Mheshimiwa Pinda awaongoza Watanzania kumbukizi ya Miaka 100 ya Mwalimu Nyerere, atoa wito

NA FRESHA KINASA

WAZIRI Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda amewaongoza Watanzania katika maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo amewataka Watanzania kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia misingi aliyoiacha.
Mheshimiwa Pinda ameyasema hayo leo Aprili 13, 2022 katika kilele cha maadhimisho hayo yaliyofanyika Katika Uwanja wa Mwenge uliopo Butiama mkoani Mara na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, chama,taasisi za umma na binafsi pamoja na wananchi.

Amesisitiza, Watanzania kuishi katika misingi ambayo Mwalimu aliicha ikiwemo amani, umoja, upendo, mshikamano na uadilifu. Huku akiwataka viongozi wote kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa kufanya kazi kwa uadilifu na weledi sambamba na kuweka mbele uzalendo.
"Tunapokuwa tunatazama kurithisha na kurishishwa lazima twende na awamu zote. Kila awamu imefanya kwa nafasi yake vizuri. Tumuenzi Mwalimu kwa yote mema ambayo aliyaishi na kutuachia Watanzania,"amesema Mheshimiwa Pinda.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Pinda amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kuchukua tahadhari ikiwemo kunawa mikono akasisitiza pia Watanzania kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya watu na makazi mwezi Agosti, mwaka huu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema, wizara hiyo inajivunia tamko la Arusha alilolitoa Mwalimu Nyerere mwaka 1961 ambalo lilipelekea kuanzishwa kwa Hifadhi za Taifa.

Amesema, wizara hiyo imeandaa mpango mkakati wa miaka 10 wa urithishaji mambo ya Mwalimu Nyerere ambapo utekelezaji wake utahusisha kukusanya, kuhifadhi na kutangaza, kujenga miundombinu bora, kuandaa mfumo shirikishi, kuelimisha Jamii kuhisiana na Mwalimu katika kuhakikisha Mwalimu anaenziwa kikamilifu na kutangaza taifa la Tanzania kitaifa na Kimataifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation, Joseph Butiku amesema Mwalimu Nyerere aliunda taasisi hiyo kama chombo cha raia kwa malengo matatu ikiwemo amani, umoja na maendeleo ya watu wote.

"Tulipomuuliza Mwalimu kwa nini taasisi hiyo ije hapa Butiama?.Alisema sababu watu wote wanaotaka mawazo yangu nendeni nilikotoka Butiama mtayakuta mawazo hayo, alisema Mwalimu hivyo,"amesema Joseph Butiku.
Butiku ameongeza kuwa, Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi mpatanishi na pia Mwalimu hakuwa mchoyo kwani alikula chakula na watu wenye ukoma na pia alipenda watu wote na kukubali watu wote ni sawa na alimpenda Mungu wake kwa kumuabudu hata akiwa amekwenda nje ya nchi.

Ameongeza kuwa, Mwalimu pia alijenga uhusiano na nchi za nje na kuweka nguvu zake katika uongozi bora ndio maana aliondoka madarakani hakuwa na mali, bali alishughulikia maendeleo ya wananachi wote, kudumisha umoja na amani.

Butiku pia amekitaka Chama Cha Mapinduzi kuzingatia misingi bora ya Mwalimu Nyerere kwa kuzingatia uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa katika chaguzi ndani ya chama hicho ili kupata viongozi bora.

Chief Japhet Wanzagi kutoka ukoo wa Burito ambaye ni msemaji wa familia ya Hayati Mwalimu Nyerere amesema, serikali inatambua na kuthamini mchango wa Mwalimu Nyerere kutokana na kuleta maadhimisho ya miaka 100 ya kuzaliwa Mwalimu Nyerere Wilaya ya Butiama na kujenga Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere ambacho amesema kitatoa fursa kwa maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa Butiama, Mara na Taifa pia.

"Mwalimu alifanya kazi ya kilimo kwa dhati kabisa sio kwa kuigiza, na alikuwa mkulima hodari, baadhi yetu tulimhurumia sana na kushangaa...kila wakati na mara kwa mara tulimsindikiza shambani, Mwalimu alikuwa kama kalenda kwa watu walipokuwa wakimuona akiandaa mashamba yake, na wao pia waliandaa mashamba yao, alilima na kuvuna mazao ya mtama, mahindi, karanga na ulezi.

"Niiombe serikali iharakishe ujenzi wa chuo hiki cha Kilimo cha Butiama nirudie kuomba chuo hiki kisibaki historia bali kianze kuchukua wanafunzi, najua kimeshapitishwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Hili si ombi langu ni ombi letu sote akiwemo Mama wa Taifa, Mama Maria Nyerere,"amesema.
Pia, Chief Wanzagi ameiomba serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kuweka sanamu ya Mwalimu Nyerere eneo la Musoma kwa ajili ya kumuenzi Mwalimu Nyerere kama ilivyo sanamu hiyo katika Mkoa wa Dodoma. Ambapo pia amepongeza Serikali kwani inaendelea kumuenzi kikamilifu Hayati Mwalimu Nyerere.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Samwely Kiboye amesema, Mwalimu Nyerere alipenda ukweli na alikuwa kiongozi muadilifu na amesema Mkoa wa Mara utahakikisha unapitisha majina ya wagombea waadilifu na wanaoheshimu chama na chama hakitaangalia umaarufu au jina la mtu.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Ally Hapi akitoa salamu za Mkoa wa Mara amesema, Serikali imeleta fedha nyingi za maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara kila jimbo, ujenzi wa madarasa 708 yamekamilika, ujenzi wa vituo 10 vya afya, ujenzi wa Hospitali za Wilaya, miradi ya maji ukiwemo mradi wa Mgango - Kiabakari unaogharimu zaidi ya Shilingi Bil.70.
Miradi mingine ni ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kwangwa Manispaa ya Musoma ambayo imeanza utoaji wa huduma za usafishaji wa figo.

Huku akiwaomba vijana kuwa wazalendo na waadilifu katika kulitumikia taifa kama alivyokuwa Hayati Mwalimu Nyerere.

Maadhimisho ya maiaka 100 ya Mwalimu Nyerere yalikuwa na kauli mbiu isemayo ' Tumuenzi kwa kudumisha umoja, amani, uhuru na kazi'.


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news