CCM yatikisa Musoma Mjini, Kiboye, Mathayo waeleza siri za ushindi Oktoba 28

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini kimefanya uzinduzi wa kampeni za kuomba kura kwa wananchi na kunadi sera zake kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Chama hicho kimewaomba wananchi wa Musoma Mjini wakichague ili kiweze kuendelea kuwaletea maendeleo kuanzia ngazi za chini hadi Taifa, anaripoti AMOS LUFUNGULO kutoka MARA.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo zilizofanyika katika uwanja wa Nyakato Mjini Musoma Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye (Namba Tatu) amesema, Serikali ya Rais Dkt.John Magufuli imefanya kazi kubwa za maendeleo ikiwemo miundombinu.

Amesema, pia imeweza kukuza uchumi wa nchi pamoja na kubooresha huduma za afya na sekta ya elimu, hivyo wananchi wamchague, Mgombea Urais Dkt Magufuli, mgombea Ubunge wa CCM, Vedastus Mathayo na madiwani ili wakaharakishe maendeleo.

Pia Kiboye,amewataka wananchi waliojiandikisha kutunza kadi zao ili siku ya uchaguzi wazitumie kuchagua viongozi bora, huku akisisitiza wagombea wa vyama vingine kutotumia lugha chafu na zisizo na staha kwani kwa kufanya hivyo ni kuvuruga amani ya nchi na utulivu ulioasisiwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

"Kinamama mjitokeze kupiga kura kukitetea Chama Cha Mapinduzi kifanye vizuri katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Vijana na watu wote tuichague CCM ili ishinde iendeleze harakati za kuipaisha nchi kiuchumi kwa miaka mingine mitano inayokuja,"amesema huku akiwahimiza wanachama wa CCM na wananchi wote kuzidi kuuombea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ufanyike kwa amani.

Kwa upande wake mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Mjini Vedastus Mathayo amesema, katika kipindi chake cha miaka mitano ya Ubunge wake ameweza kushirikiana na Serikali kutekeleza shughuli za maendeleo ikiwemo kujenga Sekondari ya Kiara, Nyabisare Sekondari, Baruti Sekondari, Makoko Sekondari, Nyabisare Sekondari, pamoja na kujenga zahanati katika Manispaa ya Musoma ikiwemo Makoko, Buhare, Nyakato, ambazo zimeimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye (Namba Tatu) akimnadi Mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Mjini, Vedastus Mathayo mwenye kofia nyeupe, huku Wanaccm wakishuhudia mkutano huo ambao umezinduliwa Uwanja wa Shule ya Msingi Nyakato Musoma Mjini. (Picha na Amos Lufungulo).

Ameongeza kuwa, upande wa huduma ya maji safi na salama ameweza kuhakikisha yanapatikana kwa kiwango kizuri katika kata zote za Manispaa ya Musoma.

Sambamba na kuhakikisha kwamba kila mwananchi anapata huduma ya kuunganishiwa kwa mkopo huduma hiyo, huku vyumba vya madarasa zaidi ya 200 akifanikisha kuvijenga pamoja na kutengeneza madawati zaidi 3000 kuwaondolea adha wanafunzi kukaa chini.

"Mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na kumuomba Rais atoe fedha na kweli akatoa kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambayo itakuwa mwarobaini wa huduma za matibabu ya kawaida na kibingwa.

"Hospitali ambayo tayari imeanza kazi kuhudumia mama na mtoto na tayari itaanza kutoa huduma ya kusafisha figo (Dialysis) ili wananchi wa Musoma mhudumiwe hapa hapa haya ni mafanikio mazuri ambayo yamepatikana naomba wananchi mnichague tena nikaendelee kuwatumikia,"amesema Mathayo.

Ameahidi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo atahakikisha wananchi wa Kata ya Kwangwa atahakikisha wanapata zahanati, pamoja na kujenga shule za kidato cha tano na sita walau tatu katika Manispaa ya Musoma.

Pia ameahidi kutatua tatizo la ajira kwa vijana kwa kuwa na wawekezaji bora watakaofufua viwanda vilivyopo Musoma ambavyo kwa sasa havifanyi kazi, kikiwemo kilichokuwa kiwanda cha nguo cha Musoma cha MUTEX, viwanda vingine vya samaki huku akiahidi kutoa bodaboda 15 kwa vijana wa Musoma Mjini na kushughulikia changamoto za wavuvi na kinamama wajasiriamali.

Samson Juma na Shabani Matiko ni Vijana wakazi wa Musoma wakizungumza kwa nyakati tofauti na Diramakini baada ya mkutano huo kumalizika wamesema watafurahi endapo Mbunge huyo akichaguliwa atashughulikia kufufua kilichokuwa kiwanda cha nguo cha Musoma cha MUTEX kwani kitasaidia kutatua tatizo la ajira kwa vijana na hivyo kuwaingiza kipato.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news