Zitto Kabwe ataja mambo 10 watakayoanza nayo, wafanyabiashara, wafanyakazi kuneemeka zaidi

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe amesema, chama hicho kinaamini kuwa sekta binafsi ndio injini ya kuendesha uchumi wetu na kuzalisha ajira, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Amesema kwa sasa, asilimia 91 ya ajira zote rasmi nchini Tanzania zinatokana na Sekta Binafsi. "Wafanyabiashara wanaowekeza mitaji yao wanapaswa kuwekewa mazingira mazuri ya kufanya biashara ili Serikali ipate Mapato ya Kodi na tozo mbalimbali kuendesha nchi ikiwemo kutoa huduma muhimu kama vile maji, afya, elimu na utawala.

"Ili kuwekeza ni lazima watu waweke akiba, lakini uwiano wa akiba kwa pato la Taifa Tanzania ni asilimia 16 na mahitaji ni angalau asilimia 30.

"Hivyo lazima kutumia akiba za watu wa nchi nyingine kuwekezwa nchini ( Foreign Direct Investments) ili kuzalisha ajira nchini, kuongeza mapato ya watu na kuongeza akiba ya ndani.

Zitto amesema, katika kipindi cha 2020-2025 Serikali itakayoundwa na ACT Wazalendo na vyama washirika itachukua hatua zifuatazo ili kukuza, kuendeleza na kulinda sekta binafsi, wafanyabiashara na uwekezaji;

Mosi ni kupitia mifumo yote ya kodi na kuhakisha kunakuwa na kodi rafiki kwa wananchi ili kuhakisha biashara zinakua na kuimarika na siyo kuwa na mfumo wa kodi ambao utapelekea kufunga au kuua biashara.

Pili amesema wataondoa mfumo unaomlazimisha mfanyabiashara kulipa kodi kabla hajaanza kufanya biashara.

Jambo la tatu amesema, Serikali yao itawapa wananchi uhuru na kuondoa urasimu katika kuanzisha na kuendesha biashara yoyote ikiwa ni pamoja na uhuru wa kununua na kuuza bidhaa zozote halali ndani na nje ya nchi bila vikwazo vyovyote.

Nne amesema, Serikali yao itarasmisha udalali wa kiasili kwa kuutambua, kuupa leseni na masharti ya kuwezesha haki katika biashara ya mazao.

Zitto amesema, jambo la tano Serikali yao itawezesha ufufuaji na uendelezaji wa viwanda vya kuchakata pamba na kuzalisha nguo (textile industry) kwa kutunga sera na sheria zitakazowezesha kupambana na biashara haramu ya nguo (smuggling of textile goods ).

"Kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango sifuri kwa vifaa vyote ambavyo ni malighafi kwa viwanda vya nguo, na kutoa mikopo maalumu kwa kipindi maalumu yenye riba maalumu ya kiwango cha mfumuko wa bei kwa mnyororo wa thamani wa pamba mpaka nguo,"amebainisha Zitto.

Amesema, jambo la sita Serikali yao itatoa ruzuku ya kikodi kufidia gharama za uzalishaji kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumiwa na wananchi wengi zaidi kama vile sukari, mafuta ya kula na vitabu au karatasi kwa kulipia asilimia 50 ya gharama za umeme.

Zitto amesema, jambo la saba, Serikali yao itarekebisha sera za kodi ili kuirejesha katika hali yake ya kawaida Sekta ya Utalii pamoja na mnyororo wake ambayo imeathirika sana na janga la COVID 19.

"Marekebisho hayo yatahusisha kutoa ruzuku kwa kampuni za utalii na kulinda ajira za wafanyakazi wa Sekta ya Utalii,"ameeleza Zitto Kabwe.

Jambo la nane, Zitto amesema, Serikali yao itaweka vivutio vya kikodi ili kuwezesha sekta binafsi kujenga miundombinu wezeshi na muhimu kwa mfumo wa ubia.

Amefafanua kuwa, hatua hii itaipa Serikali pumzi ya kujielekeza kwenye kutoa huduma muhimu kwa wananchi, kuepuka kuongeza Deni la Taifa na kukuza sekta binafsi.

Akifafanua jambo la tisa, Zitto amesema kuwa, Serikali itaweka vivutio vya kibajeti na kikodi kwenye miradi yote ya kilimo cha umwagiliaji na viwanda vyote vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.

Zitto amebainisha jambo la kuwa kuwa, Serikali yao itarekebisha muundo mzima wa makato kutoka kwenye mapato ya waajiri na waajiriwa ili kuchochea matumizi kwenye uchumi.

"Ni kwa kupunguza Kodi ya Mapato kwa Wafanyakazi (PAYE ) kima cha chini mpaka asilimia nane kutoka asilimia tisa ya sasa kwa kuanzia mapato ya shilingi 500,000 kwa mwezi na kiwango cha juu mpaka asilimia 25.

"Kurekebisha tozo ya kuongeza ujuzi (Skills Development Levy) kwa kuishusha mpaka asilimia mbili na italipwa na waajiri wote ikiwemo Serikali na taasisi zake zote. Kupunguza makato ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi WCF mpaka asilimia 12 kwa ujumla wake ( mwajiri asilimia saba na mwajiriwa asilimia tano ). Bima ya Afya na Fidia kwa Wafanyakazi itajumuishwa katika Mafao ya Hifadhi ya Jamii.

"Itaimarisha sheria ya kuzuia ukwepaji wa kodi wa makampuni ya Kimataifa ili kuokoa mapato sawa na asilimia tano ya Pato la Taifa ambayo yanapotea kupitia mbinu za kihasibu zinazofanywa na Multinational Corporations. Kuwezesha hili Serikali itaingia mikataba ya kimataifa inayosadia mataifa kuzuia ukwepaji wa kodi,"amefafanua kwa kina Kiongozi Mkuu huyo wa ACT Wazalendo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news