Majaliwa alivyotumia ilani kuwapunguza kasi wapinzani akimnadi Dkt.Magufuli, madiwani, wabunge

“Chagueni CCM, chama chenye mipango ya maendeleo na ya kueleweka. Chama chenye mipango ndani ya kitabu chenye kurasa 303. Naomba kura zenu ili tuwaletee maendeleo. Zamani tulikuwa na kitabu kidogo cha kurasa 236 lakini sasa hivi tuna buku kubwa zaidi. Tukitekeleza yote haya, mambo si yatakuwa mazuri zaidi,?” alihoji Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa...Mwandishi Diramakini anakujuza, endelea...

SERIKALI YA CCM YAAHIDI KITUO CHA AFYA IRUGWA Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akitembea katika mitaa ya kijiji cha Kamasi, Kata ya Ilangala, Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, kwenye mkutano wa kampeni za CCM, katika kata hiyo, Septemba 25, 2020. (PMO).
Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwasilimia wananchi,baada ya kuwasili kwenye kijiji cha Kamasi, Kata ya Ilangala, Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, kwenye mkutano wa kampeni za CCM, katika kata hiyo, Septemba 25, 2020. (PMO).

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kujenga kituo cha afya kata ya Irugwa wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza ili kuwaondolea wananchi wa kisiwa hicho adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya.

Hayo yamesemwa leo Septemba 25, 2020 na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Mheshimiwa Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wakazi wa kisiwa hicho kwenye mkutano wa kampeni.

Uamuzi huo unaenda sambamba na ahadi ya Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025 kwenye uk. 186 inayosema: “Hadi kufikia 2025 Serikali itaongeza vituo vya kutolea huduma za afya kwa asilimia 20 ya vituo 8,446 vilivyopo sasa; vipaumbele vitawekwa katika ujenzi wa vituo vya afya na ukamilishwaji wa maboma kwa kuzingatia uwiano wa kijiografia, idadi ya watu na wingi wa magonjwa.”

Hata hivyo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ilishatoa shilingi milioni 49.2 kwa ajili ya ujenzi wa jengo moja la kujifungulia katika zahanati ya Irugwa.

Kuhusu maji Mheshimiwa Majaliwa amesema Ilani ya CCM imeweka mipango imara ya kushughulikia upatikanaji wa maji vijijini, kama hatua ya kutekeleza azma ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mama ndoo kichwani.

Akizungumzia usafiri wa majini kwa wakazi wa eneo hilo, Mheshimiwa Majaliwa amesema, Serikali ya CCM ikiingia madarakani inakusudia kujenga vivuko mbalimbali kikiwemo kivuko cha Irugwa, Murtanga, Gana, Kakakuru na Lugezi hadi Kisorya.

Kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM (uk.83-84), Chama cha Mapinduzi kimeielekeza Serikali ikamilishe ujenzi wa vivuko vipya nane kikiwemo cha Irugwa - Murutanga (Ukerewe).

Pia Ilani hiyo imeelekeza Serikali ianze kutekeleza mradi wa ujenzi wa maegesho ya Rugezi – Kisorya (Mwanza), Kome na Nyakalilo (Mwanza), Utete (Pwani), Chato - Nkome (Geita), Iramba na Majita (Mwanza), Irugwa (Ukerewe – Mwanza).

Kwa upande wake mgombea ubunge wa jimbo la Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi amesema kivuko cha Irugwa kitakua mkombozi kwa wananchi wa eneo hilo ambao watoto wao hawajawahi kuona gari ikipita katika kisiwa hicho kutokana na ukosefu wa kivuko.

ASEMA CHAGUENI CCM, CHAMA CHENYE MIPANGO

Wakati huo huo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wananchi waichague CCM ili iweze kuwaletea maendeleo.

“Chagueni CCM, chama chenye mipango ya maendeleo na ya kueleweka. Chama chenye mipango ndani ya kitabu chenye kurasa 303. Naomba kura zenu ili tuwaletee maendeleo.”

Alitoa wito huo jana jioni Septemba 24, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Sumve wilayani Kwimba mkoani Mwanza kwenye mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Misheni.

“Zamani tulikuwa na kitabu kidogo cha kurasa 236 lakini sasa hivi tuna buku kubwa zaidi. Tukitekeleza yote haya, mambo si yatakuwa mazuri zaidi,?” alihoji.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Mwanza kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kumwombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Sumve, Bw. Kasalali Mageni, mgombea udiwani wa kata ya Sumve, Bw. Gervas Kitwala na madiwani wa kata zote za wilaya ya Kwimba.

“Ninaomba kura kwa wapenzi wa vyama vyote, pigeni kura nyingi sana kwa Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge Bw. Kasalali na madiwani wote ili mpate wawakilishi wengi zaidi kupitia viti maalum,”alisema.

Akielezea mafanikio kwenye sekta ya maji wilayani humo, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 2 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji Igumangobo, ujenzi wa mradi wa maji Igunguhya na Nyanhiga, upanuzi wa mradi wa maji Kadashi-Nyashana, upanuzi wa mradi wa maji Hungumalwa na upanuzi wa mradi wa maji KASHWASA kwenda kijiji cha Jojiro.

Alisema fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi mingine ya maji ni sh. milioni 118.6 kwa ajili ya miradi ya maji ya uchimbaji wa visima vya Nkalalo na Lyoma na mradi wa uchimbaji wa kisima katika mji wa Sumve.

Kuhusu barabara, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali iliunda TARURA ifuatilie na kukagua maeneo korofi na watoe makaridio ya matengenezo ili zitafutwe fedha za ujenzi.

“Malengo ya Serikali ya kuboresha njia za usafirishaji ni pamoja na kuimarisha barabara zote zinazounganisha kijiji na kijiji, kata na kata, wilaya na wilaya ikiwa ni pamoja na madaraja yanayopita kwenye barabara hizo kwa kuyaingiza kwenye mpango ili njia hizo ziweze kupitika,”alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news