Uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria uliofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma uliokwenda sambamba na uzinduzi wa Nembo pamoja na Bendera ya Mahakama.

Ameeleza kwamba kwa lugha nyingine sheria na taratibu za Mahakama zilizopo lazima ziendane na mipango iliyopo ya Serikali yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi kupitia Uchumi wa Buluu.
"Mimi binafsi nitafurahi sana kama wanasheria kutoka pande zote mbili za Muungano, mtakuwa na mijadala ya dhati kuhusu ni kwa kiasi gani, sheria na taratibu za kimahakama zinavyoweza kuboresha kwa lengo la kufanikisha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane ya ujenzi wa Uchumi wa Buluu,"amesema Dkt.Mwinyi.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amerejea kauli yake aliyoitoa Novemba 11,2020 katika hotuba ya uzinduzi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar pale aliposema kwamba Wazanzibari hawana budi kuigeuza bahari kuwa ndio shamba lao kwani huko ndiko fursa za ajira za Zanzibar mpya zilizopo ambapo pia, huo ndio msingi wa dhana nzima ya Uchumi wa Buluu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiondoa kipazia kuashiria kuizindua Nembo ya Mahakama Kuu Tanzania wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Wiki ya Sheria Tanzania iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma huku akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.Ibrahim Hamis Juma. (Picha na Ikulu).

Amesisitiza kwamba Zanzibar haikujaaliwa ardhi kubwa kwani ni nchi ya visiwa ambapo idadi ya watu wake imeongezeka mara tano katika kipindi cha miaka 56 ambapo mwaka 1964 Wazanzibari walikuwa laki 3 tu ambapo hivi sasa wapo takribani milioni 1.6. 

Katika hotuba hiyo Rais Dkt. Mwinyi alitoa wito kwa Wanasheria na wataalamu wa sheria, viongozi wa Mahakama na watumishi wa sekta za sheria kuielewa na kuifanyia kazi mipango mikuu ya uchumi wa Tanzania na kuwa huru kutoa ushauri wa kisheria Serikalini kwa lengo la kuifanikisha.
Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, Serikali zote mbili zinatambua kwamba zipo sheria ambazo huenda zikawa ni kikwazo cha kufikia matarajio ya kiuchumi na ustawi wa jamii ambapo sheria hizo zinahitaji kufanyiwa mabadiliko ili zifamikishe mipango ya uchumi wa kisasa.

Hivyo, amewahimiza wadau hao wa sheria, kutumia utaalamu wao kuzishauri Serikali zote mbili kuchukua hatua za kurekebisha sheria ambazo zina kasoro na kufanya hivyo kwa maslahi mapana ya Tanzania na Watanzania wote.

Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa kwa upande wa Zanzibar dhamira ya Serikali ya kujenga uchumi wa kisasa unaozingatia matumizi sahihi ya rasilimali za bahari au kama unavyofahamika Uchumi wa Buluu, ambazo ni jitihada za dhati kabisa za kujenga uchumi utakaowasaidia wananchi wa Zanzibar. 
Alieleza kwa upande wa pili ambako kuna dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kupunguza umaskini na kuwa na uchumi unaolingana na ushindani wa Karne ya 21.

Kutokana na juhudi hizo, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kwamba ni dhahiri kuwa kufanikiwa kwa dhamira na jitihada hizo za Serikali zote mbili kutategemea uwezeshaji na mchango mkubwa wa sekta ya sheria na hasa kupata ushauri wa kutoka kwa wanasheria wa hapa nchini.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo ya uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Siku ya Sheria, kukumbusha umuhimu wa kuzingatia maadili katika utoaji haki.

Alieleza kwamba amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria kwa vile anatambua kuwa miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya utawala bora ni kuwepo wka vitendo vya rushwa, ubadhirifu,uzembe,kukosa uwajibikaji na kutofuata sheria na kukiuka kwa maadili.

"Nafahamu kwamba sheria ina umuhimu mkubwa katika kujenga umoja wetu,amani yetu, udugu wetu, na pia mshikamano wetu, mafanikio ya kiuchumi, kibiashara na kiuwekezaji hutegemea kuwepo kwa misingi ya utawala wa sheria na uhuru wa Mahakama,"amesema Dkt.Mwinyi.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi alieleza kuridhishwa na hatua ya ushirikiano iliyopo baina ya Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mahakama ya Zanzibar ambapo uhusiano huo ni wa muda mrefu tokea mwaka 1965.

"Nafurahi kuona kuwa ushirikiano huo unaendelezwa kwa kupeana uzoefu na utaalamu utakaoongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu hivyo natoa wito kuendeleza kwa lengo la kuwa chachu ya kuleta mabadiliko ya utendaji na kuongeza kasi ya ufanisi katika mahakama zetu," amesisitiza Dkt. Mwinyi.

Naye Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma alieleza kwamba Wiki ya Sheria itakuwa na mambo mbalimbali ya kisheria hadi tarehe 29 na siku ya Sheria itakuwa Februari 1,2022 ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Amewakaribisha wananchi kwenda katika maonyesho hayo yaliyozinduliwa na Rais Dkt.Mwinyi ili waweze kupata mahitaji yao mbali mbali ya kisheria.

Jaji Mkuu huyo ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa kuimarisha sheria ikiwa ni pamoja na kuimarisha Uchumi wa Buluu ambao utahitaji mabadiliko ya sheria huku akiahidi ushirikiano mkubwa katika kuhalikisha dhana hiyo inafikia malengo yaliyokusudiwa sanjari na kuimarisha mashirikiano ya Kimahakama kati ya pande mbili hizo.

Pia, aliwasisitiza wananchi kuwa na utamaduni wa kujisomea hasa katika sheria huku wakiwataka wajitayarishe kwa kutumia mfumo wa akili bandia” katika kutoa ushauri wa kisheria jambo ambalo linakwenda na wakati uliopo hivi sasa pamoja na kupunguza kharama za kuendeshea kesi. 

Mapema asubuhi, Rais Dkt. Mwinyi aliongoza matembezi ya kilomita saba yaliyoanzia katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Haki, Jijini Dodoma na kupita katika maeneo mbali mbali na hatimae kuishia katika viwanja vya Nyerere Square ambapo Mama Maria Mwinyi nae alishiriki kikamilifu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akifanya mazoezi ya viungo katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma, kabla ya kuaza kwa Matembezi ya Ufunguzi wa Wiki ya Sheria na( Kushoto kwa Rais) Jaji Mkuu wa Tanzania Prof Ibrahim Hamis Juma na (kulia kwa Rais) Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mhe Dkt. Tulia Ackson , Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi, wakiwa na Viongozi wengine wa Serikali na Mahakama. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika matembezi ya Ufunguzi wa Wiki ya Sheria Tanzania inayofanyika Jijini Dodoma katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma na (kushoto kwa Rais) Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Prof Ibrahim Hamis Juma na Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla na (kulia kwa Rais) Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mhe Dkt. Tulia Ackson, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Anthony Mtaka, wakishiriki katika matembezi hayo yalioazia Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kumalizika katika viwanja vya Nyerere Square Dodoma 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akifanya mazoezi baada ya kumaliza matembezi ya Ufunguzi wa Wiki ya Sheria Tanzania yalioazia katika Kituo Jumuisho cha Utoaji Haki na kumalizia katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma na (kushoto kwa Rais) Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma na Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe.Khamis Ramadhan Abdalla na (kulia kwa Rais) Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.George Boniface Simbachawene. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akitembelea maonesho ya Ufunguzi wa Wiki ya Sheria Tanzania, katika banda la Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) akipata maelezo kutoka kwa Afisa Mradi Bi. Asha Hassan Komba na (kulia kwa Rais) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Prof Ibrahim Hamis Juma, maonesho hayo yanafanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk,Hussein Ali Mwinyi akitembelea banda la maonesho la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria,Bw.Stanislavs Kagisa na (kulia kwa Rais) Mke wa Rais Zanzibar Mama Mariam Mwinyi, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.George Boniface Simbachawene. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk,Hussein Ali Mwinyi akitembelea banda la maonesho la Wizara ya Katiba na Sheria akipata maelezo kutoka kwa Dr.Anne Malipula na (kulia kwa Rais) Mke wa Rais Zanzibar Mama Mariam Mwinyi, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Sheria Tanzania yanayofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.  Wageni waalikwa wakifuatilia hituba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) akihutubia na kufungua Wiki ya Sheria Tanzania iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma. 
Baadhi ya Waheshimiwa Majaji wa Mahkama Kuu Tanzania wakifuatilia hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kufungua Wiki ya Sheria Tanzania iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.   

Baada ya kufika katika eneo hilo la uzinduzi huo, Rais Dkt. Mwinyi alitembelea mabanda ya maonyesho pamoja na kuzindua rasmi bendera na Nembo ya Mahakama. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news