Benki ya Equity yaunga mkono uchumi wa Buluu Zanzibar

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Abdallah Hussein Kombo amesema endapo Zanzibar itajikita zaidi kwenye uchumi wa buluu kupitia shughuli za uvuvi visiwani humo utasaidia kukuza ajira na kukuza uchumi wa Zanzibar, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Waziri huyo ametekeleza miongoni mwa maagizo aliyoyatoa Rais wa Zanzibar, Dk.Hussein Ali Mwinyi kuhusu kukutana na wadau wa sekta ya uvuvi wakiwemo Kampuni ya Uvuvi ya Salmini,wavuvi na Benki ya Equity.

Akizungumza katika uzinduzi wa uvuvi na mikopo kwa wavuvi uliondaliwa na benki hiyo ya Equity, Waziri huyo amesema Serikali ya Awamu ya Nane imeamua kujikita kwenye uchumi wa bluu ambapo tayari imeonyesha ishara nzuri mpaka sasa.

“Kampuni ya uvuvi ya Salmini imepata soko la samaki aina ya jodari nchini Finland,Uturuki na China ambapo kila mwezi wanatakiwa samaki tani 5,000 hivyo kampuni hiyo imepanga kununua samaki kwa wavuvi wadogo visiwani Zanzibar,”amesema.

Waziri huyo amesema licha ya kuwepo kwa fursa hiyo pia Benki ya Equity imeonyesha utayari wake wa kutoa mikopo kwa wavuvi kutoa mikopo ya zana za kisasa za uvuvi.

“Mimi ninaomba kampuni za uvuvi ikiwemo Salmini,wavuvi na Benki ya Equity kushirikiana kwa pamoja kupitia kamati za wavuvi zilizopo vijijini ili kutimiza azma ya serikali kupitia uchumi wa buluu,”amesema.

Katika maelezo yake amesema, Serikali ya Zanzibar ya Awamu ya nane imeamua kujikita kwenye uchumi wa buluu kupitia sekta ya uvuvi ili kukuza ajira, kukuza uchumi wa Zanzibar.

“Zanzibar ina wavuvi zaidi ya 50,000 hivyo kuna haja wadau wa sekta ya uvuvi kukutana na kamati za uvuvi ili kuona namna ya kunufaika na uchumi wa buluu ambao unajumlisha pia suala la ufugaji wa samaki na si uvuvi tu pekee yake,”amesema.

Waziri huyo ameema, kuna haja ya kuona wadau hao wanakutana mara kwa mara ili kuharakisha suala la upatikanaji wa fedha katika miradi mbalimbali ya sekta ya uvuvi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity, Robert Kiboti amesema tayari wamejipanga katika kuwawezesha wavuvi wadogo kunufaika kupitia uchumi wa buluu.

Amesema, benki hiyo ipo tayari kuunga mkono kipaumbele cha Serikali ya Zanzibar ya uchumi wa buluu kwa kuwapatia mikopo wavuvi ikiwemo mikopo ya zana za kisasa za uvuvi.

“Benki yetu ipo tayari kuwafikia wavuvi wote katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar ili kuwawezesha wavuvi kufikia malengo yao na kuwa sehemu ya kuleta mabadiliko chanya katika uchumi wa buluu,”amesema.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya uvuvi ya Salmini, Dkt.Salmin Ibrahim Salmin amesema tayari kampuni hiyo imewaunganisha vikundi vidogo vya wavuvi wapatao 3,500 kwa ajili ya kupata fursa ya sekta hiyo.

“Tumeona tuwaunganishe wavuvi hao kutokana na kuwa wavuvi wanahitaji mitego ya kisasa,soko la uhakika,wanahitaji mikopo,zana bora,bandari ya uvuvi,viwanda vya kusindika samaki hivyo tuliona umuhimu wa kuwaunganisha,”amesema.

Amesema, kupitia kampuni hiyo tayari wamefanya mazungumzo na mwekezaji kutoka Uturuki kwa ajili ya kuwekeza bandari ya uvuvi na kiwanda cha kusindika samaki ambacho kitagharimu dola za kimarekani bilioni 3.

Post a Comment

0 Comments