Gesi ya helium kutoka Ziwa Rukwa kuipaisha Tanzania kiuchumi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesema, Tanzania ina jumla ya futi za ujazo bilioni 138 za gesi aina ya Helium ambayo inapatikana katika Ziwa Rukwa, anaripoti Mwandishi Diramakini.

"Aidha, tuna gesi aina mbalimbali, kama vile ethane, helium, ambayo hivi karibuni zimepatikana futi za ujazo bilioni 138 kwenye Ziwa Rukwa, ambazo zinaweza kuhudumia dunia kwa miaka 20; 

Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo leo Novemba 13, 2020 jijini Dodoma wakati akifungua Bunge la 12 na kulihutubia Taifa huku akiahidi kuimarisha sekta ya nishati zaidi.

“Sambamba na hayo, kuhusu nishati, kwenye miaka mitano ijayo, tutaanza utekelezaji wa Miradi ya kielelezo (flagship projects) ya Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga lenye urefu wa kilometa 1,445 pamoja na Mradi wa Kusindika Gesi Asilia (LNG) Mkoani Lindi,” amesema Rais Magufuli.

Pia amewasisitiza Watanzania kuendelea kutumia gesi asilia pamoja na ile ya mitungi kwenye maeneo mbalimbali nchini

“Zaidi ya hapo, tutaendelea kuhamasisha matumizi ya gesi asilia na gesi ya mitungi majumbani, kwenye taasisi, viwanda na magari ili kupunguza uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, akizungumzia kuhusu sekta ya nishati, nchini amesema serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya nishati na pia kuboresha upatikanaji wa huduma za umeme.

“Katika hilo, tunakusudia kukamilisha ujenzi wa Bwawa la kufua Umeme la Nyerere litakalozalisha Megawati 2,115 na kuanza ujenzi wa miradi mingine ya umeme wa maji Ruhudji Megawati 358; Rumakali Megawati 222; Kikonge Megawati 300 na pia umeme wa gesi asilia Mtwara Megawati 300; Somanga Fungu Megawati 330, Kinyerezi III Megawati 600 na Kinyerezi IV Megawati 300; pamoja na miradi mingine midogo midogo.

“Aidha, tunakusudia kuzalisha umeme Megawati 1,100 kwa kutumia nishati jadidifu (jua, upepo, jotoardhi),”amefafanua Rais Dkt. Magufuli.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news