Serikali yadhamiria kuimarisha zao la mkonge

NA HADIJA BAGASHA

SERIKALI imesema itahakikisha inaendelea kuimarisha zao la mkonge kwa kuhakikisha uzalishaji wa mkonge unaongezeka na kufikia laki moja na ishirini mwaka 2025.
Pia Serikali imejipanga kuhakikisha inatatua changamoto zinazowakabili wakulima wa mkonge kwa kuhakikisha mkulima analima kilimo chenye tija ili nchi iweze kufikia malengo iliyojiwekea ikiwa ni pamoja na kutengeneza ajira sambamba na kupunguza umasikini. 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Anthony Mavunde wakati alipokuwa kwenye ziara yake mkoani Tanga ya kukagua jengo la Bodi ya Mkonge linaloendelea na ukarabati pamoja na kutembelea wakulima wa mkonge wilayani Korogwe. 

Naibu Waziri Mavunde amesema kuwa, wao kama wizara wanayo mipango ya, kuwasaidia wakulima wao lengo likiwa ni kuhakikisha zao hilo linaleta tija katika nchi yetu pamoja na kuingiza fedha za kigeni. 

"Tunatamani kuona zao hili la mkonge linabadilisha maisha ya watu wetu liwatoe kwenye hali waliyonayo hivi sasa na kubadilisha maisha zaidi changamoto zimekuwa nyingi, lakini mimi na Waziri tumejipanga kuhakikisha tunazitatua na, hatimaye wakulima wafurahie zao lao,"amesisitiza Naibu waziri Mavunde.

Mavunde amesema, kama ilivyo ilani ya uchaguzi ilivyoelekeza kuongezeka kwa uzalishaji wa mkonge kutoka ulipo hivi sasa na kufikia tani 120,000.
"Lazima sisi tulipewa dhamana hii tuhakikishe kuwa tunatekeleza kwa vitendo na moja kati ya eneo kubwa na, muhimu ni kuhakikisha mnatimiza malengo yenu pamoja na kuhakikisha tuna mazingira mazuri ya kuweza kuwahudumia wakulima wetu lakini pia kama wizara tutaendelea kuweka msukumo ili kuhakikisha mnatimiza malengo yenu,"amesema Mavunde. 

Awali akizungumzia ukarabati wa ujenzi wa jengo la ofisi ya bodi hiyo jijini Tanga, Naibu Waziri Mavunde amempongeza Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Saad Kambona kwa hatua ya kuweza kusimamia ujenzi huo huku akiamini ofisi hiyo itawahudumia vyema wakulima wa mkonge mkoani Tanga na maeneo mengine yanayolima zao la mkonge nchi nzima. 

Kufuatia ujenzi huo Naibu waziri Mavunde amesisitiza jengo hilo likamilike ndani ya miezi mitatu kama bodi hiyo ilivyokusudia waanze kutoa huduma kwa jili ya wakulima. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge, Saad Kambona ameishukuru serikali kwa hatua ya kurejesha jengo hilo ambalo linakwenda kuwahudumia wakulima wa zao la mkonge nchini. 

Kambona amesema kuwa, jengo hilo ni moja ya mali ya mkonge zilizokuwa zimeuzwa kinyume na utaratibu kwa watu binafsi ma kutumika kama hospitali hivyo baada ya serikali kujiridhisha kuwa taratibu za uuzwaji hazikufuata miongozo ya serikali ndipo serikali ilipolirejesha serikalini. 

"Ninamshukuru Rais Samia kwa kuonyesha nia ya dhati ya kuwakomboa wakulima wa mkonge nchini kwa kuwaboreshea mazingira yao ipasavyo na sisi tutaendelea kuhakikisha zao hili linaleta tija kwa nchi na Taifa kwa ujumla,"amebainisha Kambona. 

Post a Comment

0 Comments