Madiwani Namtumbo wapitisha Mpango wa Bajeti ya TARURA

NA YEREMIAS NGERANGERA 

AKIWASILISHA mpango na bajeti kwa waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Namtumbo,Mhandisi Fabian Lugalaba alisema kuwa jukumu kubwa la TARURA ni kufanya thathmini ya mtandao wa barabara na kusimamia matengenezo ya barabara hizo.Mhandisi Lugalaba alidai mapendekezo ya mpango na bajeti ya 2022/2023 umezingatia ukamilishaji wa miradi viporo,kuboresha barabara zilizopo kwenye hali nzuri,kufungua maeneo ya kilimo na shughuli za kijamii pamoja na kuzingatia ukomo wa bajeti.

Aidha, Mhandisi Lugalaba alisema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 TARURA Wilaya ya Namtumbo imepanga kupokea na kutumia shilingi 6,384,000,000 ambapo shilingi 1,184,000,000 zimeombwa kwa ajili ya matengenezo kutoka serikali kuu, shilingi 1,000,000,000 zimeombwa kutoka kwenye tozo ,huku 500,000,000 zimeombwa kutoka kwenye mfuko wa majimbo na shilingi 3,700,000,000 kutoka kwenye mfuko wa barabara.

Diwani wa Kata ya Mkongo, Daniel Nyambo pamoja na kuipongeza bajeti hiyo alisema vipaumbele vya matengenezo ya barabara zimewasilishwa na waheshimiwa madiwani,hivyo aliomba waheshimiwa madiwani wakati wa kutengeneza barabara wajulishwe kazi zinazotakiwa kufanyika na mkandarasi wakati wa kutengeneza barabara hizo ili nao waweze kuzifuatilia na kuacha ujanja ujanza na kulipua kazi.

Naye Diwani wa Kata ya Likuyu, Kassimu Gunda naye kwa upande wake alidai kufungua barabara za mashambani kwa kuwa wilaya ya Namtumbo ni ya wakulima hivyo ni vyema barabara za mashambani zikafunguliwa ili kuwarahisishia wakulima kusafirisha mazao yao.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Jumma Pandu aliwataka TARURA kuhakikisha ukamilishaji wa madaraja badala ya kuweka kiporo kwa kuwa daraja halihitajiki kuwekwa kiporo kutokana na umuhimu wake.

Baraza la madiwani limepitisha mapendekezo ya mpango na bajeti shilingi 6,384,000,000 ya TARURA Wilaya ya Namtumbo baada ya kujiridhisha na kutoa mapendekezo yao yatakayofanyiwa kazi na uongozi wa TARURA.

Post a Comment

0 Comments