Rais Magufuli aahidi makubwa zaidi Sekta ya Madini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesema, ndani ya miaka mitano iliyopita Sekta ya Madini nchini imepiga hatua kubwa na anatarajia miaka mitano ijayo itasonga mbele zaidi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Ameyasema hayo leo Novemba 13, 2020 wakati akifungua Bunge la 12 na kulihutubia Taifa bungeni Dodoma.

"Kwenye miaka mitano iliyopita tumepata mafanikio makubwa kwenye sekta ya madini. Mapato yameongezeka kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2014/2015 hadi shilingi bilioni 527 mwaka 2019/2020. Mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka 2019. 

Zaidi ya hapo, kwa mara ya kwanza, katika historia ya nchi yetu, mwaka 2019, sekta ya madini iliongoza kwa kutuingizia fedha nyingi za kigeni, Dola za Marekani bilioni 2.7. Nitumie fursa hii kulipongeza Bunge la 11 kwa kutoa mchango mkubwa katika kupatikana kwa mafanikio haya.

"Nina imani kuwa Bunge hili la 12 litafuata nyayo za Bunge la 11. Na katika hili, napenda niliarifu Bunge hili Tukufu kuwa, kwenye miaka mitano ijayo, tutaendelea kuimarisha ulinzi na usimamizi wa madini yetu, (kama tulivyofanya kwa kujenga Ukuta Mirerani) kwa kuimarisha Sheria zetu ili madini yetu yasitoroshwe na Serikali kukoseshwa mapato.

Aidha, tunakusudia kuendelea kufanya majadiliano na wawekezaji wakubwa kwa kuzingatia mfano wa Makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick yaliyowezesha kuundwa kwa Kampuni ya Twiga Minerals Corporation.

Nchi yetu imebarikiwa kuwa na madini mbalimbali, ikiwemo dhahabu, almasi, Tanzanite, chuma, bati, nickel, copper, n.k.

"Aidha, tuna gesi aina mbalimbali, kama vile ethane, helium, ambayo hivi karibuni zimepatikana futi za ujazo bilioni 138 kwenye Ziwa Rukwa, ambazo zinaweza kuhudumia dunia kwa miaka 20.

Hii ndiyo sababu, kila siku nimekuwa nikisema, sisi sio masikini; sisi ni matajiri. Nchi yetu ni tajiri sana.

Lakini, kuhusu madini pia, kwenye miaka mitano ijayo pia tutaendelea kuliimarisha Shirika letu la Taifa la Madini (STAMICO) ili lishiriki kikamilifu kwenye shughuli za madini; kuwawezesha wachimbaji wetu wadogo, ikiwa ni pamoja na kuwatengea maeneo ya uchimbaji, kuwapatia mafunzo, mikopo pamoja na vifaa.

Na katika natambua kuwa, wapo baadhi ya watu wamepewa leseni za utafiti na uchimbaji lakini hawajazifanyia kazi; tutazifuta leseni zao, na maeneo hayo kuyagawa kwa wachimbaji wengine, hususan wachimbaji wadogo. Wachimbaji wadogo ni muhimu sana katika kukuza sekta ya madini.

Tutaendelea pia kuimarisha masoko ya madini pamoja na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji, uyeyushaji, usafishaji na utengenezaji wa bidhaa za madini.

Tunataka madini yachimbwe hapa Tanzania, yachenjuliwe, yayeyushwe na kisha bidhaa za bidhaa za madini zitengenezwe hapa hapa Tanzania; na ndipo ziuzwe nje ama watu kutoka nje waje kununua bidhaa za madini hapa nchini.

"Ni imani yetu kuwa, kutokana na hatua tulizopanga kuzichukua sekta ya madini itaweza kuchangia angalau asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025,"amefafanua Rais Dkt. Magufuli

Post a Comment

0 Comments