Hii ndiyo tofauti ya Sensa ya 2022 na zilizopita

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufanya Sensa ya Watu na Makazi ifikapo mwezi Agosti 2022.

Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), ipo kwenye maandalizi ya kufanya sensa hiyo.

Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012.

Hivyo Sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni sensa ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.

Umuhimu wa kipekee wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni pamoja na:-

Kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa;

Taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali;

Taarifa za msingi za hali ya kidemografia, kijamii na kiuchumi za idadi ya watu na makazi za mipango katika ngazi zote;

Kigawio katika kukokotoa viashiria vingine mfano Pato la mtu mmoja mmoja, Pato la Taifa, Ajira na ukosefu wa Ajira na kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi;

Taarifa itakayowezesha serikali kujua ongezeko la idadi ya watu, kwa mgawanyo na viashiria vingine, ambavyo ni muhimu kwa usimamizi wa mazingira; na

Msingi wa utawala bora na ujumuishaji wa demokrasia. Takwimu sahihi za Sensa zinahitajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi, kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa.
Sensa ya 2022 inatarajiwa kuwa na vitu vipya

1:Kutenga maeneo ya kijiografia ya kuhesabia watu katika ngazi za kitongoji/mtaa na upatikanaji wa taarifa za kitakwimu katika ngazi za kitongoji/mtaa pamoja na kuwa na mipaka ya kudumu katika ngazi hizo;

2:Matumizi ya Vishikwambi (tablets) katika hatua zote za utekelezaji wa sensa kwa lengo la kupunguza gharama;

3:Nyongeza ya maswali yatakayowezesha upatikanaji wa taarifa zaidi za kitakwimu ikilinganishwa na Sensa ya Mwaka 2012:-

Taarifa za kidemografia (umri wakati wa ndoa ya kwanza);

Maswali yanayohusu ulemavu (Kichwa kikubwa, Mgongo wazi, Kifafa/Epilepsy, Mbalanga/storiasis na Usonji/autism);

Maswali ya uhamaji kulingana na mapendekezo ya IOM (International Organization of Migration);

Maswali kuhusu umiliki wa nyaraka za kitaifa (vitambulisho NIDA, vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo wadogo, Mzanzibari mkazi, hati ya kusafiria, na leseni ya udereva);

Maboresho ya maswali ya shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja na idadi ya kaya ziliko kwenye sekta isiyo rasmi;

Umiliki wa ardhi na taarifa za TEHAMA
Takwimu za nyumba (orodha, hali ya umiliki na aina ya nyumba)
• Maswali ya kilimo na mifugo

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news