Dkt.Agness Gidna aiweka Tanzania kwenye ramani ya Dunia katika fani ya Palentolojia na Akiolojia

Mtandao wa Kimataifa wa Wanawake Wanasayansi Duniani (TROWELBLAZERS), umemtambua Mhifadhi mwandamizi wa Paleontolojia, Makumbusho ya Taifa nchini, Dkt.Agness Gidna kuwa ndiye mwanamke wa kwanza msomi kwenye ngazi ya Udaktari wa Falsafa katika fani ya Masalia ya Wanyama na Binadamu wa Kale (Paleontolojia), anaripoti Sixmund J Begashe (Makumbusho ya Taifa).

Mtandao huu Mkubwa wa Kimataifa lengo lake kuu ni kutambua, kuwaenzi na kuhamasisha watafiti wanawake chipukizi katika fani ya Akiolojia na Palentolojia Duniani. 

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt.Noel Lwoga, amempongeza Dkt Gidna kwa mchango wake huo mkubwa katika masuala ya utafiti wa Akiolojia na Palentolojia nchini hadi kutambulika kimataifa jambo ambalo limeipa heshima kubwa Taasisi ya Makumbusho ya Taifa na Tanzania kwa ujumla.
Pichani ni Dkt.Agness Gidna akiwa na vielelezo vya kufundishia juu ya masalia ya Wanyama na Binadamu wa Kale.

Akizungumzia kutambulika kwa Dkt. Gidna, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Indiana nchini Marekani katika fani ya Akiolojia na Paleontolojia, Prof.Jackson Njau licha ya kumpongeza Dkt. Gidna amemuelezea kuwa ni mwanamke mkakamavu na mwenye juhudi katika kufanya utafiti wa urithi wa mambo ya kale hivyo, kutambuliwa kwake kimataifa kumeipa heshima kubwa nchi katika ramani ya Dunia.

Naye Dkt.Gidna amepokea kwa furaha kutambuliwa na Mtandao wa Kimataifa wa Wanawake Wanasayansi Duniani katika fani ya Akiolojia na Palentolojia, kwani utambuzi huo umemuongezea ari, na kasi ya kuendelea kufanya utafiti zaidi na kuandaa machapicho ya matokeo ya utafiti huo kwa manufaa ya nchi.


Pichani juu na chini Dkt Agnes Gidna akiwa kwenye utafiti wa tabia za Simba katika Hifadhi ya Tarangire kwa lengo la kuelewa tabia za simba wa kale.

“Nimefurahi sana kwa heshima hii kubwa, kuwa miongoni mwa wanawake wachache sana katika fani ya Akiolojia na Palentolojia Afrika na Duniani, pia kuwa Mwanamke wa kwanza kupata Udaktari wa Falsafa katika fani Palentolojia na pia kujumishwa na Majagina katika fani hii kama Dkt Mary Leakey wa Marekani, Prof Kathy Schick wa Marekani, Dkt Emma Mbua wa Kenya na wengine,”amesema Dkt.Gidna.

Dkt.Gidna ameongeza kuwa, mchango hasa uliotambuliwa na umoja huo wa kimataifa ni pamoja na matokeo ya utafiti alioufanya katika hifadhi ya Taifa ya Tarangire kuhusu tabia za Simba wa leo inayohusishwa na Simba wa kale, matokeo ya utafiti huu umekuwa na mchango mkubwa na umekuwa ni marejeo kwa watafiti wanaofanya utafiti Afrika Mashariki katika kuelewa tabia za Simba wa kale na Babu zetu walioishi miaka milioni mbili iliyopita.

Mchango mwingine ni kuhifadhi kwa kitaalam masalia ya Zamadamu na masalia ya Akiolojia katika Makumbusho ya Taifa nchini ambayo ni urithi wa nchi kupitia ufadhili kutoka Shirika la Kiutafiti na Elimu juu ya Mambo ya Kale (PAST) la nchini Afrika ya Kusini, na ufadhili kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Mtandao huo pia umetambua utaalamu wa Dkt. Gidna katika kuandaa na kuweka Maonyesho kuhusu “Chimbuko la Binadamu Tanzania”, katika Makumbusho ya Taifa na katika Makumbusho ya Bonde la Olduvai, Ngorongoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news