Mbunge Mteule kupitia NGOs Neema Lugangira asema atakuwa kiunganishi bora kati ya asasi, Bunge, Serikali, wafadhili na chama

Mbunge Mteule Viti Maalum kundi la Asasi za Kiraia (NGOs) Tanzania Bara kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Neema Lugangira ametembelea Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Wadogo (MVIWATA) ili kujua changamoto zinazowakabili na namna ya kuzitatua.

Akiongea na uongozi wa MVIWATA mkoani Morogoro, Neema Lugangira alisema lengo la kutembelea asasi mbalimbali nchini ikiwemo MVIWATA ni kutaka kupata uelewa, kujua changamoto zilizopo na kumwezesha kupanga vipaumbele vya kuanzia atakapokuwa bungeni.

Mbunge Mteule Viti Maalum Kundi la Asasi za Kiraia (NGOs) Tanzania Bara, Neema Lugangira (kulia) akizungumza jambo na baadhi ya viongozi wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Wadogo Tanzania (MVIWATA) alipotembelea ofisi hiyo mjini Morogoro.

Alisema kuwa, ameshatembelea asasi za mikoa ya Tanga, Kagera ikiwa ni pamoja na kukutana na wakurugenzi wanawake ambao asasi zao zinashughulika na haki za wanawake na usawa wa kijinsia.

Alieleza kuwa, kwa kuongea na wadau hao anapata fursa ya kupata mambo ya kujadili yaliyomo kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yanayohusiana na asasi hizo na kuweza kubadilishana mawazo kwenye utekelezaji pamoja na kuwa kiunganishi bora kati ya asasi, bunge, serikali, wafadhili na chama.

“Natumia kipindi hiki cha kampeni kwa kukutana na wadau wa NGO’S, ili waweze kufahamu bungeni kuna hii nafasi, na kwamba CCM imetambua umuhimu wa asasi hizo katika mchango wake kwa jamii na taifa kwa ujumla na nikaona itenge nafasi hii,”alisema Neema.

Akizungumzia maeneo yaliyoguswa na Ilani ya CCM alisema lengo kubwa ni kuongeza tija katika kilimo ili kusaidia viwanda, kuimarisha miundombinu na uzalishaji, kumsaidia mkulima kuzalisha na kupata masoko, usimamizi wa mazao ya kimkakati, kuzijengea uwezo asasi za ndani na kujua namna asasi hizo zitakavyokuwa na uendelevu hasa kwa asasi za ndani.

Naye Mkurugenzi wa MVIWATA, Stephen Ruvuga, akitoa shukrani zake kwa chama na Serikali alisema, kwa ugeni huo wanapata matumaini ya kuwepo kwa maelewano mazuri kati ya serikali na asasi hizo, kitendo kitakacho chochea maendeleo kwa haraka.

Kwa upande wake Mwanasheria wa MVIWATA, Kuyunga Yango alisema kuwa ni vyema kukawepo na ongezeko la bajeti la asilimia 10 kwenye kilimo, pia ushirikishwaji wa wananchi katika utekelezaji wa mipango bora ya ardhi, pamoja na utoaji wa hati za kimila ili kuhakikisha usalama wa ardhi kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news