Mgombea Urais Rais Dkt.John Magufuli aisimamisha Nyanda za Juu Kusini ajikita kwenye sera, kuinadi ilani

Leo Septemba 29, 2020, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt.John Pombe Magufuli akiwa mkoani Njombe amevitaka vyombo vya vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa haraka kuhusu kifo cha Mwenyekiti wa Seneti ya Vyuo Vyuo na Vyuo Vikuu mkoani Njombe,Bw.Imanueli Mlelwa, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Pia ametumia nafasi hiyo kuwaomba wanachama wa chama hicho kuendelea kuwa watulivu na kufanya kampeni bila kubughudiana na mtu au kundi lolote hatua ambayo itawawezesha kunadi sera na ilani ya Uchaguzi kwa ufanisi.

Dkt.Magufuli ameyasema hayo mjini Makambako wakati akihutubia maelfu ya wananchi katika Uwanja wa Polisi ambapo amesema kuwa, hakuna Mtanzania anayetaka kusikia bla! bla! wote wanataka kusikia mipango na mikakati ya chama kupitia mgombea wao iwapo watampa ridha atawafanyia nini.

Dkt.Magufuli amesema, mbali na mambo mengi ambayo anatarajia kuwatekelezea wananchi hao wakimpa ridhaa Oktoba 28, mwaka huu miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuimarisha mazingira ya wakulima wa chai ili waweze kunufaika zaidi.

Amesema, mwaka 2015 hadi 2020 kuna mambo mengi CCM kimeweza kutekeleza katika mkoa huo, ikiwemo kutekeleza miradi ya barabara yenye thamani ya shilingi bilioni 498.76 na wanatarajia kufanya zaidi ya hapo.

Pia amesema,mradi huo kwa kiasi kikubwa umesaidia kurahisisha usafiri katika maeneo mbalimbali hususani kipindi cha msimu wa mvua, ambapo ilichukua takribani siku mbili kusafiri kutoka Ludewa hadi Makete kwenda Njombe ambapo kwa sasa wana uwezo wa kusafiri kwa saa nne au chini ya hapo.

Amesema kuwa, miaka mitano iliyopita wametumia shilingi bilioni 41.1 kuimarisha huduma za afya ikiwemo kujenga hospitali ya rufaa ya mkoa, hospitali tatu za wilaya Wanging’ombe,Ludewa na Njombe.


Sambamba na kukarabati hospitali mbili za wilaya Makete na Njombe, kujenga na kukarabati vituo vya afya 18 na zahanati 84 mkoani humo, hatua ambayo imewezesha wananchi kunufaika kwa huduma za afya karibu na kupunguza vifo vya kinamama na watoto.

Amesema, pia walipeleka shilingi Bilioni 44.108 kwa ajili ya kuboresha na kupanua sekta ya elimu kwa mkoa huo ambapo shilingi bilioni 21.939 zimetumika kwa ajili ya kugharamia elimu bila malipo, shilingi bilioni 22.169 zimetumika kutekeleza miradi ya ujenzi na ukarabati ya miundombinu ya elimu.

Dkt.Magufuli akizungumzia kwa upande wa umeme amesema, tayari wamefikisha umeme katika vijiji 290 kati ya vijiji 381 sawa na asilimia 76.

Amesema, hivyo vilivyobaki 91 wakiopewa ridhaa wanakwenda kuvikamilisha ili kila kaya iweze kupata nishati hiyo ambayo ni muhimu kwa shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuangaza.

Wakati huo huo, Dkt.Magufuli amesema, wamepanga kupeleka maji katika miji 28 kwa kupitia miradi mikubwa mitatu katika mkoa huo yenye thamani ya shilingi Bilioni 121 ambapo kwa Makambako shilingi Bilioni 42, Wanging’ombe shilingi Bilioni 50 na Njombe shilingi Bilioni 29 kwa ajili ya kufanikisha upatikanaji wa maji safi na salama.

“Tunatoa huduma za Afya kwa Wazee Bure, Watoto chini ya miaka mitano wanatibiwa bure, tunataka miaka inayokuja Bima ya Afya iwe kwa Watanzania wote, tuna mipango mikubwa kwa Taifa hili, tumetoka mbali tumefika mbali na tutaelekea mbali”.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news