Naibu Waziri Ridhiwani Kikwete awafikia wananchi walioathiriwa na mvua, atoa pole

NA MUNIR SHEMWETA- WANMM 

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete ametembelea baadhi ya maeneo yaliyoathirika na mvua iliyoambatana na upepo kwenye jimbo la Chalinze mkoani Pwani na kutoa pole kwa wote walioathirika na mvua hizo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze mkoa wa Pwani,Ridhiwani Kikwete akiwa ndani ya moja ya nyumba iliyoathirika na mvua katika kijiji cha Makombe, Chalinze mkoani Pwani alipokwenda kutoa pole na kujionea athari za mvua. 

Usiku wa kuamkia Januari 20, 2022 ilinyesha mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kwenye maeneo mbalimbali ya mikoa ya Pwani na Dar es Salaam ambapo katika jimbo la Chalinze mkoa Pwani takriban nyumba 36 zikiwemo shule mbili za msingi za Makombe na Bwilingu ziliathirika.

Naibu Waziri wa Ardhi Ridhiwani Kikwete ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Jumamosi ya Januari 22, 2022 alitembelea familia za waathirika pamoja na shule mbili za msingi ambazo mapaa yake yaliezuliwa na mvua hizo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze mkoa wa Pwani, Ridhiwani Kikwete akiangalia moja ya nyumba iliyoathirika na mvua katika kijiji cha Makombe, Chalinze mkoani Pwani alipokwenda kutoa pole na kujionea athari za mvua

Akiwa katika kijiji cha Makombe kilichopo kata ya Lugoba, Chalinze mkoani Pwani, Ridhiwani alijionea athari iliyosababishwa na mvua hizo ambapo aliwafariji waathirika na kuwaeleza kuwa, yeye kama mbunge kwa kushirikiana na Halmashauri ya Chalinze wataangalia namna ya kuwasadia wale walioathirika na kadhia hiyo ili waweze kurudi katika maisha yao ya kawaida.

“Binafsi yangu nieleze nimesikitishwa na janga lililotokea lakini wakati mwingine tuamini kila jambo limepangwa na Mwenyezi Mungu na lina sababu zake nyingi,”amesema Ridhiwani.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze mkoa wa Pwani Ridhiwani Kikwete akimsikiliza mmoja wa waathirika wa maafa ya mvua (aliyevaa kilemba) katika kijiji cha Makombe, Chalinze mkoani Pwani alipokwenda kutoa pole na kujionea athari za mvua.

Akiekezea uharibifu uliotokea kwenye shule ya Msingi Makombe, Ridhiwani ameagiza kufanyika jitihada za haraka ili kuyarejesha madarasa yaliyoathirika kurudi katika hali yake ya kawaida ili wanafunzi waweze kuyatumia kwa kuwa tayari shule zimefunguliwa.

“Binafasi namshukuru Mungu kwa sababu katika taarifa yenu hatukupata taarifa ya mtu aliyeumizwa kwa sababu wakati mwingine inapotokea wanafunzi wako darasani inakuwa ni hatari sana na kushukuru chama kwa kutoa kipaumbele kwa maisha ya watu,"amesema Ridhiwani. 

Katika kinachoonekana kuunga mkono hatua zinazofanyika kutokana na kadhia iliyotokea kwa madarasa ya shule, Mbunge huyo wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani alitoa kiasi cha shilingi milioni 5 ili kusaidia kurekebisha sehemu zilizopata athari ya mvua ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze mkoa wa Pwani Ridhiwani Kikwete akizungumza katika moja ya nyumba iliyoathirika na mvua katika kijiji cha Makombe mkoani Pwani alipokwenda kutoa pole na kujionea athari za mvua.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze Ramadhani Possi alimueleza Naibu Waziri Ridhiwani kuwa, mvua iliyonesha mbali na kuezua mapaa ya takriban nyumba 36 lakini mvua hiyo pia ilileta athari kwa shule mbili za msingi za Makombe na Bwilingu A.

Hata hivyo, alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo, ofisi yake ilianza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya tathmini ya uharibifu uliotolea shule ya msingi Makombe na kuahidi ndani ya wiki moja madarasa kuanza kutumika.

“Kule katika kijiji cja Makombe tatizo ni kubwa zaidi ambapo hatua tumeanza kuchukua kama halmashauri na leo mbunge ametuongezea nguvu, katika gharama ya milioni 26 anatuongezea milioni 5 na hela ikiingia itasaidia zaidi,”amesema Possi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze mkoa wa Pwani Ridhiwani Kikwete akielekea katika moja ya nyumba iliyoathirika na mvua katika kijiji cha Makombe, Chalinze mkoani Pwani alipokwenda kutoa pole na kujionea athari za mvua

Kwa upande wake Diwani wa Bwilingu Nasser Karama alieleza kuwa, mvua iliyonesha imeleta athari kwa baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Bwilingu pamoja na shule ya msingi Bwilingu ‘A’ ambapo baadhi ya wananchi wamepata hifadhi na kusaidiwa vyakula na wadau mbalimbali.

Hata hivyo, alikishukuru Chama cha Mapinduzi pamoja na Mbunge wa jimbo la Chalinze kwa kuchukua hatua za haraka mara baada ya kupata taarifa ya kutokea kwa maafa hayo ambapo alisema hatua hiyo imewafariji sana.

“Mie katika kata yangu nimeathirika hili darasa moja na nyumba ya mwalimu pamoja na madarasa yaliyochakaa ila tumepata tumaini baada ya kutembelewa na mbunge na mkurugenzi wa halmashauri ya Chalinze,”amesema Karama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news