TAMWA yawashirikisha wanavikundi mbinu za kutumia mitandao ya kijamii kujineemesha

Wanavikundi vya ujasiriamali kisiwani Pemba wametakiwa kutumia fursa ya uwepo wa mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuongeza wigo wa kutangaza na kuuza bidhaa zao kupitia soko mtandao,anaripoti Gaspary Charles (TAMWA) Zanzibar.
Mwezeshaji wa mafunzo akimuelekeza mmoja wa washiriki wa mafunzo namna ya kuweka bidhaa katika soko mtandao. (TAMWA/Diramakini).

Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuvijengea uwezo vikundi hivyo juu ya matumizi ya soko mtandao yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) Zanzibar mwezeshaji wa mafunzo hayo, Faki Othman Faki amesema ili mjasiriamali aweze kukua kiuchumi ni lazima ajue kutumia fursa ya mitandao ya kijamii.

Alisema, uwepo wa mitandao hiyo imerahisisha uwezekano wa mjasiriamali kuuza na kuwafikia wateja wengi zaidi kwa muda mfupi pasipo kutumia nguvu kubwa kama ilivyo kwa njia nyingine za utafutaji wa masoko.

“Ni muhimu sana kuchangamkia fursa ya soko mtandao kwani ndiyo sehemu pekee kwa sasa ambayo inaweza kukutanisha na wateja wengi zaidi na kwa haraka duniani pasipo kutumia nguvu nyingi,” alisema.

Aidha, mwezeshaji huyo alitahadharisha wajasiriamali hao kuachana na dhana ya kuzalisha bidhaa kwa mazoea kwani kufanya hivyo kutapelekea kuwakosesha wateja kutokana na bidhaa hizo kukosa mvuto na ubora wa kushindana na bidhaa nyingine sokoni.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiendelea na mafunzo.(TAMWA/Diramakini.

Pia aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia misingi ya masoko ikiwa ni pamoja na kimarisha mahusiano na mawasiliano chanya kwa wateja ili kujenga uaminifu wa wateja kwa bidhaa zao.

Alisema, “tuache tabia ya kuzalisha bidhaa kwa mazoea na badala yake tujenge misingi ya kuwa na mawasiliano ya karibu na wateja wetu ili kujua mahitaji yao kwani hii itakusaidia kujua wapi panahitaji kuboreshwa ili kuendelea kuaminika zaidi sokoni.”

Mmoja wa washiriki hao, Fadhila Ali Juma ameshukuru kutolewa kwa mafunzo hayo kwani itawasaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa soko kwa bidhaa walizokuwa wanazalisha.

“Kiukweli leo nimefurahi sana kupata mafunzo haya kwani kuanzia leo kikundi chetu tutaanza kutumia fursa hii tuliyooneshwa kwa ajili ya kuuza bidhaa zetu ambazo ni sabuni asilia, mafuta na majani ya chai kwani changamoto kubwa inayotukabili ni upatikanaji wa masoko tunazalisha sana, lakini soko ni kikwazo,”alisema.
Mwezeshaji nwa mafunzo, Faki Othman Faki, akiendelea kutoa mada kwa washiriki.(TAMWA/ Diramakini).

Mapema afisa mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi Zanzibar - (WEZA III) kutoka TAMWA ofisi ya Pemba, Asha Mussa Omar alisema lengo la kutolewa mafunzo hayo ni kuwapatia mbinu za kuongeza wigo wa upatikanaji wa soko la kuuza bidhaa zao wanazozalisha ili lengo la kujikwamua kiuchumi lifanikiwe.

“TAMWA Zanzibar imeamua kutoa mafunzo haya ili yawawezeshe wajasiriamali wetu kutambua na kuchangamkia fursa zilizopo katika soko mtandao kwa lengo la kuendelea kujikwamua kiuchumi,” alisema.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi Zanzibar - (WEZA III) unaotekelezwa na TAMWA Zanzibar kwa ufadhili wa Milele Zanzibar Foundation.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news