Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Ludovick Nduhiye amefika eneo kinapojejwa kiwanda cha kuchakata maziwa cha Kahama Fresh kinachojengwa eneo maalum la viwanda lililopo Kihanga Wilaya ya Karagwe Mkoa Kagera, anaripoti Eliud Rwechungura (Kagera).
Ujio wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara umekuwa na lengo la kukagua na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na kutatuliwa kwa baadhi ya changomoto ambazo mwekezaji amekuwa akikabiliana nazo katika ujenzi wa kiwanda hicho.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Ludovick Nduhiye (aliyevaa koti) akikagua ramani ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata maziwa cha Kahama Fresh kitakachokuwa na uwezo wa kuchakata lita 10,000 kwa mzunguko mmoja na gharama za ujezi mpaka kukamilika ni shilingi Bilioni 2.4, kinachojengwa eneo maalum la viwanda lililopo Kihanga Wilaya ya Karagwe Mkoa Kagera. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa EPZA, James Maziku na kushoto ni Mkurugenzi wa Kahama Fresh, Jossam Ntangeki. Oktoba 12,2020. (Eliud Rwechungura-WVB).
Hayo yanajiri ikiwa ni wiki moja baada Waziri wa Viwanda na
Biashara,Innocent Bashungwa kutoa maagizo kwa Wizara ya Viwanda na
Biashara kufika kwenye kiwanda cha maziwa kinachojegwa Kihanga wilayani
Karagwe ili kutatua changamoto anazopata Mwekezaji wa kiwanda hicho,
“Nimekuja kufuatilia yale tuliyokubaliana mwezi wa Sita nilipokuja Karagwe, tulikubaliana eneo hili kuwa eneo maalum la uwekezaji kiuchumi (special economic zone) chini ya EPZA lakini eneo hili tutaliunganisha na eneo la Rukombe, Chamchuzi ili kuhakikisha tunawavutia wawekezaji wa ndani na nje maana uwekezaji unaofanywa hapa na ndugu Jossam ni mfano wa kuigwa,’’amesema Nduhiye.
Nduhiye amepongeza jitihada za mwekezaji mzawa wa Kahama Fresh Limited, Bw.Jossam Ntangeki kwa hatua waliyofikia katika ujenzi wa kiwanda cha maziwa na kusaidia utekelezaji wa dira ya Serikali ya Awamu ya Tano katika ujenzi wa uchumi wa viwanda maana kwa mkoa hapakuwa na kiwanda cha maziwa chenye ukubwa wa kuchakata lita 10,000 kwa siku na amepongeza uwepo wa pango wa ujenzi wa kiwanda kinachotengeneza vyakula vya ng’ombe wa maziwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe, Godwin Kitonka ametoa ufafanuzi wa mpango wa kutangaza eneo hilo kuwa eneo maalum la uwekezaji wa viwanda kwa Wilaya ya Karagwe na akatoa takwimu ya zoezi la kugawa ngo’ombe kwa wafugaji wadogo wadogo ambapo mpaka sasa wametolewa ng’ombe 300 ambao itasaidia upatikanaji wa malighafi ya maziwa kwa ajili ya kiwanda hicho.
Nae Mkurugenzi wa Kampuni ya Kahama Fresh Limited, Jossam Ntangeki ameishukuru Serikali kuendelea kutatua changamoto ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo pia ameshukuru wizara kwa kuwawekeaa mazingira mazuri ya uwekezaji kwa kutenga maeneo maalum ya viwanda kwa kila wilaya na kuwasogezea mahitaji muhimu ambayo yanahitajika katika uwekezaji wao.
Jossam wakati akitoa taarifa ya kiwanda kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara amesema kuwa, ujenzi wa kiwanda hicho umefikia kiwango cha kujenga majengo ya ofisi na kusawazisha eneo kitakapojegwa kiwanda na amesema kiwanda kitakamilika ndani ya miezi sita na kitakuwa na uwezo wa kuchakata lita 10,000 kwa mzunguko mmoja na gharama za ujezi mpaka kukamilika ni shilingi billioni 2.4 ambapo kwa sasa kampuni imeajiri wafanyakazi 104 na madaktari wa mifugo watano.
