Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) yateketeza kilo 250.7 za dawa za kulevya

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali leo Februari 22, 2022 imeteketeza jumla ya Kilo 250.7 za dawa za kulevya zikijumuisha kilo 51.7 za heroine na kilo 199 zenye mchanganyiko wa heroine na cocaine katika kiwanda cha saruji cha Dangote mkoani Mtwara.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 22,2022 na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya,Bw.Daniel Kasokola.

"Uteketezaji huo ni kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mahakama iliyotolewa katika kesi Namba 2 ya Mwaka 2018 kwenye kikao cha Mahakama Kuu kilichoketi mwishoni mwa mwezi Oktoba na kumalizika tarehe 5 Novemba 2021 mkoani Lindi mbele ya Jaji Latifa Mansour. 

"Kesi hiyo iliwahusisha washtakiwa Sano Sidiki na Tukure Ally ambao wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani kila mmoja.
"Amri nyingine ya uteketezaji ilitolewa na Mheshimiwa Jaji Isaya Arufan tarehe 29 Novemba, 2021 kwenye kesi Namba 25 ya mwaka 2019 iliyowahusisha washtakiwa Mohamed Nyamvi na Ahmad Said Mohamed. Katika kesi hiyo washtakiwa hao walihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 kila mmoja,"amefafanua.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, zoezi hilo limefanyika kwa mujibu wa Kanuni Namba 14 ya Kanuni za Kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya za mwaka 2016 za Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015.
Kanuni hiyo inaelekeza kuteketeza dawa za kulevya baada ya shauri kumalizika Mahakamani na kwa dawa za kulevya zenye tabia ya kubadilika au kuharibika endapo zitakaa kwa muda mrefu uteketezaji wake unaweza kufanyika kabla au wakati shauri husika linaendelea kusikilizwa Mahakamani.

"Ndugu wanahabari uteketezaji huu ni wa pili kufanyika hapa kiwandani. Itakumbukwa kuwa, tarehe 15 mwezi Juni mwaka 2021, ulifanyika uteketezaji mwingine uliojumuisha jumla ya kilo 355 za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine. Zoezi la uteketezaji limekuwa likifanyika katika viwanda vya Saruji kwa lengo la kuepuka dawa hizo kuharibu mazingira na kuathiri afya za watu.

"Uteketezaji huu umefanyika kwa uwazi mbele ya wadau wote muhimu wanaotambulika kisheria na kushuhudiwa na waandishi wa habari ili kuondoa dhana iliyojengeka kwa baadhi ya wananchi kwamba, baada ya dawa za kulevya kukamatwa kurejeshwa mtaani na kuuzwa tena.
"Mamlaka inatoa shukrani kwa wadau wote walioshiriki katika kufanikisha zoezi hili muhimu la uteketezaji. Kipekee inamshukuru mwekezaji wa kiwanda cha saruji cha Dangote kwa kuendelea kutupatia ushirikiano kwa kuruhusu zoezi hili kufanyika kiwandani hapa,"imefafanua taarifa hiyo.

Wakati huo huo, DCEA imewasihi wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vinavyojihusisha na mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya kwa kutoa taarifa juu ya watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya. 

Mamlaka hiyo imesema kuwa, kupitia ushirikiano huo wanaamini kuwa, "tutaishinda vita hii na hatimaye kuifikia Tanzania yenye kizazi kisichotumia wala kushiriki kwenye biashara ya dawa za kulevya,"imeeleza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news